Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Augsburg kipimo kizuri kwa Yanga

Yanga Mpumalangaa.jpeg Augsburg kipimo kizuri kwa Yanga

Sun, 21 Jul 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Achana na matokeo ya kupoteza mchezo mbele ya FC Augsburg, lakini kilichoonyeshwa na Yanga katika pambano la kirafiki la kimataifa la kuwania ubingwa wa michuano ya Kombe la Mpumalanga kinatoa picha soka la Tanzania linazidi kusonga mbele.

Yanga ilipoteza kwa mabao 2-1 mbele ya timu hiyo ya Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) kwenye Uwanja wa Mbombela, mjini Mpumalanga, Afrika Kusini, huku Kocha Migueal Gamondi akiwatumia nyota wapya waliosajili katika dirisha lililo wazi kwa sasa.

Huo ulikuwa mchezo wa kwanza kwa Yanga tangu ianze kambi ya maandalizi ya msimu mpya wa 2024-2025 iliyoanzia Avic Town, Kigamboni kabla ya kusafiri kwenda Afrika Kusini na itakuwa huko kwa siku zisizopungua 16 kabla ya kurejea nchini kufanya tamasha la Wiki ya Mwanachi kisha kucheza Ngao ya Jamii.

Katika mchezo huo uliopigwa saa 9 alasiri kwa saa za Sauzi (sawa na saa 10 jioni), Yanga ilionyesha soka tamu na la ushindani na kama sio kukosa umakini kwa baadhi ya nyota wa timu hiyo ni wazi ingewashangaza Augsburg ambao ilichezesha vikosi viwili tofauti kwa kila kipindi na kila kimoja kufunga bao.

REKODI IMEANDIKWA

Japo kuna baadhi ya mashabiki wanaibeza Yanga kwa kupoteza mchezo huo, lakini klabu hiyo imeandika rekodi ya kuwa timu ya kwanza ya Tanzania kucheza na klabu ya Bundesliga, ambayo msimu uliiopita wa Ligi Kuu ya Ujerumani ilimaliza nafasi ya 11 katika msimamo wa ligi hiyo.

Inawezekana ni kweli Augsburg haikuchezesha fulu mkoko wa kikosi cha kwanza kilichozoeleka, lakini asilimia kubwa ya wachezaji walioanzishwa kipindi cha kwanza na hata walioingia kipindi cha pili hutumika katika kwa mechi nyingi za timu hiyo ukiondoa wachache.

Lakini hata aina ya soka ililoonyesha timu hiyo ya Ujerumani, inaweza kuwa ni faida kubwa kwa Yanga kwani imepata kitu cha kuanzia kwenye michuano iliyopo mbele yao ikiwamo ile ya Ngao ya Jamii, Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho Afrika na Ligi ya Mabingwa Afrika ikipangwa kuanza na Vital'O ya Burundi.

Kwa jinsi wachezaji wa Yanga walivyocheza kwa kujiamini mbele ya Augsburg ilifanya hata mashabiki waliokuwa wakiufuatilia mchezo huo katika nchi mbalimbali hususan Afrika Kusini na nyumbani Tanzania kuwamwagia sifa mabingwa hao wa Tanzania kwa soka ilililopiga na kuisumbua timu hiyo ya Ujerumani.

DIARRA NA MAXI

Kama kuna wachezaji ambao Augsburg wataondoka na majina ya nyota wa kikosi cha Yanga, basi Maxi Nzengeli, kipa Diarra Djigui, Chadrack Boka, Duke Abuya ambao wakionyesha soka tamu na kujiamini kupita kiasi, huku wakisumbua na kuwapa wakati mgumu wapinzani wao hao.

Diarra pamoja na kufungwa mabao mawili moja kila kipindi, aliokoa michomo mingine kadhaa na kuifanya Yanga kuepuka kupata aibu ugenini kwa kufungwa idadi kubwa ya mabao kama ilivyokuwa ikitabiriwa na baadhi ya mashabiki mapema kabla ya mchezo huo.

Kwa upande wa Maxi alionyesha yeye ni mchezaji wa aina gani kwa alivyocheza bila kuchoka kwa dakika zote 90, akifanya mashambulizi makali na kuitoka mara kadhaa ngome ya Augsburg na kufanya majaribio kadhaa langoni mwa timu hiyo ya Ujerumani.

Alikuwa na uwezo wa kukaa na mpira, kumilikia na kupiga chenga mbali na kutoa pasi na kupiga mashuti makali, ikiwamo lile lililogonga mtambaa panya katika kipindi cha kwanza.

Abuya aliyeingia kipindi cha pili kama ilivyokuwa kwa Aziz Andambwile, Prince Dube, Jean Baleke, Shekhan Ibrahim, Chadrack Boka na Bakar Mwamnyeto ili kuchukua nafasi za Nickson Kibabage, Ibrahim Bacca, Salum Abubakar 'Sure Boy', Mudathir Yahya, Aziz Ki, Clatous Chama na Clement Mzize, aliupiga mwingi.

Mkenya huyo aliisumbua ngome ya Augsburg na kuonyesha Yanga haikukosea kumsajili kutoka Singida BS kwa alikuwa akitiririka na mpira na kugawa 'vyumba' na kushirikiana vyema na wenzake muda wote uwanjani.

CHAMA FRESHI

Licha ya kutokuwa na maajabu, lakini Chama ameonekana kwake mambo freshi kwa kuanzishwa katika kikosi cha kwanza na kucheza kwa dakika 64 kabla ya kutoka kumpisha Baleke, huku akicheza kwa utulivu na kutoa pasi zenye macho, ingawa bado tatizo lake lipo pale anapokuwa hana mpira.

Katika mechi ya juzi aligusa mpira mara nyingi ndani ya eneo la Augsburg akiwa nyuma ya Maxi, Mzize na Aziz KI na pasi yake kwa Maxi kama ingetumiwa vyema katika kipindi cha kwanza ingeitanguliza Yanga, kwani shuti kali la Mkongoman huyo liliishia kugonga besela na kurudi na kushindwa kumaliziwa na Aziz KI.

Ni ngumu kumjaji Chama kwa dakika alizocheza sambamba na hata wachezaji wengine wapya wa Yanga kwa vile huo ulikuwa ni mchezo wa kwanza kwao, lakini wakiwa ndio wametoka kukusanyana kuanza kambi ya maandalizi ya msimu na wamekutana na timu ya daraja la juu kutoka bara Ulaya.

Nyota huyo na wenzake wanaweza kuja kupigwa Jumatano wakati watakaporudi tena kwenye michuano hiyo ya Mpumalanga kuvaana na wenyeji wao, TS Galaxy ya Afrika Kusini kisha kumalizana na Kaizer Chiefs katika mchezo wa michuano ya Kombe la Toyota utakaopigwa Julai 28 kabla ya timu kurejea nchini.

BALEKE, DUBE WAMO

Washambuliaji Jean Baleke na Prince Dube walioingia kipindi cha pili wameonyesha uhai na kutoa ishara wakizoeana na wenzao waliowakuta watatengeneza kombinesheni matata itakayoweza kusumbua katika Ligi Kuu Bara, kwani katika mechi ya juzi walicheza kwa ushirikiano na utulivu wa hali ya juu.

Bao alilofunga Baleke kwa kichwa dakika ya 86 ilikuwa ni mfano halisi wa utulivu aliokuwa nao mshambuliaji huyo wa zamani wa Simba aliyekuwa akikipiga Al Ittihad ya Libya kwani alijiweka katika nafasi nzuri kuisindikiza wavuni pasi tamu ya Maxi iliyotokea pembeni.

Pia kuna wakati waligongeana na Dube na Abuya na kulitia msukosuko lango la Augsburg, japo Yanga ilipoteza bao dakika za lala salama.

PENGO LA AUCHO, PACOME

Katika mechi hiyo ya juzi, Pacome Zouzoua na Khalid Aucho hawakuwa kabisa sehemu ya kikosi hicho na mapengo yao yalionekana hasa kipindi cha kwanza kwa Yanga kukosa utulivu na kukaa na mpira muda mrefu.

Pacome hajaambatana na timu kabisa Afrika Kusini, huku Aucho akiwa amechelewa kuungana na wenzake kambini, hivyo kulazimisha Sure Boy na Mudathir kucheza katika nafasi zao kabla ya kutolewa kipindi cha pili kuwapisha kina Abuya na Andambwile ambao waliziba mashimo na kuirejeshea Yanga uhai.

Ni wazi kama nyota hao wawili wakiungana na wenzao na kucheza walivyocheza na Augsburg timu pinzani zitapata tabu sana, kwani mziki wa Maxi, Aziz KI, Chama sambamba na Baleke na Dube huenda ukawasumbua, japo soka wakati mwingine huwa na maajabu yake.

Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi alisema mechi hiyo kwake ni kipimo na mwanzo mzuri wa maandalizi ya msimu ujao na amefurahia wachezaji walivyocheza hata walipoteza mchezo kwani walicheza na timu bora na iliyowa ushindani mzuri wa kujiweka fiti zaidi kwa mashindano yaliyopo mbele yao.

Yanga ikimaliza kambi hiyo ya Sauzi, itarejea nchini kabla ya Agosti Mosi, ili kujiandaa na Tamasha la Wiki ya Mwananchi litakalofanyika Agosti 4, kisha siku nne baadae kucheza na Simba katika Dabi ya Kariakoo ya Ngao ya Jamii siku ya Nane Nane na kujiandaa na mechi za Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa Afrika.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: