Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Awesu aliuza mafuta aje Dar, azikacha Simba, Yanga

Awesu Awesu Awesu Awesu

Mon, 4 Sep 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kwenye dirisha la usajili 2020/21 mojawapo wa majina yaliyoshtua ni la Awesu Awesu na kati ya timu zilizokuwa zikiwania saini yake ni Simba, Yanga na Azam FC.

Hata hivyo, Awesu alitua Azam na kuitosa miamba ya soka nchini Simba na Yanga akiwashangaza wengi walioamini angetua kwenye moja ya timu hizo kubwa.

Awesu ambaye alitokea Madini FC ya Arusha alikoonyesha ubora hadi kuwekewa mezani pesa na Azam, hivi karibuni alitembelea ofisi za gazeti hili zilizopo Tabata Relini na kufunguka mengi ikiwamo usajili huo na maisha yake kabla ya kucheza soka na kama hujui, alishauza mafuta ya nazi ili apate nauli ya kwenda Dar es Salaam kutafuta maisha.

ALIWAZA MUZIKI, AKAIBUKIA SOKA

Awesu anasema hakuwawahi kufikiria soka kwamba litamtoa kwani tangu mwanzo alikuwa akitafuta namna ya kufika Dar es Salaam ili kujiunga na kikundi cha dansi.

Katika jitihada za kukamilisha hilo, anasema ilimlazimu kutafuta pesa za kumfikisha Dar na ndipo alipoamua kuuza mafuta ya nazi.

Awesu ambaye ni mzaliwa wa Zanzibar, anasema alimshirikisha mama yake kwenye jambo hilo kwani ana ndugu Dar na aliona itakuwa rahisi kwake akifika.

“Nauli ya kuja kwa meli ya mizigo ilikuwa ni Sh7,000. Hakuna aliyenipa hivyo (pesa) nikajiongeza kwa kufanya biashara na baadaye kufika Dar,” anasema.

“Familia haikuwa na uwezo jambo pekee nililohitaji wakati huo ni kuondoka na kuanza maisha ya ndoto zangu kuwa mcheza muziki na sio mpira tena. Kuhusu kuibukia kwenye soka ni baada ya kuona mambo ya muziki hayaendi.

“Nilikubalika namna yangu ya uchezaji muziki kuliko soka, hiyo ikanifanya nichague njia moja ambayo niliifurahia zaidi.

“Nilipofika mjini mambo yalibadilika na kila nilipojaribu kutafuta nafasi (ya kucheza muziki) sikupata na ndipo nikaamua kujaribu soka kwa mara nyingine.”

AANZA SOKA, AJIPELEKA AZAM

Mchezaji huyo anasema alipofika Dar aliishi Kinondoni kwa mama mdogo na alikutana kaka aliyekuwa anacheza Azam U-20. Hilo lilimtamanisha kurudi kucheza soka baada ya kuona mambo hayaendi kwenye muziki na hasa jezi zake zilimvutia na kuhisi kuna kitu anaweza kufanya.

Anasema mazingira ya Azam FC kuanzia basi, wachezaji na miundombinu vilimvutia na kuamua kuanza jitihada za kwenda kwenye klabu hiyo.

“Kupanda gari na wachezaji wa Azam kulizidi kunichanganya na kutaka kuwa mmoja kati yao, hivyo juhudi zilianza upya.

“Niliamua kwenda kwenye majaribio yao nikiamini nitafanikiwa kuvuka ndani ya miezi mitatu ili niingie timu ya vijana na nilifanikiwa kuchaguliwa.”

ACHUJWA KIKOSINI, ARUDI MTAANI

Kwa masikitiko, Awesu anakumbuka jinsi alivyoachwa kwenye kikosi cha Azam baada ya jina lake kukatwa ndani ya muda mfupi baada ya taarifa kutoka za wachezaji kupunguzwa na kusababisha kuanza kuchukia soka.

Anasema: “Nililia sana na kugawa kila nilicho nacho nje ya geti la kambi tuliyokuwa tukiishi na kuapa sitarudia tena kujihusisha na soka.”

Mchezaji huyo anasema baada ya kutoka Azam alirudi kuanza maisha ya mtaani upya na mambo yalibadilika kwani hakuwa na la kufanya, kabla ya kupata taarifa kuwa kuna timu ya Makumbusho FC inahitaji huduma yake na ndipo alipojiunga nayo kwa makubaliano maalumu.

Hata hivyo, anasema hilo liliwezekana lakini maisha yalizidi kubadilika baada ya miezi sita ya kodi ya nyumba kumalizika.

“Niliwaomba wanilipie kodi kama mshahara wangu wa chumba kimoja na baada ya miezi sita kumalizika hawakuendelea tena na maisha yalibadilika,” anasema.

AZIKACHA SIMBA YANGA

Baada ya kuona mambo hayaendi Dar alitimkia Arusha na kujiunga na timu ya Madini FC.

“Niliamua kutimkia Madini FC na niliishi kambini, kwani sikuwa na uwezo wa kucheza na kurudi nyumbani.”

Akiwa Madini alionyesha kiwango safi kwenye mchezo dhidi ya Simba na kuanza kutajwa kabla ya miamba hiyo pamoja na Yanga kumuwekea ofa mezani.

Hata hivyo, timu hizo ziliweka ofa ndogo ambazo hazikumridhisha, kabla ya Azam kuja tena na ofa nono iliyomshawishi kujiunga nayo.

“Simba walitoa pesa ndogo ili kunisajili. Yanga waliwatuma wazee ambao mpaka sasa sijawaelewa walikuwa kina nani (kwa ajili ya kumshawishi).”

Baada ya kutua Azam, anasema pesa alizovuna kwa usajili alizitumia kununulia viwanja na gari analotembelea hadi sasa.

“Maokoto ya Azam yalinifanya nipate mafanikio haya niliyonayo na nikaamini kupitia soka naweza kuishi maisha ya ndoto zangu.”

“Niliapa kurudi kwa heshima Azam kwani kipindi naondoka najua tulitolewa ili waingie wengine, hivyo haikuwa haki, kwa sababu walijaribu kukatisha ndoto tulizozipambania kwa tabu sana.”

KMC ILIKUWAJE?

Awesu anasema kisa cha kuomba Azam kumtoa na kwenda KMC kwa mkopo ni kwa sababu hakuwa chaguo la kocha mpya wa kikosi hicho, baada ya kutumika kwa msimu mmoja. “Sikuwa chaguo la kocha mpya, hivyo sikuona umuhimu wa kuendelea kubaki na ndipo nilipoamua kutafuta timu itakayokuwa mjini na nitapata nafasi ya kucheza,” anasema.

“Niliichagua KMC kwani sikutaka kwenda mkoani na sikuwahi kufurahia maisha yangu ya soka nje na Dar es salaam.”

BATA LA KMC BALAA

Awesu anasema katika maisha ya soka amezunguka timu kadhaa, lakini furaha anayopata ndani ya KMC ni tofauti sana.

“Tunaishi kwa upendo, amani na kushirikiana kama familia ndio maana kila anayechezea kikosi kile lazima abaki na kumbukumbu njema,” anasema.

Anasema hakuna mchezaji asiyetaka kwenda kucheza soka nje ya nchi akilinganisha malipo ya nchini na huko.

Mchezaji huyo anasema fursa hizo zinakuja mara kadhaa, lakini zinashindwa kutimia kwa sababu mbalimbali ikiwamo malipo madogo

“Unalipwa pesa ndogo na ni ugenini huna ndugu atakayeweza kukusaidia kwa wepesi, hivyo lazima uwe na malipo mazuri yatakayokufanya uweze kuishi huko. Wachezaji wengi tunakwama hapo kwani matarajio yetu huwa ni makubwa kulinganisha na kile tunachowekewa mezani.”

ANAWAKUBALI WOTE

Awesu anasema hana mchezaji anayemkubali kuliko mwingine kwani wote wana vipaji ndio maana wanacheza na kuonekana.

“Nimeshindwa kuwa shabiki wa mtu yeyote kwani natambua namna ilivyo vigumu kufanikiwa katika maisha ya soka, hivyo siwezi kuona aliye bora. Kwangu nawaheshimu wote na ni rafiki wa kila mtu na safari yake ya soka,” anasema.

Chanzo: Mwanaspoti