Kwa mara ya kwanza nimemtazama kipa mpya wa Simba, Ayoub dhidi ya Dynamos. Simba wamelamba dume. Pamoja na kufungwa nyavu zake, lakini unaona sifa zote za kipa bora ndani yake.
Uwezo wa kuongea na mabeki wake ni wa hali ya juu. Ugawaji wa mipira ni levo nyingine. Hana papara langoni, miguu yake ni ufundi mtupu. Ayoub Lakred ni fundi kwelikweli. Hapa Simba wamepata mtu ambaye Aishi Manula anapokosekana kuna mtu wa kuziba pengo lake.
Bado Manula atabaki kuwa kipa bora kuzalishwa nchini miaka 10 ya hivi karibuni, lakini Simba wanaonekana watakuwa imara pale anapokosekana.
Aishi ni kipa aliyepitia mikikimikiki mingi ya nje na ndani ya uwanja. Ni ngumu sana kumpeleka benchi kirahisi, lakini Ayoub anajua. Huyu Mmorocco anajua sana mpira na Simba wamefanya uamuzi mzuri kumsajili.
Kufungwa kwenye mpira sio uwezo tu wa kipa, ni uwajibikaji wa kila idara. Sina lawama yotote kwake. Ni suala la muda tu. Atakuja kuimbwa muda sio mrefu. Najua na wewe unalipata nafasi ya kutazama mechi hebu niambie namna ulivyomtazama kipa mpya wa Simba, Ayoub.