Kiungo wa Yanga, Khalid Aucho raia wa Uganda, ameeleza kwamba, baada ya kumaliza majukumu ya timu ya taifa, sasa yupo tayari kuitumikia klabu yake.
Aucho alikuwa na kikosi cha Uganda katika mchezo wa mwisho wa kufuzu AFCON dhidi ya Niger ambao walishinda 2-0.
Baada ya kumalizika kwa majukumu ya timu za taifa, sasa ni wakati wa wachezaji kurejea katika klabu zao huku Yanga tukiwa na mchezo muhimu mbele dhidi ya Al Merreikh kuwania kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Akizungumzia utayari wake, Aucho amesema: “Majukumu ya timu ya Taifa yameshamalizika na sasa akili na nguvu nazihamishia kwenye klabu yangu.
“Tuna mchezo muhimu sana unakuja, kama wachezaji tunatakiwa tuwe tayari kwenda kupambana kuhakikisha tunaipeleka timu yetu hatua ya makundi.
“Nimerudi salama na niko tayari kuungana na wenzangu kufanya vizuri kwenye mchezo dhidi ya Al Merreikh.”
Mchezo wa kwanza unatarajiwa kuchezwa Septemba 16, 2023 nchini Rwanda, kisha marudiano Uwanja wa Azam Complex, Dar.