Kocha wa AFC Leopards, Patrick Aussems, anayejulikana kwa kusema yaliyo moyoni bila ya kupepesa macho, alisema marefa bora wanaochezesha Ligi Kuu Kenya ni wanawake.
Kauli hiyo ya Aussems imekuja baada ya timu yake kutoka sare tasa na Nzoia Sugar mechi iliyopigwa mwishoni mwa wiki Uwanja wa Sudi kaunti ya Bungoma.
“Kusema kweli soka la Kenya haina marefa wa viwango, yaani kukiwa na presha kidogo tu kutoka kwa mashabiki au benchi la wapinzani, mnaona wakihaha na kuanza kufanya maamuzi ya kimapendeleo. Kwangu mimi marefa bora niliowaona Kenya hadi sasa ni marefa wa kike,” alisema.
Aussems alimshushia lawama refa aliyechezesha mechi yao dhidi ya vinara wa ligi, Nzoia Sugar, akisema alikua na nia ovu dhidi ya Ingwe.
Kocha huyo raia wa Ubelgiji alisema refa huyo ndiye aliyechezesha mechi yao dhidi ya Wazito FC wiki mbili zilizopita na kupoteza kwa mabao 2-1.
“Alifurahia sana baada ya sisi yetu kupoteza mchezo huo na kwenye mechi yetu ya Jumapili, alijaribu tena kila mbinu kuhakikisha wapinzani wanashinda kwani kila kulipotokea fursa alitaka kuwapa wao lakini alichokusudia haikuwezekana,” alisema Aussems.
Kauli ya Aussems inaendana na tetesi zilizoshamiri kwasasa kuwa marefa wengi nchini wanahusishwa na upangaji matokeo.