Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Aussems, Miraji watwaa tuzo VPL

78460 Pic+miraj

Fri, 4 Oct 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

MSHAMBULIAJI wa timu ya Simba, Miraji Athumani amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Ligi Kuu ya Vodacom  (VPL) mwezi uliopita Septemba huku kocha wake Patrick Aussems akiwa Kocha Bora wa mwezi huo.

Miraji na Aussems wametwaa tuzo hiyo baada ya kuwashinda wenzao walioingia nao fainali katika uchaguzi uliofanywa na Kamati ya Tuzo ya VPL inayotolewa na Shirikisho la Soka nchini (TFF) kutokana na mapendekezo ya makocha wanaokuwa viwanja mbalimbali, ambavyo ligi hiyo inachezwa msimu huu.

Kwa mwezi huo wa Septemba, Simba ilicheza michezo mitatu na kushinda yote ikiifunga Mtibwa Sugar mabao 2-1, Kagera Sugar mabao 3-0 na Biashara United mabao 2-0, ambapo Miraji alikuwa na kiwango kizuri uwanjani kwa mwezi huo akichangia kwa asilimia kubwa mafanikio ya Simba ikiwa ni pamoja na kufunga mabao mawili na kutoa pasi za mabao mawili.

Miraji aliwashinda Meddie Kagere wa Simba aliyetoa mchango mkubwa pia katika mafanikio ya Simba ikiwa ni pamoja na kufunga mabao manne.

Mchezaji mwingine aliyeingia fainali alikuwa Ismail Kada wa Prisons aliyeonesha kiwango kizuri na kutoa mchango katika michezo ambayo Prisons  ilicheza ikishinda miwili, sare mmoja, ambapo iliifunga Ruvu Shooting mabao 2-1, Mtibwa Sugar mabao 3-1 na kutoka sare na Lipuli mabao 2-2.

Kwa kutwaa tuzo hiyo, Miraji atazawadiwa kikombe na Sh. 1,000,000 milioni kutoka kwa wadhamini wa ligi hiyo pamoja na Kisimbusi  kutoka Azam TV ambao ni wadhamini wenza.

Upande wa Aussems aliwashinda Mohammed Rishard wa Prisons na Abdallah Mohammed 'Bares' wa JKT Tanzania, ambapo Aussems aliongoza timu yake kupata ushindi michezo mitatu, kati ya hiyo mmoja nyumbani dhidi ya Mtibwa Sugar na miwili ugenini mabao 3-0 dhidi ya Kagera Sugar na mabao 2-0 dhidi ya Biashara United, huku Simba ikimaliza mwezi ikiwa nafasi ya kwanza.

Rishard aliingia hatua ya fainali baada ya kuiongoza Prisons kushinda michezo miwili na kutoa sare mmoja, ilishinda nyumbani mabao 2-1 dhidi ya Ruvu Shooting,  alishinda ugenini mabao 3-1 dhidi ya Mtibwa na kutoka sare ugenini na Lipuli ya mabao 2-2, wakati Bares aliingoza JKT Tanzania kushinda michezo miwili, sare moja na kupoteza mmoja.

 JKT Tanzania ilifungwa ugenini bao 1-0 na Lipuli,  ikatoka sare tasa nyumbani na Mtibwa Sugar,  ikashinda bao 1-0 ugenini dhidi ya Biashara United na pia ikapata ushindi ugenini kama huo dhidi ya Kagera Sugar.

Chanzo: mwananchi.co.tz