Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi ametamba kuwa timu yake inaweza kufanya vizuri katika mechi tatu zinazofuata za Ligi Kuu Tanzania Bara ambazo atamkosa kiungo wake Khalid Aucho lakini amefurahishwa na taarifa za kiungo huyo kuwa na uwezekano wa kuwahi mechi za hatua ya robo fainali ya ligi ya mabingwa Afrika zitakazochezwa mwishoni mwa mwezi huu na mwanzoni mwa mwezi ujao.
Kiungo huyo raia wa Uganda, juzi alifanyiwa upasuaji mdogo wa goti mwanzoni mwa wiki hii ambao utamfanya awe nje kwa muda wa wiki tatu, jambo litakalomfanya akose michezo mitatu inayofuata ya Yanga kwenye Ligi Kuu.
"Klabu imeshatoa taarifa kwamba Khalid Aucho amefanyiwa upasuaji mdogo ambao utamfanya akosekane kwa muda wa kama wiki tatu hivi na kama mambo yataenda kama yalivyopangwa, atarejea uwanjani baada ya muda huo," alisema meneja wa Yanga, Walter Samuel.
Ndani ya kipindi hicho, Yanga itakabiliwa na mechi tatu za ligi ambazo ni dhidi ya Ihefu, Machi 11, dhidi ya Geita Gold, Machi 14 na pia itakabiliana na Azam FC, Machi 17, ambazo zote zitachezwa katika Uwanja wa Azam Complex Chamazi.
Baada ya hapo, Yanga itakabiliwa na mechi mbili za hatua ya robo fainali ambazo ya kwanza itachezwa kati ya Machi 29, 30 na 31 na pia ya marudiano ambayo itachezwa kati ya Aprili 5 na 6, jambo ambalo kocha Gamondi anaamini haliwezi kuipa athari kubwa Yanga.
Kocha huyo alisema kuwa kwa michezo ambayo Aucho atakosekana, kikosi chake kinaweza kucheza vyema na kupata ushindi ingawa atafurahi zaidi kuwa na kiungo huyo kwenye hatua ya robo fainali.
"Akili yetu kwa sasa tunaielekeza katika mechi zinazofuata ambazo tunapaswa kupata ushindi ili tujiweke katika nafasi nzuri kwenye mbio za ubingwa. Yanga ina kikosi kipana chenye wachezaji ambao wanaweza kucheza vyema na kuipa timu matokeo mazuri kama ilivyotokea dhidi ya Namungo ambapo tuliwakosa wachezaji watano wa kikosi cha kwanza.
"Namuombea Aucho apone kwa haraka na kurejea kikosini na kama akiwahi mechi za robo fainali itakuwa jambo la muhimu sana kwa upande wetu kutokana na mchango wake kikosini. Wanayanga hawapaswi kuwa na hofu na kipindi hiki ninawaomba waendelee tu kutupa sapoti yao," alisema Gamondi.
Kwa upande wake Aucho alisema kuwa upasuaji huo umefanyika vizuri na anategemea kuonekana uwanjani muda sio mrefu.
"Napenda kusema asante kwa salamu za kunitakia kheri za kuniombea nipone mapema. Nategemea kurejea nikiwa imara na kuisaidia timu. Asante kwa upendo na ninauthamini sana," Aucho.
Katika hatua nyingine, nyota wa kikosi cha Yanga, wametamba kuwa watahakikisha wanalinda nafasi yao kileleni mwa msimamo wa ligi hadi pale watakapojihakikishia taji la Ligi Kuu msimu huu.
Nahodha wa Yanga, Bakari Mwamnyeto alisema kuwa kadri mechi za ligi zinavyozidi kupungua, ndivyo ushindani unavoongezeka hivyo watahakikisha wanajitoa kwa kadri ya uwezo wao ili waweze kumaliza vizuri.
"Tunaongoza ligi kwa pointi 10, sisi kila mechi ni fainali na tunazidi kusonga mbele. Msimu huu lengo la kwanza ni kuchukua taji na tutahakikisha tunalitimiza hilo," alisema Mwamnyeto.
Kiungo Mudathir Yahya alisema kuwa wanahitaji kutwaa ubingwa kwa ajili ya mashabiki wa timu hiyo hivyo watahakikisha hawawaangushi.