Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Arteta ana jambo lake, Klopp, Pep watajibeba

Mikel Arteta Arsenal V Man City 1 Kocha wa Arsenal Mikel Arteta

Sat, 9 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Bato la Jurgen Klopp na Pep Guardiola. Mahasimu wakubwa kwenye Ligi Kuu England kwa muongo wa karibuni. Lakini, kesho Jumapili, kinapigwa kipute cha mwisho kwa mahasimu hao kumenyana kwenye Ligi Kuu England.

Mwisho wa msimu, mmoja ataondoka. Klopp ametangaza kwamba ataachana na timu yake ya Liverpool msimu huu utakapofika tamati.

Lakini, mchezo wao huo, unakuja wakati mzuri, vita ya kusaka ubingwa wa Ligi Kuu England ikizidi kunoga. Chama la Klopp, Liverpool ndilo linaloshika usukani wa Ligi Kuu England kwa sasa, pointi 63 kileleni. Lakini, amelizidi chama la Guardiola, Manchester City kwa pointi moja tu, ambapo wababe hao wa Etihad wapo nafasi ya pili na pointi zao 62.

Utamu wote utakuwa huko Anfield. Kuna mambo mengi yanakwenda kutokea kwenye mchezo huo.

1. Klopp afanikiwe kulinda pengo la pointi na kubakia hiyo hiyo moja.

2. Guardiola amshushe Klopp na kuweka pengo la pointi mbili.

3. Klopp aweke pengo la pointi na kufikia nne dhidi ya Guardiola.

KIPI KITAKWENDA KUTOKEA?

Rekodi zinaonyesha kwamba Klopp na Guardiola wamekutana mara 15 kwenye Ligi Kuu England, ambapo wametoka sare mara sita, huku Guardiola akishinda tano na Klopp nne. Unaweza kuona vita yao ilivyokuwa na ukali.

Kuhusu rekodi ya timu zenyewe, Liverpool na Man City zimekutana mara 53 kwenye Ligi Kuu England. Mara 20 miamba hiyo imetoka sare, wakati Liverpool imeshinda 21, mara 17 nyumbani uwanjani Anfield na mara nne imefanya hivyo kwenye uwanja wa ugenini, Etihad.

Man City imepata ushindi mbele ya Liverpool mara 12 tu, 10 kwenye uwanja wake wa nyumbani Etihad na mara mbili tu, ugenini Anfield. Hivyo, mchezo huo, Liverpool inakwenda kusaka ushindi wake wa 18 nyumbani dhidi ya Man City, huku Man City yenyewe ikienda Anfield kusaka ushindi wao wa tatu.

Nani atamtambia mwenzake, Klopp au Guardiola? Kazi ipo.

ARSENAL YACHEKELEA

Kama kuna wikiendi ambayo Arsenal itacheza mechi yake ikiwa na furaha kubwa basi ni hii, kwa sababu wapinzani wake wawili, Liverpool na Man City watamalizana wenyewe huko Anfield. Uzuri kwa kikosi hicho cha kocha Mikel Arteta ni kwamba wakati Liverpool na Man City zikisubiri kumalizana kesho Jumapili, wao The Gunners watashuka uwanjani Emirates, leo Jumamosi kukipiga na Brentford. Ushindi wa Arsenal kwenye mechi hiyo, utafanya kikosi hicho cha Arteta kupata kileleni kwenye msimamo wa Ligi Kuu England kwa kukusanya pointi 64, moja zaidi ya Liverpool na mbili zaidi ya Man City. Arteta ataomba asipatikane mshindi huko Anfield ili amalize wikiendi hii yeye na kikosi chake kuwa kileleni kwenye msimamo wa Ligi Kuu England, kutokana na kuwa na wastani mzuri wa kufunga na kufunga. Sare itaifanya Liverpool kufikisha pointi 64, sawa na ambazo itakuwa imevuna Arsenal itakapoichapa Brentford.

Lakini, vijana wa Emirates wana wastani mzuri wa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa. Arsenal ina mabao 45, Liverpool 39 na Man City 35.

Rekodi za Arsenal na Brentford kwenye Ligi Kuu England zinasoma kwamba timu hizo zimekutana mara tano, sare moja, huku Arsenal ikishinda tatu, moja nyumbani na mbili ugenini, huku Brentford imeshinda moja tu, ilipocheza nyumbani.

MAN UNITED VITA YA TOP FOUR

Manchester United ipo nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi Kuu England, pointi 11 nyuma kuifikia Aston Villa iliyopo kwenye Top Four.

Man United imekusanya pointi 44, pointi sita nyuma ya timu inayoshika nafasi ya tano kwenye msimamo huo, Tottenham Hotspur.

Kwa mechi ambazo zimebaki kwenye Ligi Kuu England, Man United kuwepo kwenye Top Four ili kukamatia tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao itahitaji kugangamala kwelikweli kwa maana ya kushinda mechi zake, pengine zote zilizobaki. Mchana wa leo, Jumamosi watajimwaga uwanjani kwao Old Trafford kuwakabili Everton katika mechi inayotazamiwa kuwa na upinzani mkali ndani ya uwanja.

Man United na Everton zimekutana mara 63 kwenye Ligi Kuu England, ambapo mara 13 timu hizo zilitoka sare, huku Mashetani Wekundu wakishinda 40, mara 21 ilipocheza Old Trafford na 19 ugenini uwanjani Goodison Park.

Everton yenyewe imeshinda 10, nane nyumbani na mbili tu ugenini. Mechi tano za mwisho, Man United imeshinda tatu, Everton moja na sare moja. Man United ikishindwa kupata ushindi mbele ya Everton, kisha West Ham United ikiwachapa Burnley basi wataiporomosha kwenye msimamo timu hiyo ya Erik ten Hag hadi kwenye nafasi ya saba.

KUSHUKA DARAJA PATAMU

Kwenye msimamo wa Ligi Kuu England unavyosoma, timu tatu za chini, Sheffield United imekusanya pointi 13 katika mechi 27, Burnley pointi 13 katika mechi 27 na Luton Town pointi 20 katika mechi 26. Hizo ndiyo timu tatu za mkiani kwenye msimamo wa Ligi Kuu England.

Lakini, vita ya kushuka daraja inaweza kuwahusu pia timu nyingine kama Nottingham Forest, Everton, Brentford, Crystal Palace na Bournemouth.

Wikiendi hii, Sheffield utakuwa ugenini huko Vitality kucheza na Bournemouth, katika mechi inayotazamiwa kuwa na upinzani mkali kutokana na kila timu kujaribu kutafuta pointi za kuwaweka salama kwenye ligi.

Rekodi zinaonyesha Bournemouth na Sheffield United zimekutana mara tatu kwenye Ligi Kuu England, ambapo kila mmoja ameshinda mara moja na mechi moja iliyobaki ilimalizika kwa sare. Je, kuna mbabe atapatikana leo? Luton Town wao vita yao ya kujinasua kwenye kasheshe la kushuka daraja, watakipiga na Palace, ambayo pia haipo salama.

Mechi hiyo itapigwa Selhurst Park, ambapo rekodi zinaonyesha Palace na Luton zimekutana mara moja tu kwenye Ligi Kuu England, ambapo mechi hiyo ni ya msimu huu, iliyoshuhudia Luton ikishinda ilipocheza nyumbani.

Burnley yenyewe itakuwa ugenini kukipiga na West Ham katika kipute kitakachopigwa huko London. Miamba hiyo imekutana mara 17 kwenye Ligi Kuu England, ambapo mechi tatu zilimalizika kwa sare, huku West Ham ikishinda tisa, tano nyumbani na nne ugenini, wakati Burnley imeshinda tano, mara tatu nyumbani na mbili tu ugenini.

Nottingham Forest wao kasheshe lao litakuwa ni kuwakabiri Brighton ugenini. Forest inatambua wazi haipo salama, hivyo itahitaji kushinda mechi zake kutoka sasa hadi mwisho wa msimu ili kubaki Ligi Kuu England.

Namba zinaonyesha timu hizo zimekutana mara tatu kwenye Ligi Kuu England na kila moja imeshinda mara moja, huku mechi nyingine ilimalizika kwa sare. Mchezo wa mzunguko wa kwanza kwenye ligi, Brighton ilishinda.

ASTON VILLA VS SPURS; VITA MAALUMU

Kwenye msimamo, Aston Villa imekusanya pointi 55 katika mechi 27, wakati Tottenham Hotspur imekusanya pointi 50 katika mechi 26. Timu moja ipo nafasi ya nne na nyingine kwenye namba tano. Kitu kitamu ni kwamba kesho timu hizo mbili zitakutana zenyewe na matokeo ya mechi hiyo yatatoa taswira halisi ya timu yenye uwezo wa kumaliza ndani ya Top Four na kufuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

Ushindi wa Spurs, utafanya pengo la pointi kupungua na kufikia mbili na endapo kama watashinda mechi yao moja ya kiporo, basi wataweza kuishusha Aston Villa. Lakini, vijana wa Unai Emery, ambapo watakuwa Villa Park, endapo watashinda, wataweka pengo la pointi kufikia nane na hapo watakuwa wamejiimarisha zaidi katika kufukuzia nafasi hiyo ya kucheza michuano ya Ulaya msimu ujao. Rekodi zinaonyesha Aston Villa na Spurs kwenye Ligi Kuu England zimekutana mara 57, mara 15 zilitoka sare, wakati Villa imeshinda 18, mara 10 nyumbani na nane ugenini, huku Spurs ikishinda 24, mara 14 nyumbani na 10 ugenini. Safari hii, itakuwaje? Ngoja tuone.

MECHI NYINGINE

Kwenye mchakamchaka wa Ligi Kuu England utamu mwingine utakuwa huko Molineux hii leo, wakati Wolves itakapokuwa na kazi nzito mbele ya Fulham. Wolves na Fulham kila timu inasaka pointi za kuwafanya kuendelea kubaki kwenye Ligi Kuu England msimu ujao. Rekodi zao zinaonyesha timu hizo zimekutana mara 15 kwenye ligi, Wolves ikishinda sita, tano nyumbani na moja ugenini, huku Fulham ikishinda tatu tu, zote nyumbani na mechi sita zilimalizika kwa sare. Chelsea inayojitafuta itakuwa nyumbani Stamford Bridge keshokutwa Jumatatu kukipiga na Newcastle United. Bonge la mechi.

Namba zinaonyesha timu hizo zimekutana mara 57 kwenye Ligi Kuu England, ambapo The Blues imeshinda 29, mara 20 nyumbani uwanjani Stamford Bridge na mara 9 ugenini, huku Newcastle yenyewe imeshinda 15, mara 14 nyumbani na moja tu ugenini. Miamba hiyo imetoka sare mara 13.

Chanzo: Mwanaspoti