Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Atta: Hawa Horoya si mchezo

Atta Agyei Enock Atta Agyei

Thu, 23 Feb 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Utamu wa Mghana Enock Atta Agyei wanaujua Azam FC kwa sababu ndio timu iliyomtengeneza kisha ikamuanzishia maisha ya soka baada ya kumsajili 2016 na kudumu katika kikosi hicho hadi 2019 na kutimkia Guinea katika klabu ya Horoya.

Mshambuliaji huyu kwa sasa amerejea nchini na kutua Singida Big Stars katika dirisha dogo la msimu huu kwa mkataba wa miaka mitatu.

Mwanaspoti lilifanya naye mahojiano kuhusu urejeo wake huku akifunguka sababu ya kutoonekana uwanjani licha ya kucheza mechi za Kombe la Mapinduzi.

HOROYA SI MCHEZO

Atta anasema Horoya ni miongoni mwa timu kubwa na bora Afrika kutokana na namna ambavyo imejitengeneza nchini Guinea na inafuatiliwa na watu wengi.

Mshambuliaji huyo anasema akiwa Horoya maisha yalikuwa mazuri kutokana na mazingira na hakuwa na changamoto yoyote ile ndani na nje ya uwanja.

“Horoya ni timu kubwa sana kule na imekamilika katika kila idara. Ina ushindani wa kutosha kuanzia ndani ya kikosi na hata upande wa timu pinzani tulipokuwa tunakutana nazo wanajua siku hiyo kazi ni ngumu,” anasema Atta.

“Ukiwa pale muda wote unatakiwa uwe tayari kwa kila mchezo kwa sababu ni timu kubwa. Kwa muda wangu niliokuwa pale tulikuwa tunacheza ligi kama tatu na zote inabidi uwe tayari na kila mchezo mshinde.”

PLUIJM AMVUTA SINGIDA BIG STARS

Baada ya kuwa na maisha mazuri ndani ya Horoya na mkataba wake kumalizika, Atta anasema alishawishika kurejea Tanzania kuja kujiunga na kocha wake wa zamani, Hans van Pluijm.

Anasema Pluijm ni kocha ambaye hapendi mchezaji apoteze kipaji chake kirahisi kwa sababu siku zote anapenda wapambanaji ndani ya timu yake.

“Ni kocha ambaye alinipa wakati mzuri na hapendi mtu upotee. Kufanya naye kazi katika miaka ya nyuma katika kikosi cha Azam na mambo tuliyofanya pamoja yamechangia kuwa hapa kwani tunaweza kufanya zaidi ya tuliyofanya.

“Azam ni nyumbani kwangu na nina maelewano mazuri pale, lakini nilikuwa nahitaji kwanza kupata changamoto mpya na ndio maana nikaja hapa (Tanzania).”

ITC YAMCHELEWESHA

Baada ya kujiunga na Singida Big Stars kwenye dirisha dogo hadi sasa, Atta hajacheza mchezo wowote na yeye mwenyewe anakiri kilichochangia yote hayo kuwa ni kutokana na hati ya usajili wa kimataifa (ITC) kuchelewa kufika nchini.

Anasema wakati akiendelea kuisubiri ITC anafanya mazoezi na kikosi ili kujiweka fiti kwa asilimia 100.

“Kuna muda ni ngumu kuwa unafanya mazoezi tu halafu huchezi, lakini wakati mwingine ni vizuri kusubiri kwa sababu unakuwa umejiandaa vizuri na utakaporudi ni kufanya kazi tu,” anasema.

Akizungumzia changamoto ya namba kikosini kutokana na aina ya usajili ambao umefanywa na Singida Big Stars, Atta anasema huwa hafikirii ushindani na mtu.

“Sina changamoto ya namba na mtu yeyote yule. Kikubwa fanya mazoezi ya kutosha, jitume na kuisaidia timu pale inapohitajika. Huwa najipa changamoto mwenyewe kwa kujituma,” anasema.

AMZUNGUMZIA MAKAMBO

Atta na aliyekuwa mshambuliaji wa Yanga, Heritier Makambo walicheza pamoja kwenye kikosi cha Horoya, lakini msimu uliopita Makambo akarejea nchini na kujiunga na Yanga.

Katika msimu huu wakati Atta anaingia Singida Big Stars, Makambo ametoka kwenye kikosi cha Yanga na kuwafanya wawili hao wapishane Ligi Kuu Bara.

Akimzungumzia Makambo, Atta anasema ni mchezaji mzuri na anajua kufunga lakini kuondoka kwake Horoya ni sehemu ya maisha ya wachezaji kwenye kusaka changamoto mpya za maisha.

“Nimecheza na Makambo na ni mshambuliaji mzuri sana. Anajituma sana, kuondoka kwake pale nadhani ni kuhitaji changamoto mpya tu na si kingine.”

AIONA SINGIDA BIG STARS CAF

Kumbe lile analosema kocha wa Singida Big Stars, Pluijm kwamba lengo ni kumaliza nafasi nne za juu ili washiriki mashindano ya kimataifa limewaingia hadi wachezaji baada ya Atta kuweka wazi hilo.

Mchezaji huyo anasema timu yao ina wachezaji wazuri ambao wanaweza kufanya vizuri na kumaliza nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi na kukata tiketi ya kucheza mashindano ya CAF msimu ujao.

“Kama sio Ligi ya Mabingwa Afrika, basi hata Shirikisho tunaweza kushiriki msimu ujao. Kwa ambacho nakiona hapa tuna timu nzuri ambayo inampa changamoto kila moja,” anasema Atta.

“Mimi pia nikichanganya na uzoefu niliokuwa nao kwa kushirikiana na wenzangu imani yangu inaniambia tutapata kitu kikubwa zaidi.”

LIGI YA BONGO KIBOKO

Atta anasema kwa sasa Ligi Kuu Bara inazidi kuwa ngumu kwa kuwa hakuna timu ambayo ni nyepesi kutokana na kila moja kujipanga vyema pamoja na kuwa na uwezo wa kusajili wachezaji zinaowataka.

Mshambuliaji huyo anasema jambo hilo linaifanya ligi iwe ngumu na ndio maana hata mabosi wake wa zamani, Azam, wanapata wakati mgumu kuchukua ubingwa.

“Kwa sasa hauwezi kudharau timu yoyote ile kwa sababu wachezaji wote wanajituma na ni jambo zuri kuona ligi ya namna hiyo. Timu zimewekeza kwenye usajili wa wachezaji wazuri,” anasema mchezaji huyo.

“Azam ina kikosi kizuri, lakini inatakiwa iendelee kupambana na muda ukifika kila kitu kitakuwa sawa.”

Chanzo: Mwanaspoti