Wakati kumtaja kiungo wa KMC FC, Awesu Awesu ametajwa kuwa katika rada za Yanga, Kocha Mkuu wa mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Miguel Gamondi, amefurahishwa na kiwango kilichoonyeshwa na straika wake, Joseph Guede.
Straika huyo raia wa Ghana alifungua akaunti yake ya mabao mawili Yanga ikipata ushindi wa magoli 5-0 katika mechi ya michuano ya Kombe la FA dhidi ya Polisi Tanzania iliyochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam juzi.
Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, ameiambia Nipashe Awesu yuko katika mipango ya timu yao kuelekea dirisha 'kubwa' la usajili litakalofunguliwa baadaye mwaka huu.
Kamwe amesema wakati umefika kwa Awesu kutoka KMC na kujiunga na timu 'kubwa' kutokana na uwezo aliokuwa nao katika kucheza soka.
Ofisa huyo ameenda mbali na kusema ikitokea Yanga watahitaji kiungo wa ndani, kiungo huyo atakuwa sehemu ya mipango ya usajili wao kwa kuushawishi uongozi kumnasa kutokana na kiwango bora alichonacho.
Naye Awesu amesema amefurahi kusikia kauli hiyo ya kuhusishwa na Yanga na kuongeza ni lazima kufanyike makubaliano rasmi ya pande zote tatu lakini upande wake hana tatizo.
Awesu amesema endapo Yanga na KMC zitakubaliana basi hana mashaka kwa sababu kazi yake ni kucheza mpira na atakuwa tayari kujiunga na Yanga au klabu yoyote ambayo wataafikiana na uongozi wa timu yake.
“Unajua kwangu ni faraja kubwa sana kuona kiongozi wa Yanga akinizungumzia, ubora wa kazi yangu unaonekana naamini huu ndio mwanzo mwingine wa safari yangu ya soka.
Bado nina mkataba hadi 2025, suala la kupendekeza jina langu kwa uongozi na benchi la ufundi kuwa sehemu ya nyota watakaowasajili hilo ni jambo zuri, lakini kwa sasa naheshimu mkataba wangu,” amesema Awesu.
Ameongeza mafanikio ni jitihada za mchezaji mwenyewe inatakiwa kupambana kwa ajili ya timu la sivyo wachezaji wakigeni watakuwa wanasajili kila kukicha.
Gamondi amesema anajivunia wachezaji wake kuonyesha uwezo mkubwa katika kila mechi na hii inaonyesha wanafuata vyema yale anayowapa kwenye uwanja wa mazoezi.
Amesema anaanza kuona washambuliaji wake wanafunga kama ilivyo kwa Guede, huku akimwambia asiwe na presha kwa sababu atafunga mabao mengi kutokana na mfumo ambao anataka kuutumia.
Ameongeza awali walipata mabao kupitia viungo hali imeanza kubadilika kwa kutumia mawinga imesababisha Guede kufunga magoli mawili katika mchezo huo wa FA.
“Kuhusu kutengeneza nafasi tunazipata nyingi, ukiangalia mechi ya Morogoro tulitengeneza nafasi zaidi ya 10 lakini tukapata mabao matatu, ninaimani tutaendelea kutengeneza nafasi na kutumia katika mechi zijazo kufunga idadi ya mabao mengi,” amesema kocha huyo.
Kuhusu maandalizi ya mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya CR Belouizdad, Gamondi, amesema wanatarajia kufanya vizuri katika mchezo huo kwa sababu malengo yao ni kusonga mbele.
“Utaratibu wangu ninafanya maandalizi hatua kwa hatua, baada ya mechi hii (Polisi Tanzania), tunarejea uwanjani kujiandaa na mchezo dhidi ya CR Belouizdad. Tulitaka kufuzu hatua ya makundi tukafanikiwa baada ya miaka mingi na sasa tunataka kutafuta matokeo mazuri yenye ushindi mkubwa ili mwisho wa siku tukacheza robo fainali, " Gamondi ameongeza.
Guede amesema anafurahi kuona amefunga mabao mawili ikiwa ni mara ya kwanza na anaimani sasa amezaliwa upya na atahakikisha anaendelea kupambania timu yake kupata matokeo mazuri.