Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Azam FC: Ubingwa wetu upo mikononi mwa Biashara

Azam Pol Azam wanajiandaa kukipiga na Polisi Tanzania

Mon, 21 Feb 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kesho Azam FC itahitimisha mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Bara msimu wa mwaka 2021-2022 kwa kucheza mchezo wake wa mwisho dhidi ya Biashara United huku Kocha Msaidizi wa kikosi hicho, John Matambala akitamba kuwa wanahitaji ushindi ili kupalilia safari yao ya kushinda ubingwa msimu huu.

Mchezo huo namba 119 utapigwa saa 10 jioni katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza ambapo Biashara United watakuwa wenyeji baada ya uwanja wao wa Karume mjini Musoma kuwa kwenye ukarabati.

Akizungumzia maandalizi ya timu hiyo katika mkutano na waandishi wa habari leo jijini Mwanza, Matambala amesema wanatambua umuhimu wa mchezo huo katika kutimiza malengo yao ndiyo maana walifika mapema jijini hapa tangu Februari 16 ili kufanya maandalizi mazuri yatakayowapa ushindi.

"Tunafahamu umuhimu wa mchezo huu ndiyo sababu tulifika mapema huku Mwanza kujiandaa vizuri zaidi na maandalizi yetu yanakwenda vyema hadi sasa kuhakikisha tunapata ushindi,"

"Matumaini ya ubingwa yapo na tunahitaji kuendelea kushinda na kufanya vizuri ili tuwe kwenye mbio za ubingwa na kusogea Kwenye mazingira mazuri ya ushindani wa ubingwa," amesema Matambala.

Nahodha wa kikosi hicho, Aggrey Morris amesema kwa sasa timu yao ina morali kubwa na imeimarika baada ya kuanza kwa kusasua mwanzoni ambapo wachezaji wako tayari kutimiza wajibu wao kwa kuipa ushindi katika mechi zao zote zilizo mbele yao.

"Wachezaji tuko vizuri tunahitaji kesho kushinda, mwanzo tulianza kwa spidi ndogo lakini sasa morali iko juu tunazidi kuimarika kuhakikisha tunatimiza malengo ya kushinda mechi zetu na kupata ubingwa," amesema Morris.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live