Leo mchana klabu ya Singida FG imetoa taarifa kwa vyombo vya habari ikizungumzia kuhusu kipa wake Benno Kakolanya kuondoka kambini kwao, wakati wakijiandaa na mchezo dhidi ya Yanga Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza unaotarajiwa kuchezwa alasiri hii.
Mchezaji wa zamani wa Kariakoo Lindi, Mukura Victory ya Rwanda, 82 Rangers na Kahama United zote za Shinyanga, Vijana ya Ilala, Dar es Salaam na timu ya Taifa 'Taifa Stars', Jemedari Said Kazumari, ameandikia kupitia mtandao wake wa kijamii kuwa tukio kama hilo liliwahi kutokea kwa timu ya Bandari Mtwara ilipokuwa ikijiandaa kucheza na Yanga mwaka 1991 mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza (sasa Ligi Kuu Tanzania Bara).
"Mwaka 1991 timu ya Bandari ya Mtwara ikiwa inajiandaa kucheza mechi ya Ligi daraja la kwanza (sasa Ligi Kuu) dhidi ya Yanga SC ya Dar es Salaam, ilipatwa mkasa wa kukimbiwa na mganga wake waliyefanya nae kazi msimu mzima wa mwaka 1990 wakiwa daraja la pili.
"Mzee huyo alifahamika kwa jina moja la Mzee Namoto alikuwa anaishi Railways nyumbani kwa marehemu Mzee Mussa Mnyelema jirani na nyumbani kwetu. Mzee Namoto aliamka zake alfajiri akaenda kuswali Msikiti wa Railways siku ya mechi, alipotoka huko hakuonekana mpaka baada ya mchezo ambao Bandari walipoteza kwa mabao 4-2.
"Mzee Namoto alipokuja kuonekana baada ya mechi akaulizwa kilitokea nini alijibu kirahisi tu: “Mimi siwezi kuiroga Yanga, Yanga mimi imenipandisha ndege kwa mara ya kwanza katika maisha yangu na imenipeleka mpaka nje ya nchi, siwezi kuiroga ikafungwa”,ameandika Jemedari ambaye pia ni mchambuzi mahiri nchini wa masuala ya michezo na kuongeza kuwa. "Wacha tumsubiri Beno Kakolanya akirudi kutoka kusikojulikana atasemaje au atakuwa kama Mzee Namoto?"