Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Aucho anapopewa kadi nyekundu mezani

Aucho9175 Aucho anapopewa kadi nyekundu mezani

Mon, 20 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Katika moja ya akaunti za mitandao ya kijamii ya Bodi ya Kimataifa ya Mpira wa Miguu (IFAB) kuna maswali yanayohusu matukio yenye utata katika mechi na majibu ya jinsi ya kushughulikia matukio hayo, kuanzia kusimamisha mpira, kutoa adhabu na kuanzisha tena mpira.

Kwa kuwa bodi hiyo ndiyo chombo kinachotengeneza tafsiri za sharia za mpira wa miguu, huwa nafuatilia sana maswali hayo na majibu yake ili niweze kulinganisha na hiki tunachokiona kwa waamuzi wetu katika mechi za soka na mijadala ambayo huibuka baada ya matukio hayo.

Si mijadala tu, bali hata maamuzi zaidi ya vyombo vya mamlaka ya soka, na hasa ile kamati maarufu ya saa 72 ambayo pamoja na ile Kamati ya Maadili ndio vyombo pekee vinavyoonekana kuvikwa madaraka yote; yawe ya kuadhibu waamuzi, wachezaji na viongozi hadi—ilipofikia sasa— ya kupuuza kadi iliyotolewa na mwamuzi na kuweka adhabu mpya, kama ilivyofanyika kwa Khalid Aucho.

Nimechukua suala la Aucho pekee kati ya mengi yaliyoamuliwa na kamati hiyo wiki hii kwa kuwa ninaona dhahiri kuwa linakwenda kinyume na utamaduni wa mpira wa miguu, hasa ule unaoheshimika sana wa kumwachia refa maamuzi ya mwisho kwa matukio ya uwanjani.

Niliandika wiki iliyopita kitakachofuata ni adhabu, lakini nilichokuwa najenga hoja ni kuwepo na mkakati wa kushughulikia udhaifu wa waamuzi ambao unazidi kujionyesha karibu kila wiki.

Kama nilivyotarajia ndivyo ilivyotokea, lakini kamati imekwenda mbali zaidi kufanya uamuzi wa kuridhisha wachambuzi badala ya kuendelea kuheshimu utamaduni wa mpira wa miguu.

Kiungo huyo Mganda wa Yanga alikuwa ameinama kuchukua mpira kwa ajili ya kurusha. Lakini wakati anakaribia kuugusa, kiungo wa Coastal Union akaudokoa na kusababisha Aucho aokote hewa, kitu kilichomuudhi hadi kuamua kunyoosha mkono wake hadi usoni mwa Ajibu, ambaye mara moja alijidondosha chini kuashiria kuwa alipigwa kiwiko.

Refa hakuwa ameona tukio na hali akishangaa, akaitwa na refa wa akiba na baada ya mazungumzp alirejea na baada ya muda akawaonyesha wote wawili kadi ya njano.

Ile kamati ya masaa ikaona haitoshi, ikisema Aucho alimpiga kiwiko Ajibu na hivyo alistahili kadi nyekundu. Imemfungia Aucho Mechi tatu.

Kwa kanuni zetu, mchezaji anayeonyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja, huongezewa adhabu. Kadi nyekundu humanisha mchezaji anakosa mechi moja na ile ya moja kwa moja ni mechi mbili na hivyo kamati inaweza kumuonmgezea mechi moja. Na mchezaji anapoonyeshwa kadi nyekundu kwa kupigana, pia huongezewa adhabu na kamati.

Lakini tukio la juzi linamaanisha kuwa kamati imefuta kadi ya njano iliyotolewa na refa na hali ikiwa mezani, ikamuonyesha Aucho kadi nyekundu ya moja kwa moja na hivyo kutakiwa kukosa mechi mbili na kwa kuwa ina uwezo wa kuongeza adhabu, ikamuongezea na mechi moja zaidi. Ndiyo tafsiri ya uamuzi wa ile kamati ya masaa.

Kwamba sasa inaweza kumuonyesha mchezaji kadi nyekundu kwa kuangalia marudio ya video iliyotokana na kamera mbili pekee na kutoa adhabu iliyotakiwa itolewe na refa na kumuongezea adhabu inayotakiwa itolewe na kamati. Ni wapi mpira wetu unakwenda.

Katika ukurasa wa IFAB kuna swali linalohusiana na tukio kama hilo. Swali linasema “beki anamchezea vibaya mshambuliaji wa timu pinzani ambaye baadaye anadondoka chini. Beki anamwambia mshambuliaji anyanyuke ili waweze kuanzisha mchezo haraka kwa mpira wa adhabu. Baada ya hapo, mchezaji wa timu ya mshambuliaji anakuja kwa ajili ya kumkinga mchezaji mwenzake. Mchezaji huyo anasukumwa kwa makusudi na Yule beki. Uamuzi sahihi ni upi?”

Jibu linalotolewa na IFAB wenyewe linasema: “Kwa kutegemea nguvu iliyotumika kusukuma, beki (1) ataonywa kwa kadi ya njano kwa kuonyesha tabia isiyo ya kimichezo au (2) ataonyeshwa kadi nyekundu kwa kosa la kushambulia mwilini (kama nguvu iliyotumika ni kubwa au ya ziada.”

IFAB wanasema kwa kuwa tukio hilo lilitokea wakati mchezo umesimama, refa ataanzisha mchezo kwa ile ya adhabu ya awali ya beki kumuangusha mshambuliaji.

Hao ndio watunzi wa tafsi za sharia 17 za soka wanavyotuambia. Sasa ile kamati ya masaa sijui ilichukua tafsiri ya wapi hadi kufikia uamuzi wa kufuta kadi ya njano na kumuonyesha mchezaji kadi nyekundu ‘kutokea mezani’ na si uwanjani.

Ukijaribu kuingia akilini mwa mwamuzi aliyetoa kadi ya njano badala ya nyekundu kama wengi walivyotarajia, unaona kabisa kuwa asingeweza kutoa kadi nyekundu kwa tukio ambalo hakuwa hajaliona na hata maelezo ya mwamuzi wa akiba yasingetosheleza kufanya moja ya maamuzi makubwa kabisa katika soka.

Ndio maana hata Yule Mwamuzi Msaidizi wa Video (V.A.R) huwa hafanyi uamuzi, bali humuita mwamuzi wa kati kwenye runinga kwa ajili ya kuliangalia vizuri tukio na kufanya uamuzi.

Hakuna mwingine anayeweza kufanya uamuzi zaidi ya mwamuzi wa kati.

Hao wengine kazi yao ni kumpa taarifa za kutosha mwamuzi wa kati ili afanye uamuzi unaoweza kuwa sahihi.

Ndio maana Yule mwamuzi alipoelezwa na wenzake kuhusu tukio hilo, alirudi kuangalia ukubwa wa kitendo cha Aucho usoni mwa Ajibu na huenda aliridhika kuwa hakukuwa na matumizi makubwa ya nguvu kama tafsiri hiyo ya IFAB inavyoeleza.

Sasa yale maoni ya mwamuzi na uamuzi wake (discretion) yamefutwa na watu waliokaa mezani na si uwanjani na wao wakaweka maoni yao kuwa kulikuwa na matumizi ya nguvu za kupita kiasi na hivyo Aucho aadhibiwe “kwa kadi nyekundu ya moja kwa moja” na akose mechi mbili za kadi na moja ya nyongeza ya kamati.

Mpira hauwezi kuendeshwa namna hii. Navyojua kamati inaweza kufuta kadi tu baada ya kuangalia marudio ya video na kujiridhishali, lakini hii ya ‘kuonyesha’ kadi ni mpya na haikubaliki katika mpira tusijekufikia hatua hata mabao yaliyofungwa uwanjani, yakakataliwa na wajumbe waliokaa mezani na sio waliochezesha mechi.

Mpira wa miguu una utamaduni wake wa kuhesimu maamuzi ya refa na pale inapoonekana panahitajika msaada, basi ni kwa kutumia teknolojia kumpa taarifa zaidi ili anapofanya maamuzi awe ameelewa tukio kiasi cha kutosha.

Tusiruhusu kikundi cha watu kufikia hatua ya kuamua nani acheze na nani asicheze kwa kisingizio cha kamati ya masaa 72 na marudio ya matukio kwa kutumia video.

Hata marudio hayo ya matukio bado hayatoi taarifa za kutosha. Mara nyingi matukio mengi yanarekodiwa kwa kamera mbili pekee, ambazo haziwezi kuwapa wale wajumbe taarifa za kutosha kuhusu tukio.

Hata Yule Othman Kazi anayechambua matukio na kuelezea sharia inasemaje, hutumia matukio hayohayo yaliyorekodiwa na kamera mbili na matokeo yake ni kuwasulubisha waamuzi wenzake isivyo sahihi.

Kama bado hatujafikia maendeleo ya juu ya teknolojia, ni lazima tuendane na rasilimali zetu za sasa kufanya maamuzi badala ya kutumia nusu teknolojia kufanya maamuzi makubwa ya kimpira.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live