Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Aucho wa Ligi Kuu ni tofauti na wa Afrika

Khalid Auchoooooooo Aucho wa Ligi Kuu ni tofauti na wa Afrika

Mon, 26 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kila baada ya mechi za raundi moja, ambazo kwa kawaida huchezwa Ijumaa hadi Jumapili, hufuata uchambuzi wa jinsi zilivyochezwa, nafasi ya kila timu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara na nafasi ya ubingwa au kushuka daraja.

Lakini uchambuzi mkubwa zaidi hujikita katika makosa ya uamuzi na hasa katika mechi zinazohusu timu mbili za Simba na Yanga, ambazo hakuna siri kwamba ndizo zinazoangaliwa na wengi, na kwa mtindo wa siku hizi, ndizo zinazokufanya uonekane sana (views) katika mitandao.

Si jambo la ajabu kusikia, “Ile ilikuwa penalti ya wazi kabisa” au timu fulani “imenyimwa bao halali” au “bao halikustahili kusimama kwa kuwa mfungaji alikuwa ameshaotea” au mchezo mbaya.

Bahati mbaya sana uchambuzi huo wa “mchezaji kustahili kadi nyekundu”, humuhusu sana kiungo wa nyuma wa Yanga, Khalid Aucho.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Uganda husakamwa sana kila anapomaliza mechi kiasi cha kuonekana anabebwa na waamuzi kwa kutoonyeshwa kadi za njano za kutosha kumepeleka nje eti kwa kuwa anacheza rafu sana.

Ilifikia wakati hadi ile Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji Ligi ikafikia uamuzi wa “kumuonyesha kadi nyekundu” kutokea mezani kutokana na kutoridhika na maoni ya mwamuzi ambaye aliona tukio lake na Ibrahim Ajibu lilistahili kadi ya njano.

“Ile kamati” ikatafuta kipengele kimoja kwenye kanuni ambacho kinahusu mchezaji kumpiga kiongozi, mchezaji mwenzake au shabiki kumtia hatiani Aucho na kumfungia kucheza mechi tatu ambazo ameshamaliza.

Hivi sasa inasubiriwa kadi nyingine nyekundu ya “kutokea mezani” baada ya wachambuzi kuona kiungo huyo alimvuta jezi mchezaji wa timu pinzani, lakini hakuonyeshwa kadi ya pili ya njano.

Ni kweli kiungo huyo mwenye umbile la miraba minne huonekana anacheza rafu wakati akigombea mpira na wachezaji wa timu pinzani, lakini mara nyingi adhabu zake huishia kwenye kadi moja ya njano na ni nadra sana kukumbana na kadi nyekundu ya moja kwa moja.

‘Dhambi zake pale kwenye dimba la chini ndizo huiwezesha ngome ya Yanga kuwa na kazi ndogo ya kuokoa mipira kwa sababu ama huwezesha timu yake kupokonya mipira kirahisi, ama ngome kupata mipira iliyokwishapoa, ama wakati mwingine ngome kuwa mapumzikoni kwa muda mrefu. Na pengine ndio sababu ni nadra sana kwa mabeki wa Yanga kujikuta wakienda chini kupiga ngwala kama afanyavyo Ibrahim Bacca kwa nadra.

Na sifa hizo ndizo zimewafanya makocha wawili waliopita Yanga au waliopo kumtegemea sana Aucho katika ukabaji, achilia mbali kuichezesha timu na kuifanya kuwa kitu kimoja na hivyo kuwa imara.

Ni Aucho huyohuyo aliyeaminiwa na Nasredine Nabi katika mechi za Ligi Kuu na kimataifa, akiwa mmoja wa wachezaji walioifikisha Yanga fainali ya Kombe la Shirikisho msimu uliopita.

Na Gamondi ameshikilia msimamo uleule. Ni Khalid Aucho anayeshikilia nafasi ya kiungo mkabaji wa Yanga katika mechi za Ligi Kuu na zile za Ligi ya Mabingwa na Jumamosi aliiongoza Yanga kutawala katima kiungo wakati ilipoishinda CR Belouizdad kwa mabao 4-0, ikiwa ni timu ya kwanza ya Tanzania kuibuka na ushindi mkubwa wa zaidi ya mabao 2-0 dhidi ya timu kutoka Afrika Kaskazini, hasa Morocco, Algeria, Tunisia na Algeria.

Baada ya mechi hizo za kimataifa, husikii ule uchambuzi wa rafu za Aucho na tuhuma za kubebwa na waamuzi. Na amekuwa na rekodi nzuri ya nidhamu kwenye mechi za kimataifa kuliko za Ligi Kuu, ambako waamuzi wakiona hakustahili kadi, wajumbe wanaenda ‘mezani kumuonyesha ya kwao’.

Unashangaa Khalid Aucho anayecheza Ligi Kuu ni yuleyule anayecheza mechi za kimataifa? Au huwa anabadilika kiuchezaji na kuwa na nidhamu kubwa kuliko anapocheza mechi za ndani? Hilo kweli linawezekana kwa mchezaji mwenye tabia ya kucheza rafu? Pengine linawezekana kwa mchezaji kujizuia mechi moja lakini si zote.

Ukifuatilia utaona pengine ni udhaifu wetu wa kujichukulia mamlaka ya kuwatia hatiani wachezaji na kupingana na yule anayepewa majukumu ya mwisho na sheria za mpira wa miguu kuwa maoni yake yatawale.

Uamuzi wa mechi za soka bado unategemea maoni ya refa pale uwanjani na kwa wenzetu wana teknolojia ya Mwamuzi Msaidizi wa Video (V.A.R) ambayo pia hairudii matukio yote isipokuwa yale muhimu yanayotokea golini au wakati wa kuanzisha shambulizi linalozaa bao au tukio linalostahili kadi nyekundu ya moja kwa moja.

Hata wao kwa sasa wako matatizoni na hiyo teknolojia huku Kampuni ya Waamuzi wa Mechi za Soka la Kulipwa (PGMOL) ya England ikilazimika kutoa ufafanuzi kila wakati kuhusu uamuzi wa marefa na wakati mwingine kukiri makosa na kuomba radhi. Ufaransa ndiko bomu limelipuka baada ya mwamuzi mmoja kukiambia chombo kimoja cha habari kuwa huwa wanaambiwa wachakachue matukio baada ya kuangalia kwenye video kwa lengo la kuibeba timu, jambo ambalo linaweza kusababisha bosi wa waamuzi ama kujiuzulu au kutimuliwa.

Lakini kwa utamaduni wa mpira ni lazima maoni ya refa ndiyo yatawale, huku tunajaribu kurekebisha maoni yao. Tumeona wiki iliyopita ‘ile kamati’ ilifuta kadi ya pili ya njano, ikitoa maoni yake kuwa mchezaji aliunawa mpira baada ya kusukumwa na kufuta maoni ya refa ambaye aliona mchezaji alijirusha ili apate penalti.

Ili kuulinda mpira, ni lazima tuendelee kuheshimu maoni ya waamuzi na ni muhimu kuwakosoa kwa staha na si kuwabebesha tuhuma nyingine juu kwamba wanabeba timu au wachezaji. Kile tunachoangalia katika picha za marudio za Azam TV hakitoshi kuhitimisha kuwa mwamuzi amekosea au alikuwa sahihi kwa sababu kampuni hiyo ya habari pia haina vifaa vya kutosha kutuonyesha tukio kwa ukamilifu.

Zaidi ya yote, waamuzi hutumia miongozo yao kutafsiri matukio kabla ya kuamua na si tu kukariri sharia kwamba “alikuwa ametanua mikono wakati sharia inasema mikono ikiwa katika sehemu yake ya kawaida haiwi faulo”. Unahitaji kujua mengi zaidi kabla ya kuhitimisha maoni yako kwa kukariri mstari mmoja tu wa sharia.

Ndio maana maoni ya waamuzi wa Ligi Kuu ya Tanzania hayatofautiani na ya wale wa mechi za Kombe la Shirikisho au Ligi ya Mabingwa ambako Khalid Aucho hakumbani na zile kadi za pili za njano ambazo wengi wanatamani kuziona kwa Mganda huyo.

Hiyo haimaanishi kuwa Aucho haonyeshwi kadi nyekundu au hajawahi kuonyeshwa kadi nyekundu, la hasha. Ila zile ambazo wengi wanazitamani, hakumbani nazo mechi za ndani na zile za kimataifa. Kwa kifupi, Khalid Aucho anayecheza Ligi Kuu ndiye huyohuyo sasa anacheza Ligi ya Mabingwa na staili yake ni ileile, iweje tutamani apewe kadi nyekundu katika mechi za ndani tu?

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: