Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Aucho, Yao, Pacome waandaliwa kuwamaliza Simba

Pacomeeee Auchooo Pacome Zouzoua.

Thu, 11 Apr 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Yanga imeanza kupiga hesabu za mchezo wake dhidi ya Simba 'Dabi ya Kariakoo' ambapo jana iliamua kutowatumia nyota wake watatu waliokuwa majeruhi, Khalid Aucho, Pacome Zouzoua na Yao Attohoula dhidi ya Dodoma Jiji ikilenga kuwatumia katika mechi dhidi ya watani wao, Aprili 20 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Habari za uhakika ambazo tumezipata zikithibitishwa na ofisa habari wa Yanga Ally Kamwe ni kuwa watatu hao tayari wameshapona majeraha yaliyokuwa yakiwakabili na wameshaungana na wenzao katika program za mazoezi lakini hawatotumika kwa mechi za hivi karibuni ili kutowaweka katika hatari ya kuikosa Simba.

"Tuna mchezo muhimu dhidi ya Simba hapo Aprili 20 ambao tunahitaji kupata ushindi wa kishindo ambao utatuweka katika nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa na hili hilo litimie tunapaswa kuwa na hao watatu hivyo ndio maana kwa sasa tunawaandaa kimyakimya ili waje kuionyesha kazi Simba," alisema mmoja wa viongozi wa timu hiyo.

Akizungumza nasi, Kamwe alisema kuwa watatu hao wamesharejea kikosini na wanaendelea vizuri na maandalizi ya kuivaa Simba katika mchezo ambao wamepania kupata ushindi kwa sababu tatu kubwa.

"Tunafahamu kuwa Simba wanataka kutumia mechi dhidi yetu ili wapate faraja msimu huu kwa vile hawana uwezekano wa kuchukua kombe lolote hivyo watajiandaa sana jambo ambalo hatuko tayari kuona likitokea na ndio maana tunataka kuona siku tunayocheza dhidi yao, tuna kikosi kilichokamilika kikiwa na silaha zote muhimu wakiwemo hao watatu.

"Hiyo kwa Yanga ni zaidi ya mechi na tutahakikisha tunafanya maandalizi mara nne zaidi ya yale tuliyofanya kwa ajili ya mechi zetu mbili dhidi ya Mamelodi Sundowns katika Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kamwe alisema kuna mambo matatu yanayoisukuma Yanga kujiandaa vilivyo na mechi hiyo dhidi ya Simba.

"Kwanza ni mchezo ambao una nafasi kubwa ya kuamua ubingwa kwa upande wetu kama tukifanikiwa kuchukua pointi tatu lakini jambo la pili ni kutowapa nafasi ya wao kulipa kisasi cha sisi kuwafunga mzunguko wa kwanza na pia kumaliza msimu wakiwa wamepata ushindi dhidi yetu na sababu ya tatu ni kuwadhohofisha zaidi.

"Sherehe za ubingwa ili zinoge, ni lazima tuwe tumepata ushindi dhidi ya Simba. Tumeshafanya hivyo katika mzunguko wa kwanza kwa kuwafunga mabao matano na sasa tunataka tumalizie kwenye mzunguko wa pili," alisema Kamwe.

Aucho amekosekana kwa kipindi cha takribani mwezi mmoja akipatiwa matibabu ya goti wakati majeraha yaliyokuwa yakimkabili Pacome ni ya enka na Attohoula alipata tatizo la kuchanika nyama.

Pacome amekuwa tegemeo la Yanga katika kufunga na kutengeneza mabao ambapo hadi sasa amehusika na mabao 11, akifunga mabao saba na kupiga pasi nne za mwisho wakati Yao amekuwa lulu katika kupika mabao ambapo hadi sasa amepiga pasi saba za mwisho.

Kwa upande wa Aucho, amekuwa nguzo muhimu katika kuilinda safu ya ulinzi ya Yanga ambayo hadi sasa ndio imeruhusu idadi ndogo ya mabao katika Ligi Kuu ikifungwa mabao 11.

Yanga inaongoza msimamo wa Ligi Kuu ikiwa imekusanya idadi ya pointi 52 ilizovuna katika michezo 20, Azam ikiwa nafasi ya pili na pointi zake 47 ilizokusanya katika mechi 21 huku Simba iliyocheza michezo 19 ikiwa nafasi ya tatu na pointi 45

Chanzo: www.tanzaniaweb.live