Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Aussems hofu tupu, Kagere pointi moja safi

39645 Aussems+pict Aussems hofu tupu, Kagere pointi moja safi

Mon, 4 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Simba inaikabili Al Ahly leo katika mchezo wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika utakaofanyika Kwenye Uwanja wa Borg El Arab mjini Alexandria, huku kocha wa kikosi hicho Mbelgiji Patrick Aussems akisema matokeo yoyote atakayopata kwake poa tu.

Aussems tayari ameonyesha wasiwasi kabla ya mchezo huo kwani alisema kwamba: “Niwe mkweli. Sidhani kama tunaweza kupata pointi kutoka kwa Al Ahly. Mkazo wetu ni kukusanya pointi nyumbani.

“Huwa sipendelei ndoto. Hatuwezi kupata pointi hapa dhidi ya Al Ahly kwa sababu watapata penalti, mchezaji wetu mmoja ataonyeshwa kadi nyekundu na pia watapewa bao la kuotea,” alisema Aussems saa chache kabla ya mchezo.

Kauli ya Aussems ambayo ameitoa kupitia kituo cha luninga cha Sada-El-balad inaendana na rekodi ya Al Ahly katika mechi tatu za mwisho ilizocheza uwanja wa nyumbani katika Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Esperance, Jimma Aba Jifar na AS Vita.

Timu hiyo ilipata penalti tatu na mchezaji mmoja wa timu pinzani alionyeshwa kadi nyekundu.

Pia rekodi mbaya ya Simba dhidi ya timu za uarabuni inaweza kuwa imempa wasiwasi Aussems kwani timu hiyo katika mechi 10 ilizokutana na timu kutoka Misri au Ukanda wa Kaskazini mwa Afrika,imetoa sare mara moja na kupoteza mechi tisa ndani ya dakika 90 za mchezo.

Wakati Aussems akisema hayo mshambuliaji wa timu hiyo Meddy Kagere amesema wataingia uwanjani leo kusaka pointi moja tu kwani kupata ushindi mbele ya timu hiyo ni kazi ngumu.

“Ukiangalia hii ligi inavyokwenda hasa kundi letu kila mmoja anapambana kupata pointi tatu nyumbani.Hivyo tunachotafuta kwenye mchezo huo ni pointi moja tu na kama ikitokea tukashinda tutamshukuru Mungu ingawa ni kazi ngumu kushinda dhidi ya Al Ahly kwao”alisema Kagere.

Kagere ambaye anashika nafasi ya pili katika orodha ya wafungaji bora wa Ligi ya Mabingwa Afrika akiwa amefunga mabao matano alisema muhimu ni kila mchezaji kujituma, kushirikiana ili kuhakikisha wanafanya vizuri katika mchezo huo.

Miamba hiyo ya Misri inajivunia uwepo wa Salah Mohsen, Hesham Mohamed na usajili mpya, Geraldo naye atakuwepo baada ya kuwa majeruhi kwa muda.

Mwamuzi.

Mechi hiyo Misri itachezeshwa na mwamuzi Maguette N’Diaye kutoka Senegal ambaye hana rekodi nzuri kwa timu zinazocheza ugenini dhidi ya klabu kutoka uarabuni

Rekodi zinaonyesha kuwa ni vigumu kwa timu kutoka Uarabuni kupoteza mechi ya nyumbani kwenye mashindano ya Afrika kwa ngazi ya klabu pindi inapochezeshwa na N’Diaye.

Katika msimu wa 2018 na huu wa 2018/2019, N’Diaye amechezesha jumla ya mechi tisa kwenye ardhi ya Uarabuni, ambapo kwenye mechi hizo tisa, timu mwenyeji iliibuka na ushindi mara saba na mechi mbili ziliisha kwa sare.

Moja ya mechi ambayo N’Diaye alilaumiwa kwa kuwabeba wenyeji ni ule wa kwanza wa fainali ya Kombe la Shirikisho baina ya wenyeji Raja Casablanca ya Morocco na AS Vita ya DR Congo.

“Mwaka 2003 tulipocheza na Zamalek ndani ya dakika 25 kipindi cha kwanza safu yote ya ulinzi, kuanzia kipa hadi kiungo mkabaji ulipewa kadi za njano na yote mwamuzi alifanya hivyo kutupunguza kasi, tulivyorudi kipindi cha pili tuliambiana tubadilishe aina ya uchezaji, tukabe kwa nguvu tuzuie mpira lakini tusiwaguse na tulishukuru mpaka mpira unaisha tunashinda ile mechi hakuna mchezaji aliyepata kadi nyekundu”alisema Pawasa.

Wachezaji wa kuchungwa

Simba inatakiwa kuwa makini na mshambuliaji wa Al Ahly Nasser Maher mwenye mabao mawili na Marwan Mohsen mwenye bao moja.

Pia timu hiyo ina beki mahiri Ali Maaloul mwenye bao moja katika mashindano hayo.



Chanzo: mwananchi.co.tz