Kikosi cha wachezaji 23 wa Simba SC na benchi la ufundi pamoja na viongozi wengine wa timu hiyo kinatarajia kuondoka nchini kesho alfajiri kuelekea nchini Ivory Coast kwa ajili ya mchezo wa marudiano wa hatua ya makundi dhidi ya ASEC Mimosas.
Hayo yamesemwa leo na Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Simba, Ahmed Ally wakati akizungumzia maandalizi ya mchezo huo unaotarajiwa kupigwa Ijumaa, Februari 23, 2024 nchini Ivory Coast huku kipa Ayub lakred na kiungo mshambuliaji, Willy Onana wakiachwa Dar es Salaam.
“Tayari jopo la kwanza la maofisa kutoka Simba likiongozwa na mratibu Abbas Ally Suleiman wameshatangulia Ivory Coast kwa ajili ya kuandaa taratibu zote ili timu ikifika, kila kitu kiwe katika msitari wake. Kwa hiyo kiufupi tupo katika maandalizi ya mwisho kuelekea mchezo huo.
“Tunatarajia kusafiri na wachezaji 23 pamoja na benchi la ufundi, wapo wachezaji kadhaa ambao watakosekana kutokana na game plan ya mwalimu. Wachezaji watakaokosekana ni pamoja na Ayoub Lakred kwa sababu ana kadi tatu za njano ambapo kikanuni hawezi kucheza wala hatuwezi kusafiri nae.
“Vilevile tutamkosa Willy Onana kwa vile bado ana majeraha, lakini wachezaji wengine wote wapo vizuri na tayari kwa mapambano na kuhakikisha tunapata ushindi katika mchezo huo,” amesema Ahmed Ally.