Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Aussems aipigia hesabu Mbabane

29544 Pic+simba TanzaniaWeb

Fri, 30 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Licha ya Simba kupata ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Mbabane Swallows ya Swaziland katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Kocha Patrick Aussems, amesema hawapaswi kubweteka kwenye mechi ya marudiano Jumanne wiki ijayo.

Akizungumza Dar es Salaam, Aussems alisema Mbabane siyo timu ya kubeza kwa kuwa inaundwa na kikosi imara ambacho kilitoa ushindani mkali katika mchezo wa juzi.

Aussems, raia wa Ubelgiji, alisema wanatakiwa kujipanga kurekebisha kasoro zilizojitokeza katika mchezo huo ili kujiweka katika nafasi nzuri kwa mchezo ujao.

Alisema mchezo ulikuwa mgumu na haikuwa kazi rahisi kupata ushindi na mabao waliyofunga yalitokana na bahati kwa kutumia vyema kasoro za mabeki wa Mbabane.

“Haukuwa mchezo rahisi, nawapongeza wachezaji wangu walitumia vizuri nafasi, tunatakiwa kujipanga vyema kwa mchezo wa marudiano,” alisema Aussems.

Nahodha msaidizi wa Simba, Mohammed Hussein ‘Zimbwe Junior’ alisema mchezo ulikuwa mgumu kwa kuwa Mbabane ni timu bora, hivyo watakwenda Swaziland kwa tahadhari kubwa.

Simba ambayo itakuwa ugenini Desemba 4 kwa mchezo wa marudiano, inapaswa kufanyia kazi uimara wa Mbabane na pia upungufu wao ili kupata matokeo mazuri yatakayowavusha kwenda raundi ya kwanza.

Simba inahitaji sare ama ushindi wa aina yoyote ile ili kusonga mbele ambako itakutana na mshindi baina ya Nkana Red Devils ya Zambia au UD Songo ya Msumbiji.

Uwezo binafsi wa mchezaji mmoja mmoja wa Mbabane walioonyesha katika mechi ya juzi Jumatano, ni sifa moja ya msingi ambayo Simba inapaswa kuifanyia kazi vinginevyo inaweza kugharamika.

Mbabane licha ya kuzidiwa kitimu na Simba, nyota wake mmoja mmoja walionyesha uwezo mkubwa wa kukaa na mpira kwa muda mrefu, kujiweka kwenye nafasi, kupiga chenga na pasi zilizokamilika kwenda kwa walengwa, jambo ambalo lilionekana kuwapa shida Simba katika muda fulani.

Wachezaji hao wa Mbabane walionyesha utulivu walipokuwa na mpira lakini hata walipopoteza waliwahi kuziba njia za Simba kupenyeza mipira kwenda kwenye lango lao jambo linaloweza kuwabeba kwao.

Pia Mbabane inaonekana kuwa tishio zaidi inapofika langoni mwa wapinzani wao kwa kuwa katika mchezo wa juzi, mashambulizi machache waliyofanya yalionekana kuwa na madhara kwa wenyeji wao kuliko yale ambayo Simba ilipeleka langoni mwao.

Lakini pamoja na sifa za Mbabane, Simba inatakiwa kufanyia kazi kasi ya wachezaji wake hasa pale wanapokwenda kushambulia kwa kuwa mara kadhaa wamekuwa wakikosa mabao kutokana na mchezaji husika kushindwa kuiwahi pasi kwa haraka.

Upande wa kulia alikocheza Gyan Nicholas ndiko kumeonekana kasi kupungua zaidi, Mghana huyo amekuwa hanyumbuliki kwa haraka kama ambavyo Shomari Kapombe ambaye amekuwa akicheza upande huo mara kwa mara huwa na kasi na uwiano mzuri wa kushambulia na kuzuia.

Gyan amekuwa na tatizo la kupiga krosi nzuri na haraka ambazo zingekuwa zinaipa timu yake mabao mengi. Kasoro hii ipo hata kwa beki wa kushoto Mohammed Hussein.

Simba pia imekuwa ikikabiliwa kasoro ya ya kushindwa kukaba na pindi mpira unapokuwa kwa wapinzani wao jambo ambalo linaweza kuwasaidia Mbabane pindi watakapokuwa kwao iwapo haitafanyiwa kazi na kurekebishwa.

Pamoja na kuibuka na ushindi mnono wa mabao manne, bado safu ya ushambuliaji inakuwa inababaika kila inapopata nafasi za kufunga ambapo ama imekua ikipoteza kwa kupiga nje au kuokolewa na walinzi wa wapinzani.

Lakini pia benchi la ufundi la Simba linapaswa kuumiza kichwa kujilipua kutowapaga washambuliaji John Bocco, Emmanuel Okwi na Meddie Kagere ambao mara kwa mara hushindwa kuelewana wanapoanza pamoja katika kikosi.



Chanzo: mwananchi.co.tz