Baada ya ubishi wa muda juu ya nafasi gani zaidi inamfaa staa wa Arsenal, Kai Havertz kucheza uwanjani Kocha Mikel Arteta amemaliza ubishi kwa kutaja nafasi rasmi ya staa huyo.
Havertz ambaye amejiunga na Arsenal kwa ada ya Pauni 65 milioni kutoka Chelsea katika dirisha lililopita la majira ya kiangazi hivi karibuni ameonyesha kiwango bora akifanikiwa kufunga mabao matano katika mechi saba za mwisho za ligi.
Alipojiunga katika mechi za mwanzo alikuwa akichezeshwa kama kiungo mshambuliaji mbele ya Declan Rice na Martin Odegaard. Pia katika tovuti ya Arsenal nafasi yake iliyoandikwa ilikuwa ni kiungo.
Lakini tangu kuanza kwa mwaka huu, Havertz ameonekana kwenye safu ya ushambuliaji na amekuwa akifanya vizuri.
Uwezo wake wa kufunga umekuwa ukizua mjadala anafaa zaidi kuwa namba tisa kuliko kiungo kama invyotambulika.
“Nafikiria anafanya vizuri akicheza namba tisa, lakini anafanya hivyohivyo akiwa namba nane. Lakini sina uhakika sana juu ya nini kinamfanya awe bora akiwa namba tisa au nane, mara nyingi huchangia na aina ya mechi na tabia ya timu pinzani na nafasi anayocheza. Siwezi kusema anakuwa anajisikia huru zaidi akicheza namba tisa.”
Havertz mwenyewe amewahi kuulizwa juu ya hili mwezi uliopita baada ya mchezo wa Arsenal na Brentfordna akasema: “Sijui ni mara ngapi nimejibu swali hili, lakini niseme najisikia furaha tu niwapo uwanjani, mimi sio mchezaji ambaye anacheza nafasi moja, naweza kucheza namba tisa, nane na 10 na popote utakapohitaji nicheze, nikiwa Ujerumani niliwahi kucheza kama beki wa kushoto kwahiyo kwangu mimi ni sawa tu.”