Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Arteta: Hatutumii pesa

Pic Arteta Data Arteta: Hatutumii pesa

Tue, 6 Aug 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta amesisitiza kwamba timu hiyo haitavunja rekodi ya usajili kwa kutumia kiasi kikubwa cha pesa kununua mchezaji mmoja katika dirisha hili kama ilivyokuwa mwaka jana.

Washika Mitutu hao wa London, Juni, mwaka jana walifanikiwa kumsajili,  Declan Rice kutoka West Ham United kwa dau la Pauni 105 milioni kiasi ambacho kilivunja rekodi ya timu hiyo.

Nyota huyo katika msimu wa kwanza alicheza mechi 51 za michuano yote na akafunga mabao saba na kutoa asisti 10. Licha ya kufanya vizuri na kulipa thamani ya pesa aliyosajiliwa nayo, Arteta ameweka wazi kwamba dirisha hili hawatafungua tena mfuko kiasi hicho.

“Hatutarajii kufanya kitu kama hicho. Huo ndio ukweli, lazima tusubiri kuona mwenendo sokoni. Tayari tumetaja maeneo ambayo tunaweza kuyaboresha. Hadi sasa ninafuraha juu ya kikosi nilichonacho,” alisema kocha huyo.

Katika dirisha hili Arsenal imeonekana kuwa kimya zaidi kuliko ilivyokuwa msimu uliopita ambapo hadi sasa imesajili wachezaji wawili ikiwa pamoja na kipa David Raya aliyesainishwa mkataba wa kudumu baada ya kufurahishwa na kiwango alichoonyesha alipocheza kwa mkopo msimu uliopita.

Mbali ya Raya pia imemsajili  Riccardo Calafiori kutoka Bologna  aliyetua kwa Pauni 40 milioni akiwa ni beki wa 11 kusajiliwa na Arsenal tangu Arteta aingie katika timu akitumia zaidi ya Pauni 240 milioni.

Taarifa nyingine zinaeleza kwamba Arsenal bado ipo sokoni kutafuta mshambuliaji mpya atakayesaidia kupunguza mzigo wa ufungaji mabegani mwa Bukayo Saka na katika majina yanayotajwa ni  mshambuliaji wa Sporting CP, Viktor Gyokeres na Leroy Sane wa Bayern Munich.

Arsenal pia inadaiwa pia inataka kuuza baadhi ya wachezaji wake wa kikosi cha kwanza ambapo baada ya kuanza na Emile Smith Rowe aliyetua Fulham kuna Eddie Nkeitah anaywindwa vikali na Marseille ya Roberto de Zerbi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live