Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ayoub anayepita njia za Msuva

Msuva Lakred Msuva na Ayoub Lakred pichani.

Thu, 21 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Maisha bila unafiki hayaendi.”’ Huu ni msemo maarufu anaopenda kuutumia mwandishi na mchambuzi wa soka wa Gazeti la Mwanaspoti, Edo Kumwembe.

Huenda Edo aliamua kuutumia kwa kushuhudia mashabiki wa soka nchini walivyo. Wanaishi kinafiki. Wamekuwa kama ndumilakuwili. Leo wanamponda mchezaji au kiongozi, halafu kesho wanageuka na kumshangilia kwa mapambio.

Ukitaka kujua maisha ya mashabiki hayaendi bila unafiki rejea mkasa uliowahi kumpata Simon Msuva. Alipotua Yanga 2012 alikuwa akiponda sana na mashabiki. Alikuwa akizomewa kuliko mchezaji yeyote, licha ya kuisaidia uwanjani. Bahati nzuri, Msuva hakujali. Aliiamini miguu yake na kuendelea kupambana, kiasi cha kuja kuwa nyota tegemeo Jangwani. Alifunga na kuasisti mabao ya kutosha yaliyoipa Yanga ufalme wa Ligi Kuu na michuano ya kimataifa kwa misimu kadhaa kabla ya kuuzwa Morocco.

Wale waliokuwa wakimzomea na kumponda ndio baadae walikuwa wakishindana kubeba viroba vya mchele uwanjani kumzawadia Msuva, huku wakishangilia na kumpigia makofi kumtukuza.

AYOUB NAYE

Unafiki huohuo aliokuwa akifanyiwa Msuva miaka zaidi ya 10 iliyopita, sasa umejirudia  kwa kipa wa Simba, Ayoub Lakred.

Kipa huyu alisajiliwa msimu huu kutoka FAR Rabat ya Morocco akitoka kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya huko ‘Batola Pro’. Alipopolewa mno. Alisakamwa na kuandamwa kiasi cha kumuonea huruma. Mashabiki walimuona kipa miyeyusho. Wakamponda sana. Wapo waliodiriki hata kumzoea uwanjani na wengine wakitaka afyekwe kwenye dirisha dogo.

Walimuona mchezaji wa daraja la chini na wengine wakaleta ubaguzi juu yake. Lakini mwamba kumbe alikuwa akiwasoma tu. Alikuwa akizoea mazingira na kisha kujivua gamba kuonyesha rangi yake halisi.

Ndio mashabiki walewale waliompopoa baada ya kufungwa kwenye sare mbili dhidi ya Power Dynamos ya Zambia, leo wanaliimba jina lake. Wamesahau dharau walizomfanyia kipa huyo mwenye umri wa miaka 28. Baadhi wameanza kukiri hadharani kwamba walimkosea adabu kwa kumponda, ilihali kumbe ni bonge la kipa.

NAMBA ZINAMBEBA

Achana na mechi za Ligi Kuu Bara, Lakred ndiye aliyesimama kwenye mechi  mbili za raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Dynamos. Alijifunga bao la kwanza la Wazambia kwenye mechi ya ugenini mjini Ndola, Zambia, lakini alichangia kuivusha timu makundi.

Katika mechi nne zilizochezwa hadi sasa katika Kundi B, zikiiweka Simba nafasi ya pili, Ayoub amedaka zote ikiwa na maana ya kutumika kwa dakika 360.

Alianza mechi ya kwanza nyumbani dhidi ya Asec Mimosas ya Ivory Coast iliyoisha kwa sare ya bao 1-1 kabla ya kwenda kupata ‘clean sheet’ ya kwanza katika Jiji la Francistown, Botswana wakati Simba ikitoka suluhu na Jwaneng Galaxy.

Simba ilipokwenda Marrakech, Morocco katika nchi aliyozaliwa, Ayoub alifanya makubwa ikiwamo kudaka penalti ya kipindi cha kwanza na kuokoa michomo kadhaa ya nyota wa Wydad Casablanca, licha ya kuruhusu bao moja jioni, wenyeji wakishinda 1-0. Ndio maana haikuwa ajabu kuwa mchezaji namba mbili wa Simba  aliyepewa alama nyingi ktika mchezo huo akivuna 6.9 nyuma ya kinara Che Malone aliyepata 7.1. Hii ni kwa mujibu wa mtandao wa flashscore.

Juzi jioni, Simba ilirudi nyumbani kuikaribisha Wydad kwenye mechi ya marudiano na Simba ilishinda mabao 2-0 yote yakifungwa na Willy Onana, lakini kazi kubwa ikifanywa na Ayoub.

Kipa huyo aliokoa michomo hatari mitano ambayo kama angekuwa goigoi, Mnyama angepoteza Kwa Mkapa.

Kuonyesha kiwango alichoonyesha hakikuwa cha kubahatisha, mwamba huyo alipewa alama 7.8 akiwa tena ni mchezaji namba mbili wa Simba kupata maksi nyingine nyuma ya mfungaji wa mabao yaliyoibeba Simba, yaani Onana aliyevuna alama 8.3 akiwa ndiye nyota wa mchezo. Hii ni kwa mujibu wa flashscore, huku Google ikimpa 4.6 akilingana na Henock Inonga wakiwa ndio vinara wa Simba kwenye mchezo huo, huku Onana akipewa 4.3. Kwa sasa, rekodi zinaonyesha Ayoub ana clean sheet mbili za Ligi ya Mabingwa Afrika na mbili za Ligi Kuu Bara, kuonyesha kadri anavyoendelea kuchezeshwa anazidi kuwa mtamu na kujiamini langoni. Kinatakiwa kitu gani kingine kwa kipa wa kigeni kama huyo?

APUNGUZE PRESHA

Kwa jinsi anavyocheza ni wazi Ayoub amepunguza presha za awali na kawashusha presha mashabiki na wapenzi wa klabu hiyo waliokuwa na wasiwasi naye na pia kukosekana muda mrefu kwa kipa namba moja, Aishi Manula aliye majeruhi

Manula aliyeumia kwenye mechi ya ASFC dhidi ya Ihefu iliyopigwa Aprili, mwaka huu, alirejea katika Kariakoo Derby na kutunguliwa mabao matano na Yanga kabla ya kujitonesha jeraha akiwa timu ya taifa na kuibua presha Simba.

Hata hivyo kwa kazi kubwa aliyoionyesha Ayoub kwenye mechi nne zilizopita za CAF na kuiweka Simba katika nafasi ya kuendeleza rekodi ya kucheza robo fainali, ni wazi anaweka rehani nafasi za makipa wenzake kuanzia Manula mwenyewe hadi Ally Salim na Hussein Abel ambao kwa sasa wanasugua benchi.

Kitu kizuri ni kwamba hata wakati anashambuliwa na mashabiki, enzi akidaka chini ya kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’ alikuwa akikingiwa kifua na kocha wa makipa, Dani Cadena aliyekuwa akisisitiza Ayoub ni bonge la kipa, ila anaangushwa na ugeni wa mazingira ya soka nchini.

Kifupi ni kwamba Ayoub kaamua kupita njia zile zile alizopita Msuva za kuiacha mikono yake ifanye kazi uwanjani, badala ya kutumia mdomo kuwajibu waliompopoa. Huenda naye akabebewa viroba vya mchele, kama pongezi  kwa kazi kubwa anayoifanya, si maisha bila unafiki hayaendi? Tusubiri tuone!

Chanzo: www.tanzaniaweb.live