Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Aston mbunifu aliyeleta matumizi ya kadi mbili katika soka

Kenneth George Aston Pencipta Kartu Merah Dan Kuning Dalam Sepakbola Kenneth George Aston

Fri, 17 Feb 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Wapo watu ambao kila zikifanyika simulizi za maendeleo ya mchezo wa kandanda inakuwa sio haki kutowataja walichofanya wakiwamo wachezaji, waamuzi, viongozi au mashabiki. Mmojawao ni aliyekuwa mwamuzi wa mchezo huu wa Uingereza, Kenneth George Aston aliyeishi kati ya 1915- 2001, ambaye mwanzoni mwa mwaka huu alikuwa miongoni mwa waliotunukiwa nishani na mfalme wa Uingereza, Charles III miaka 22 baada ya kuaga dunia.

Mchezo huu umepitia hatua nyingi za mabadiliko ya kimfumo wa uchezaji, mavazi na vifaa, sheria, taratibu na mambo mengine mengi. Kwa miaka mingi mchezaji aliyevunja sheria alionywa kwa kunyooshewa kidole na mwamuzi, kuambiwa alivyofanya sio vizuri au kumuonyesha mkono wa kumtoa nje ya uwanja.

Baadhi ya nyakati ishara zilizua mzozo na ilikuwa rahisi mwamuzi kubadili msimamo alipoombwa samahani na mchezaji. Hatimaye mwaka 1966 Aston alikuja kufungua ukurasa mpya wa historia ya mchezo huu kwa kuchukua hatua iliyobuni sheria na kanuni mpya za kutumia kadi za njano kama onyo na nyekundu kumtoa mchezaji nje ya uwanja.

Aston ambaye baada ya mchezo wa Argentina na England katika fainali za Kombe la Duni 1966 zilizofanyika Uingereza zilisikika taarifa za mchezaji wa England, Bobby Charlton kustahiki kutolewa kwa vile hapo kabla alionywa na mwamuzi wa Ujerumani, Rudolf Kreitlein. Lakini Charlton alibaki uwanjanai na kuendelea na mchezo.

Suala hili lilimuumiza kichwa Aston ambaye alikuwa kiongozi wa jopo la waamuzi katika fainali zile. Wakati akiendesha gari kutoka Uwanja wa Wembley kwenda nyumbani kwake Lancaster Gate alikuwa anasumbuliwa na suala la Charlton.

Akiwa njiani alisimama kwenye taa zinazoongoza magari na kuangalia taa za njano na nyekundu zilivyosaidia kuongoza magari kwa usalama kwa ile ya njano kutoa onyo na nyekundu kumsimamisha dereva. Hapo ikamjia dhana ya kutumia mfumo huo katika soka kwa mchezaji kuonywa kwa kupewa kadi ya njano na kusimamishwa kuendelea na mchezo kwa kupewa kadi nyekundu.

Alipofika nyumbani alimweleza mkewe Hilda usumbufu alionao na mawazo aliyopata alipoangalia taa za kuongoza magari alipokuwa anarudi nyumbani. Mkewe, Hilda aliyekuwa akimsikiliza kwa makini aliondoka polepole na kurudi baada ya dakika chache akiwa na kadi mbili, njano na nyekundu za gamba gumu la karatasi ambazo alizitumbukiza ndani ya shati la Aston.

Hilda alimwambia ikitokea amemuudhi amuonyeshe kadi ya njano kama onyo na akimkasirisha amfukuze kwa kumpa kadi nyekundu. Hicho ndicho chanzo cha wachezaji kupewa kadi katika kandanda na zilianza kutumika kwa mara ya kwanza katika fainali za Kombe la Dunia za 1970 zilizofanyika Mexico na Brazil iliyokuwa na Pele, Jairzinho, Rvelino na Tostato kuwa mabingwa kwa kuifunga Italia mabao 4-1 katika fainali.

Matumizi ya hizi kadi pia yalitumika kwa michezo mengine, lakini kwa matumizi tofauti ya sheria na kanuni za michezo hiyo. Maisha ya Kenneth George Aston aliyezaliwa Colchester, Uingereza, Septemba Mosi, 1915 ni yenye simulizi nyingi katika kandanda.

Baada ya kumaliza masomo Chuo cha St Luke, Exeter alianza kazi ya ualimu. Baadaye alijiunga na jeshi la ardhini katika Vita Kuu vya Pili vya Dunia na kupelekwa India na Singapore, ambako alipanda vyeo na kufikia luteni kanali.

Vita vilipomalizika 1945 alifanya kazi katika Tume ya Kuchunguza Uhalifu wa Vita uliofanyika katika kambi ya Japan ilipokuwa Singapore. Baadaye alirudia kufundisha kwa miaka zaidi ya 20 huku akitumia muda mwingi katika masuala ya soka, hasa fani ya uamuzi.

Miongoni mwa michezo yenye utata mkubwa aliyoisimamia kama mwamuzi ni wa ufunguzi wa fainali za Kombe la Dunia za 1962 zilizofanyika Chile kwa wenyeji kupambana na Italia. Alichukua nafasi hiyo baada ya mwamuzi aliyepangiwa kwanza kuchezesha kukataa kwa kuhofia usalama wa maisha yake.

Siku chache kabla ya mchezo huo magazeti ya Italia yaliandika makala nyingi za kuzungungumzia ukahaba uliokithiri wa wanawake wa Chile na yale ya Chile yakasema wanachoabudu Wataliano ni dawa za kulevya na ufuska.

Katika mchezo ule uliojaa mateke uwanjani na matusi kutoka kwa watazamaji 66,000 walioshuhudia mchezo Chile ilishinda kwa maba 2-0. Kadi ya kwanza nyekundu ilitolewa katika fainali za 10 za mashindano hayo zilizofanyika Ujerumani Magharibi kwa Carlos Caszely wa Chile katika dakika ya 67 kwani awali alipewa kadi ya njano katika dakika ya 13.

Aston alifaulu kuwa mwamuzi wa kandanda 1936 na kuwa mshika bendera katika Ligi ya England msimu wa 1949-50. Aliwashangaza watu alipojitokeza kuwa mwamuzi wa kwanza kuvaa sare nyeusi, kivazi ambacho kilikuja kutumika kila nchi. Kabla ya hapo waamuzi walivaa mashati ya rangi nyeupe na majaketi.

Mwaka 1947 alianzisha mfumo wa kutumia bendera nyekundu badala ya zile za rangi mbalimbali zilizotumika wakati ule. Mwaka 1966 Aston alianzisha mfumo wa kuwa na mwamuzi wa akiba ili kuchukua nafasi ya mwamuzi atayeshindwa kuendelea na mchezo kwa sababu mbalimbali kama ugonjwa wa ghafla.

Vilevile alitoa ushauri wa kuwepo kipimo maalumu cha pumzi za mpira na kufanikiwa kukiingiza katika sheria za mchezo huo. Mwaka 1974 alianzisha mtindo wa kutumia vibao venye namba ya mchezaji anayetakiwa kubadilishwa badala ya kupiga kelele za kumuita kwa jina aliyetakiwa kubadilishwa na kocha.

Kuanzia 1980 mpaka alipofariki dunia akiwa na umri wa miaka 83 Aston hakuwa mbali na kandanda na mara nyingi alifika uwanjani na wajukuu zake.

Chanzo: Mwanaspoti