Baada ya Abdelhak Bechikha kuachana na Simba kwa kile kilichotajwa ana matatizo ya kifamilia, kocha wa zamani wa timu hiyo, Patrick Aussems amesema tatizo la Simba ni lile lile.
Aussems aliyeinoa Simba kuanzia Julai 2018 hadi Novemba 2019 amesema tatizo la Simba kutodumu na makocha wengi ni viongozi kutokuwa waadilifu jambo ambalo alilolisema wakati anaondoka.
"Kuna sababu nyingi za makocha kuondoka, lakini kwa Simba nadhani kuna shida kwenye uongozi kutokuwa waadilifu 'professional'. Hilo sio tatizo la Simba tu, bali Afrika nzima viongozi wanataka kuingilia majukumu ya benchi la ufundi wakitumia vyeo vyao," amesema Aussems ambaye kwa sasa yupo nyumbani kwake nchini Ufaransa na kuongeza:
"Naogopa, nadhani tatizo hilo litachelewa kuisha hususan kama viongozi hawatataka kubaki kwenye vyeo vyao na kutimiza majukumu yao bila kuingilia ya wengine."
Kocha huyo aliyeipa Simba makombe mawili, Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho (FA), sambamba na kuifikisha timu hiyo robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika amesema watu pamoja na vyombo vya habari vinapaswa kupaza sauti ili kukomesha jambo hilo Afrika.
"Nimekuwa Afrika kwa muda na hilo ni tatizo sugu. Nadhani njia pekee ya kulikomesha ni watu kuzungumza na kulikalipia hususan nyie wana habari," amesema kocha huyo aliyeondoka Simba na kuchapisha andiko kwenye mtandao wake wa kijamii wa Instagram lililosomeka Simba ili ikue inapaswa kuepukana na viongozi wasio na maarifa na waongo.
Tangu kuondoka kwa Aussems mwaka 2019, Simba imefundishwa na makocha saba tofauti ambao ni Sven Vandebroeck, Didier Gomes, Pablo Franco, Zoran Maki, Juma Mgunda, Roberto Oliveira 'Robertinho' na Benchikha.
Wakati Benchikha akiondoka Simba timu hiyo itakuwa chini ya Juma Mgunda na Selemani Matola na kesho itacheza mechi ya ligi dhidi ya Namungo katika Uwanja wa Majaliwa, Lindi.