KIUNGO matata wa Yanga Sc raia wa Uganda, Khaalid Aucho amerejea mazoezini tayari kwa kuiwinda mechi yao dhidi ya Simba inayotarajiwa kupigwa Aprili 30, mwaka huu.
Aucho alikuwa nje ya kikosi cha Yanga baada ya kusumbuliwa na tatizo la nyama za paja ambazo zimemweka nje ya uwanja kwa takriban mwezi mmoja sasa.
Chanzo chetu kutoka Yanga, kimeliambia Championi Jumatano kuwa, tayari Aucho ameshapona majeraha yake na ataungana na wenzake kwa ajili ya mazoezi ya kujiandaa na mechi ya Aprili 30, mwaka huu dhidi ya Simba.
“Tumecheza takribani mechi tatu bila Aucho jambo ambalo kwa namna fulani lilikuwa gumu sana kwenye safu yetu ya kiungo, ila faraja kwa sasa ni kwamba tayari aucho amerejea na mechi yetu ijayo atakuwa ndani ya kikosi baada ya mwenyewe kuthibitisha kupona,” kilisema chanzo hicho.