Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Aubameyang afunguka chanzo ugomvi na Arteta

Auba Vs Arteta Aubameyang afunguka chanzo ugomvi na Arteta

Sat, 1 Jun 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Noma sana. Supastaa wa zamani wa Arsenal, Pierre-Emerick Aubameyang ameweka mambo hadharani akifuchua ugomvi wake na Mikel Arteta kwamba kocha huyo alimtuhumu kwamba anamsengenya!

Straika huyo mwenye umri wa 34, amefichua kilichotokea ambacho kimesababisha afungashe virago vyake na kuachana na Arsenal miaka miwili iliyopita baada ya kutibuana na kocha Arteta.

Auba alivuliwa unahodha wa Arsenal, Desemba 2021 baada ya kuchelewa kujiunga na timu yake akitokea Ufaransa.

Ilikuwa ni safari iliyofahamika kwa klabu, kwa sababu alisafiri kwenda kumwona mama yake aliyekuwa mgonjwa, lakini kwa kipindi kulikuwa na mazuio ya kusafiri ya kipindi cha Uviko 19, hivyo, mchezaji huyo alipaswa kusubiri kwa saa 24 kabla ya kuungana na wenzake na kumfanya akose mazoezi.

Arteta kwa hasira alimwambia gwiji huyo wa Gabon akafanye mazoezi kivyake na kumwondoa kabisa kwenye kikosi chake kwa mechi iliyofuata, ambapo Arsenal ilicheza na Southampton.

Auba alisema: “Niliwasili, kocha akiwa amemaliza kikao na wachezaji, alinishika mkono na kuanza kupayuka. Alipiga kelele ni kama vile chizi.

“Alisema, “Unanisengenya, huwezi kunifanyia hivyo mimi, hasa kwa nyakati hizi tunazopita.

“Kwa wakati huo, nilijiambia mweyewe, sitamjibu kitu isije tukaishia kwenye kuchukiana zaidi. Sikuwa nimekwenda kwenye sherehe. Alifahamu kila kitu sababu za mimi kusafiri, hivyo kwa kipindi hicho sikuwa nimemwelewa kabisa alivyokuwa akinipigia kelele.

“Nilitoka kwenda nyumbani, kisha daktari alinipigia simu na kuniambia,” kocha kasema, kesho asikuone, hakutaki”.

“Siku zilipita na daktari aliniambia, “Sikia, hakutaki tena uendelee

kuwapo kwenye timu. Unaweza kuja mazoezini, lakini utafanya kivyako.

“Nilijisemea mweyewe, sawa. Kisha kocha mwenyewe alinipigia simu na kuwa na kikao na hapo kwanza aliniambia, ananivua kitambaa cha unahodha na pili, sitafanya mazoezi na wachezaji wengine tena.”

Aubameyang, ambaye kwa sasa anakipiga huko kwenye kikosi cha Marseille ya Ufaransa, alisema alivyoona vile alifahamu wazi hatakutaka kuichezea tena Arsenal.

Machi 2021, Aubameyang aliwekwa benchi baada ya kudaiwa kuchelewa kwenye kikao cha timu kilichokuwa kikijiandaa na mechi ya mahasimu wao, Tottenham Hotspur.

Na ilipofika dirisha la Januari lilipofunguliwa, Arsenal ilitafuta namna ya kuachana na mshambuliaji huyo na hivyo iliingia kwenye mazungumzo na Barcelona kwa ajili ya kumpeleka huko bure kabisa ili asiendelee kuwapo kwenye kikosi chao huko Emirates.

Na hapo uhamisho wa kushtua ulifanyika baada ya Auba kuonekana akiwa Barcelona, huku ikidaiwa kwamba Arsenal ilikuwa haifahamu kama mchezaji huyo amekwenda huko.

Baadaye ilikuja kufahamika kwamba mkurugenzi wa michezo, Edu alikuwa na ufahamu Auba alikuwa anaelekea Barcelona.

Jambo hilo linadaiwa kumwingiza Auba kwenye msongo wa mawazo.

Auba alisema: “Iliniumiza sana. Kulianza kutoka mambo tofauti kabisa na maisha yangu. Nilianza kulewa sana. Kilikuwa kipindi kigumu sana kwangu.”

Auba alikamilisha uhamisho wake kwenda Barcelona, Februari 2022 baada ya Arsenal kusitisha mkataba wake na kumruhusu kuondoka bure kabisa.

Chanzo: Mwanaspoti