Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Aucho ni zaidi ya mchezaji Yanga, Nabi amshangaa

Aucho Pic Kiungo wa Yanga, Khalid Aucho

Mon, 1 Nov 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wanajangwani, Yanga SC juzi usiku ilikuwa uwanjani ikipambana na Azam FC katika mchezo wa nne wa Ligi Kuu Bara na kikosi chao kuna mastaa wapya saba waliokiongeza ubora, lakini kiungo wao mmoja, Khalid Aucho amemsapraizi kocha Nasreddine Nabi na mastaa wenzake mazoezini kuonyesha asivyo na masihara.

Kiungo kutoka Uganda, alifanya kitu ambacho sio rahisi kwa wachezaji na hata manahodha ni wachache wanaomudu katika ratiba ya mazoezi baada ya kuwataka wenzake wasibweteke.

Aucho aliwashtukia wenzake kuwa hawajitumi mazoezini kama watu walioridhika na mafanikio ya muda mfupi na kuwaambia hapana, akasimamisha ratiba hiyo akiwataka kila mmoja wao kujituma.

Aliyefichua hilo ni Kocha Nabi, aliyesema kiungo huyo alimshtua akitaka kila mmoja kupambana mazoezini.

Nabi alisema Aucho aliwataka wenzake kuacha kubweteka na kushinda mechi tatu (kabla ya jana) na ligi bado ngumu vinginevyo watapoteza malengo.

“Nilishtuka alipowatamkia vile wenzake tukiwa mazoezini. Ni mmoja kati ya wachezaji waliokomaa kiakili tulionao ambao wanatambua umuhimu wa kushindana kuanzia mazoezini,” alifafanua Nabi na kuongeza.

“Alieleweka kwa wenzake, kwani kila mmoja alibadilika na kuongeza juhudi unahitaji kuwa na watu bora kama hao kwenye timu na hii ni kielelezo kingine kwamba tuna timu imara.”

Nabi amesema anafurahia ukomavu wa Aucho katika kikosi chao ambapo endapo kila mchezaji wake atajitambua kwa kiwango hicho msimu huu wanaweza kufikia malengo.

“Sina mashaka na akili ya wachezaji wangu, ila unahitaji kuwa na watu wanaotambua kwanini wako hapa Yanga na uzito wa kujituma kwa ajili ya klabu kubwa kama hii. Tuna deni kubwa hapa msimu huu kuhakikisha mashabiki wote wanafurahia haya ambayo wanatamani kuona yanatimia,” amesema Nabi aliyeipa Yanga Ngao ya Jamii kwa kuifumua Simba bao 1-0 la Fiston Mayele.

MSIKIE CHUJI

Kiungo wa zamani wa Yanga na Simba, Athuman Idd ‘Chuji’ amesema alichofanya Aucho ni dalili kwamba ni mchezaji anayejitambua.

“Sishangai kitu kama hicho kufanywa na mchezaji kama Aucho hapa, maana rahisi inayokuja ni kwamba ni mchezaji anayejitambua,” amesema Chuji.

“Alichokuwa anakataa hapo ni wachezaji kuanza kujisahau na hiyo ipo sana hata mimi wakati nacheza hali kama hiyo ilikuwa inatokea na nilikuwa nawaambia wenzangu kama unaona hujisikii kufanya mazoezi ni bora ukamuomba kocha upumzike.”

Yanga inakwenda kucheza mchezo wake wa tano dhidi ya Ruvu Shooting siku ya Jumanne majira ya saa 12:15 jioni, na tayari wametoa tahadhari kwa kikosi hicho kinachonolewa na Mchezaji na Kocha wake wa zamani Charles Boniface Mkwasa.

Katika msimamo wa Ligi Kuu mpaka sasa Yanga ndio kinara akiwa kileleni na alama 12 baada ya kushuka dimbani michezo minne.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live