Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Atapasuka mtu kwa Mkapa leo

Yanga Vs Kmc Pic Kiungo wa Yanga, Mudathir Yahaya

Wed, 22 Feb 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Hesabu ni ile ile moja , kushinda mechi zake tu. Ndiyo wanayoingia nayo Yanga leo katika mchezo dhidi ya KMC utakaochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa leo kuanzia saa 10 jioni.

Matokeo yoyote ya mchezo wa jana baina ya Simba na Azam FC hayatakuwa na athari kwa Yanga iwapo itapata ushindi leo kwani itafikisha jumla ya pointi 62 na hivi kuhitajika kushinda mechi nne tu zitakazofuata ili ijihakikishi rasmi taji la Ligi Kuu msimu huu.

Yanga imekuwa na historia ya ubabe dhidi ya KMC kwani imeibuka na ushindi mara nyingi zaidi pindi walipokutana katika mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara kwa nyakati tofauti.

Timu hizo zimekutana katika mechi tisa za ligi na Yanga imeibuka na ushindi katika mechi sita, ikipoteza moja na kutoka sare michezo miwili, ikifunga mabao 12 huku KMC yenyewe ikifumania nyavu mara tano tu.

Hapana shaka presha ni kubwa kwa upande wa KMC kutokana na mwenendo mbovu walionao Ligi Kuu siku za hivi karibuni ambao umesababisha wawe katika nafasi isiyoridhisha kwenye msimamo wa ligi.

Timu hiyo haijapata ushindi katika mechi tano mfululizo zilizopita za ligi na imefungwa michezo minne na kutoka sare mmoja huku ikifunga mabao manne na kuruhusu nyavu zao kutikiswa mara 10.

Hadi sasa, KMC inashika nafasi ya 12 katika msimamo wa ligi ikiwa imekusanya pointi 23 ambazo ni sita tu zaidi ya zile za Ruvu Shooting inayoshika mkia.

Hata hivyo, Kocha msaidizi wa KMC, Ahmad Ally alisema watapambana kuhakikisha wanafanya vizuri dhidi ya Yanga ili wajiondoe katika nafasi waliyopo sasa.

“Tangu mechi ya mwisho tulipocheza tumepata mechi tatu za kirafiki ambazo zimewajengea wachezaji utimamu wa mwili ingawa sio za kimashindano tofauti na wapinzani wetu ambao walikuwa katika mechi za kiushandani. Wachezaji wetu wapo katika morali kubwa ya mechi ingawa tutamkosa Hance Maoud ambaye ni majeruhi wa muda mrefu,” alisema Ally.

Wakati KMC wakijipanga kusaka ushindi kwa Yanga tangu walipofanya hivyo kwa mara ya mwisho mwaka 2020, Yanga kwa upande wao wametamba hesabu zao ni kuendelea kufanya vizuri ili wazidi kujikita katika kilele cha msimamo wa ligi.

“Kikubwa ambacho tumekifanya kwa wachezaji ni kuwakumbusha waachane na furaha ya ushindi katika mchezo uliopita dhidi ya TP Mazembe na akili yao ifikirie zaidi mchezo dhidi ya KMC ambao uko mbele yetu tunaohitaji kupata ushindi ili utuweke katika mazingira mazuri ya kutetea ubingwa wetu,” alisema Kocha msaidizi wa Yanga Cedrick Kaze.

Chanzo: Mwanaspoti