Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Awesu anukia Yanga, kazi kwa Gamondi na Hersi

Awesu Yangaaaa Awesu anukia Yanga, kazi kwa Gamondi na Hersi

Mon, 19 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kiungo fundi kutoka Visiwa vya Marashi ya Karafuu Zanzibar, Awesu Ally Awesu anayekipiga katika Klabu ya KMC, ametajwa kutakiwa na Klabu ya Yanga katika dirisha kubwa la usajili baada ya msimu huu kumalizika.

Hayo yamesemwa na Ofisa Habari wa Klabu ya Yanga, Ally Kamwe akizungumzia uwezo mkubwa aliouonesha mchezaji huyo kwenye mchezo wa Ligi uliopigwa juzi, dhidi ya KMC, katika Dimba la Jamhuri Morogoro ambapo Yanga ilishinda kwa mabao 3-0.

Baada ya mchezo huo kumalizika, Kamwe alimfuata Awesu na kumpongeza kutokana na uwezo mkubwa aliouonesha kwenye mchezo huo huku akidai kuwa atamshawishi Rais wa Klabu hiyo, Injinia Hersi Said amsajili katika dirisha kubwa.

“Awesu nimemfuata na nimemwambia hongera kwa mechi nzuri, amecheza vizuri sana, yani kwenye kundi la samaki wadogo, samaki mkubwa anaonekana. Kimsingi Awesu kwa quality yake anatakiwa sasa atoke KMC aende timu kubwa zaidi.

“Nimemwambia Awesu daraja lako sasa hivi na KMC ni mbingu na ardhi, ameiacha mbali sana KMC anatakiwa atoke sasa, kwa hiyo timu kubwa sasa tutamtazama Awesu.

“Kama nitapewa nafasi ya kukutana na Injinia Hersi Said na akanisikiliza ombi langu, katika machaguo ambayo nitamwambia aongeze ni 'Rastafari' Awesu Awesu, lazima aje kwenye timu ambayo inakusanya mashabiki milioni 35 wakiwemo hata wao KMC.

“Tunampongeza Awesu na mimi binafsi kama mwalimu wa mpira, nitakwenda moja kwa moja kumwambia Injinia Hersi kama kuna nafasi ya kiungo kuongeza dirisha kubwa, basi ni Awesu. Awesu angevaa jezi ya Yanga leo hii nyote mngesema ni ‘man of the match’, ameonekana peke yake kati ya wachezaji wote wa KMC,” amesema Ally Kamwe.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live