Kiungo mkabaji wa Yanga, Khalid Aucho amezungumzia jinsi majeraha yalivyompunguzia kasi ya kupambana msimu huu (2023/24), hata hivyo kilichompa faraja ni timu hiyo kunyakua taji la ubingwa mara tatu mfululizo.
Aucho ambaye amechukua ubingwa mara mbili akiwa na Yanga aliyojiunga nayo msimu wa 2021/22 akitokea El Makkasa, alisema kuna kitu kimeongezeka kwenye karia yake, tangu aanze kucheza Ligi Kuu Bara hasa mafanikio aliyoyapata akiwa na klabu ya Wanajangwani.
“Ni ndoto ya kila mchezaji anapomaliza msimu avae medali ya ubingwa, nimebahatika kuchukua mara mbili kwa muda ambao nimekaa Yanga, hilo ni jambo kubwa kwenye CV ya kazi zangu,” amesema na kuongeza;
“Kitu kilichoniumiza ni kuumia ambako kulifanya nikae nje na kukosa baadhi ya mechi, kwani kuna wakati kama mchezaji nilikuwa natamani kuitumikia timu yangu mwanzo mwisho.
“Japokuwa kulikuwa na ushindani mkubwa, kila timu inayocheza Ligi Kuu ilikuwa inatamani kuchukua ubingwa, ila tumebahatika sisi, kilichotupa mafanikio ni upambanaji wa pamoja, tukiwa na malengo ya pamoja, hilo lilitupa nguvu ya kutimiza malengo yetu.”