Kiungo cha Yanga kinahesabu saa kabla ya kushuka kwa Mkapa kuvaana na Tanzania Prisons katika mechi ya Ligi Kuu, lakini kiungo fundi ameiweka kwenye wakati mgumu baada ya kuomba kusepa zake, huku nyota wengine watatu wakiwa kwenye hatihati baada ya kumaliza mikataba.
Achana na Feisal Salum ‘Fei Toto’ ambaye anawaumiza vichwa mabosi wake kwa kutaka kuboreshewa mkataba wake ili aendelee kusalia kikosini baada ya kuletwa mezani ofa kibao ikiwamo ya Azam FC, lakini kiungo Khalid Aucho ‘Dokta’ ameomba asiongezwe mkataba ili atimkie Arabuni.
Aucho mkataba wake upo ukingoni kama ilivyo kwa beki wa kati, Dickson Job na kipa Djigui Diarra na taarifa za ndani zinasema kuwa vigogo wameanza kufanya mazungumzo nao ili kuwaongezea mkataba kabla ile ya awali haijaisha, lakini kiungo huyo Mganda ameweka bayana anataka kuondoka Jangwani.
Kwa mujibu wa mikataba waliyoingia mastaa hao mwanzoni mwa msimu uliopita na kuisaidia timu hiyo kutwaa ubingwa sasa wanamalizia msimu huu ili kukamilisha mikataba yao.
Job na Diarra mchakato wa kuongeza mikataba mipya unaendelea, ila Aucho inaelezwa amegoma baada ya kupokea ofa mpya kutoka moja ya klabu kutoka Saudia. Juu ya ishu ya Fei Toto inaelezwa kuwa kiungo huo ambaye anatajwa kuwa na ofa nyingi ndani na nje na ana mkataba na Yanga unaoelezwa utamalizika 2024, lakini anahitaji kuboreshewa mshahara wake kama ilivyofanywa kwa Fiston Mayele, Yanick Bangala na Djuma Shabani.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya klabu hiyo kimelithibitishia Mwanaspoti, uongozi umeshaanza mchakato wa kuzungumza na mastaa hao huku jukumu likiwa chini ya mwekezaji mkuu wa timu Gharib Said Mohammed (GSM).
Mwanaspoti lilimtafuta meneja wa Job, George Job, aliyefunguka kwa kusema ni kweli mchezaji wake mkataba wake unaelekea ukingoni na hawana presha na hilo kutokana na uwezo anaouonyesha.
“Kwa sasa mchezaji anapambania timu iweze kutetea taji juhudi zote kawekeza huko, suala la mkataba linazungumzika hii ni kutokana na uwezo wake anaouonyesha,” alisema Job na kuongeza;
“Mazungumzo kwa ajili ya mkataba mpya yameanza lakini sio kwa presha kwani mchezaji anaonyesha kile klabu inachotaka pia nakiri kuwa kwa kiwango alichonacho hakuna timu ambayo haitamani kuwa na beki kama yeye, lakini kubwa ni kwamba mchezaji anazingatia michezo iliyo mbele yake kuhakikisha anafanya vizuri.” Wakati huohuo, kocha wa Yanga Nasreddine Nabi amefungiwa mechi tatu na kutozwa faini ya Sh500,000 na Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu (TPLB).
Kocha huyo amefungiwa mechi hizo na kutozwa faini kwa kuwashambulia kwa maneno mwamuzi wa kati Ally Mnyupe na yule wa mezani Joachim Akamba katika mchezo wa ligi dhidi ya Ihefu ambao Yanga ililala kwa mabao 2-1.
Nabi aliendelea kufanya kitendo hicho hata baada ya kuonyeshwa kadi ya njano.
Kocha huyo atakosekana dhidi ya Tanzania Prisons (kesho), Namungo Desemba 7 (Jumatano) na kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) dhidi ya Kurugenzi.
Mbali na Nabi, Simba imetozwa faini ya Sh1 milioni na beki wake Gadiel Michael kufungiwa mechi tatu kwa vitendo vinavyohisiwa ni vya kishirikina mchezo dhidi ya Mbeya City ulioisha kwa sare ya 1-1.