Klabu ya Azam imesema kuwa kocha wao Mkuu, Youssouph Dabo raia wa Senegal anavyo vigezo vya kitaaluma vya kusimama katika benchi kuongoza timu hiyo kwenye michezo yake tofauti na taarifa iliyotolewa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuwa Dabo ni miongoni mwa makocha ambao hawana sifa hizo.
Hayo yameelzwa na Mkuu wa idara ya Habari na Mawasiliano Azam FC, Thabiti Zakaria 'Zakazakazi' wakati akihojiwa na chombo kimoja cha habari kuhusu taarifa hiyo ya TFF.
"Kuna taarifa zilichelewa kufika TFF, kwa hiyo wakati wanaandika hiyo Orodha na vyeti ambavyo walikuwa navyo mkononi, cheti cha Dabo ambacho kinamfanya astahili kuwemo kwenye benchi yaani ile "Not Allowed" iondolewe iwe "Allowed" au iwe "Cleared".
"Kilichelewa kufika, kwahiyo wao wakatoa orodha kwa kile ambacho walikuwa nacho mkononi, kimsingi ni kwamba Youssouph Dabo ana Diploma A ya UEFA alisoma Paris Ufaransa," amesema Zakazakazi.
Taarifa iliyotolewa jana na TFF ilimtaja Dabo pamoja na makocha wengine wakiwemo Kocha Msaidizi wa Simba na kocha wao wa viungo, Kocha Msaidizi wa Yanga, Mussa Ndaw na Kocha wa Coastal Union Mwinyi Zahera kuwa hawana vigezo vya kusimama kwenye benchi.