Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ayubu Lyanga afunguka ya moyoni

Ayoub Lyangaaaa Ayubu Lyanga afunguka ya moyoni

Wed, 25 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kama hujapata nafasi ya kukaa chini ukapiga naye stori za hapa na pale winga wa Azam FC, Ayubu Lyanga, kwa haraka haraka unaweza kudhani ni mtu flani anayejisikia kumbe ni tofauti kabisa, jamaa ni mpole na mcheshi.

Mwanaspoti lilifunga safari hadi Chamazi ambako ni makao makuu ya Klabu ya Azam lengo likikuwa ni kufanya mahojiano na wachezaji tofauti akiwemo Ayubu, na ndipo lilipogundua kuwa ni mchezaji wa aina gani baada ya kupata wasaa wa kuzungumza naye.

Huyu ni mchezaji anayezungumza kwa vituo kama vile hataki, lakini mwenye majibu makini ya kile anachoulizwa ilhali pia pia ni mkweli wa kufunguka kama kuna jambo linamkera.

Katika mahojiano hayo mchezaji huyo kafunguka mambo mengi kuhusiana na maisha yake ya soka akijibu kwa nini aliamua kuichagua Azam mbele ya Simba na Yanga ambazo zilimpelekea ofa kipindi kile zikimtaka.

“Wakati Azam inaleta ofa na klabu kongwe zilihitaji huduma yangu binafsi sikuona kama itakuwa sawa kwangu kuzichagua timu hizo kabla sijakomaa kisawasawa. Kulingana na ushindani wa namba wa wachezaji wanaowasajili nikaona timu niliopo kwa sasa ni sahihi sana kunijenga na imenijenga,” anasema.

PANDA, SHUKA

Kiwango chake kinapanda wakati mwingine hushuka, na hapa anafanunua sababu ya hilo akisema: “Hayo ni maisha ya kawaida kwa mchezaji. Binafsi hilo haliwezi kuniondoa kwenye mapambano ya kuisaidia timu na sababu kubwa ni changamoto ya majeraha ya hapa na pale ambayo yanapita kisha naendelea na majukumu kama kawaida.”

Anasema ukifika muda wake wa kucheza huwa anafanya kazi yake kwa bidii akiamini anapopewa nafasi kocha anakuwa anataka huduma yake aisaidie timu kufikia malengo.

“Malengo ninayo kibao mbele ni ya timu, kwani ndani ya malengo ya timu na yangu binafsi ni rahisi kutimia nikiwa na maana ukiona timu imefanikiwa, basi wachezaji wanacheza kwa viwango vya juu,” anasema.

Ayubu akiwa kwenye kiwango chake ni mtaalumu wa kupiga mipira ya kutenga na hapo anatoa elimu kidogo.

“Ninapopewa nafasi hiyo najipa utulivu wa kutafakari cha kufanya kisha napiga mpira kwenye uwazi wa mguu kwa maana kutoufikisha kwenye kidole gumba. Ukipiga hivyo unakuwa unakwenda kwa nguvu.”

Anaongeza: “Napenda kujiongeza zaidi ya kile kocha anachoniambia. Mfano anaweza akanielekeza eneo la kupiga ikitokea hakuna wachezaji wa kuwapa mpira eneo hilo unafanyaje, lazima akili yako ifanye kazi kubwa ya kuhakikisha unapiga mpira wa faida na sehemu iliyo na wenzako.”

KAKA’KE DANIEL

Ayubu anaelezea maisha anayoishi na kaka yake, Daniel ambaye anaichezea JKT Tanzania, kwamba ni zaidi ya washikaji, lakini wawapo kazini hawana mchezo kila mmoja anakuwa anatetea kibarua chake.

“Nachojifunza kwa kaka yangu Danny ana nidhamu kubwa ya soka na maisha yake kwa ujumla. Huwa namshuhudia sana tukiwa mapumziko staili yake ya maisha, ni mtu anayependa kufanya vitu kwa unyoofu na kuzingatia muda,” anasema.

“Kuna wakati ananishauri vitu gani nivifanye ili nizidi kuwa bora kwenye majukumu yangu. Ana kauli yake anayosema mpira ukiuheshimu utakuheshimu, lakini tuwapo uwanjani tukikutana kwenye mechi kila mtu anakuwa upande wake anaoufanyia kazi.”

Anaendelea kusema: “Pia kuna utani inapotokea ambaye timu yake imefungwa, ila jambo la msingi zaidi ni kujenga maana tumechagua soka liwe sehemu la kutuingizia kipato cha kujikimu na maisha na ikitokea nikipata changamoto huwa anaumia sana, hata mimi naumia nikiona anapitia kitu cha kumhuzunisha.”

AZAM NA MAISHA

Ingawa hakutaka kuweka wazi ni mambo gani ya maendeleo kayafanya kupitia pesa anazopata Azam FC, lakini anakiri kuwa na hatua kubwa kimaisha tofauti na mwanzo kabla hajawa na timu hiyo.

“Siyo muumini wa kusema nimefanya hiki na kile, lakini Azam imenipa hatua fulani ya maendeleo. Pia imefanya kipaji changu kizidi kukua na kujulikana kwa watu, hivyo timu hiyo ni sehemu ya maisha yangu,” anasema.

“Azam ni timu kubwa, ina wachezaji wazawa na wageni wenye ushindani mkubwa, hivyo inanifanya nisibweteke kujituma na kufanya kazi kwa bidii ili huduma yangu iendelee kuwa muhimu kikosini.”

Ndani ya kikosi hicho anamtaja straika Prince Dube kuwa miongoni mwa wachezaji bora katika Ligi Kuu Bara kulingana na aina yake ya uchezaji.

“Dube anajua mpira. Ukifuatilia aina yake ya mabao anayoyafunga utanielewa ndio maana namuona ni straika bora kwa muda wote ambao amecheza nchini,” anasema.

Pia anasema hatamsahau aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Aristica Cioaba akitaja sababu kuwa, “sina maana kwamba makocha wengine ni wabaya, ila Cioaba kwangu alikuwa ananiambia nina kipaji kikubwa nipambane nitafika mbali. Wakati mwingine ukicheza chini ya kiwango anakufuatilia kujua changamoto zako ni zipi na anakupa moyo ili uzivuke na zisikuondoe kwenye mstari wa kazi.”

UNYONGE KWA SIMBA

Ayubu anasema angalau nyota wa Azam FC walipumua na kuondoa unyonge baada ya kuifunga Simba msimu uliopita, kwani mashabiki wa soka nchini walikuwa wanawachukulia kuwa ni tawi la Msimbazi, jambo analodai lilikuwa linamuumiza.

Mechi ambayo Azam FC iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Simba ilipigwa Mei 7, 2023 wafungaji wa mabao wakiwa Lusajo Mwaikenda katika dakika ya 22 na Prince Dube ile ya 75, ilhali kwa Simba alikuwa Sadio Kanoute. “Kila tulipokuwa tunakutana na Simba tunafungwa, jambo lililowafanya (mashabiki) wengine waamini sisi ni kama tawi la Simba kitendo ambacho kinaumiza sana wachezaji. Siku ambayo tuliifunga nilifurahi sana na ilipunguza kutuona sisi ni Simba. Ile ni kazi ambayo tunaingia 11 kwa 11 anayefanikiwa kupata matokeo ya ushindi bahati inakuwa upande wake,” anasema.

Japokuwa anakiri Simba na Yanga ni klabu kongwe na zenye ushindani mkali, lakini pamoja na hilo haziwafanyi waone wanastahili kufungwa nazo, badala yake anaamini na wao watakuwa wanapata ushindi dhidi yao.

“Msimu uliopita tulipoteza kwa Yanga, ila naamini awamu hii hatutakubali unyonge tena. Tutapambana na sisi kuwaonyesha tupo imara na tunahitaji kuwafunga,” anasema.

Kitu kingine kinachomuumiza ni kuona timu yake inaondolewa mapema kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF) kila inaposhiriki na kwa hilo anatamani kuona siku moja wanafika fainali.

Chanzo: Mwanaspoti