Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Arteta: Hapa hatutoboi

Bosi Wa Zamani Wa Arsenal Adai Arteta 'amechafua Picha Ya Klabu' Mikel Arteta

Wed, 24 Jul 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Mapema tu Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta ameona afunguke kuhusu msimu ujao wa Ligi Kuu England kutokana na kile kinachoendelea katika kikosi chake na hadi sasa bado haijasajili nyota yeyote na kuna maeneo anayaona kabisa kama hayatashughulikiwa dirisha hili basi hawatakuwa na chao Ligi Kuu England itakapoanza.

Dirisha la usajili Ulaya liko wazi kwa sasa na miamba ya soka huko inapambana kushusha mashine za kuvifanya vikosi vyao kuwa moto, lakini kwa Arsenal ambayo imekuwa ikihusishwa na wachezaji wengi, hadi sasa bado haijasajili nyota yeyote.

Arteta amesema Arsenal inahitaji kufanyiwa maboresho ili kufanya vizuri kwenye ligi hiyo maarufu zaidi duniani kabla mambo hayajawa magumu watakapoanza msimu.

Kwa sasa miamba hiyo ambayo ilimaliza nafasi ya pili msimu uliopita na almanusura ibebe taji hilo, kabla ya kuzuiwa na Manchester City ya Pep Guardiola ikiwa bingwa kwa tofauti ya pointi mbili, ipo Marekani ikijiandaa na msimu ujao na itakuwa na mechi za kirafiki dhidi ya Bournemouth na Manchester United ndani ya wiki hii.

“Tunapaswa kuboresha, unahitaji kuwa na wachezaji bora katika kila eneo ili kushinda Ligi Kuu, hivyo ndivyo tunapaswa kuboresha kikosi kwa sasa.”

“Siwezi kusema ni eneo gani tunalopaswa kuboresha moja kwa moja, tunahitaji kuboresha karibia kila eneo na vitu vyote tunavyofanya,” alisema Arteta.

Kocha huyo pia alipoulizwa kuhusu beki wa Bologna, Ricardo Calafiori ambaye uhamisho wake unaweza kukamilika kabla ya wiki hii kuisha kama ni sehemu ya maboresho hayo alisema:

“Sidhani kama eneo hilo tunahitaji kufanya maboresho sana, kimsingi sisi tunajua ni nafasi zipi tunatakiwa tuziboreshe na tutajaribu kadri ya uwezo wetu kuhakikisha tunaziweka sawa.”

Katika kikosi hicho cha washika mitutu hao kilichopo Marekani, baadhi ya wachezaji ikiwemo Bukayo Saka, Declan Rice na Aaron Ramsdale hawamo baada ya kupewa mapumziko kwa kuwa walikuwa wakiitumikia England katika michuano ya Euro na walifika fainali dhidi ya Hispania.

Katika michuano hiyo staa wa Arsenal, Saka alifunga penalti katika robo fainali dhidi ya Uswizi ambayo iliondoa mzimu wake wa kukosa penalti katika fainali ya Euro mwaka 2020 dhidi ya Italia ambapo mashabiki wengi walimwandama katika mitandao ya kijamii na kumfanyia vitendo vya kibaguzi.

Kuhusu hilo Arteta alisema: “Nilikuwa na wasiwasi sana, kama bado lile tukio lilikuwa linaishi katika akili yake, lakini alionyesha ujarisi wa hali ya juu na utulivu, kiukweli siku hadi siku (Saka), anazidi kuimarika amekuwa mchezaji muhimu kwetu na timu ya taifa pia.”

Mbali ya mechi za wiki hii, Arsenal inatarajiwa kucheza mechi nyingine za kirafiki kuanzia Agosti 01 na itacheza dhidi ya Liverpool kisha itakutana na Bayer Leverkusen Agosti 07 na mwisho dhidi ya Olympique Lyon, Agosti 11 siku sita kabla ya kuanza rasmi kampeni za kulisaka taji la Ligi Kuu England dhidi ya Wolves Agosti 17, mchezo utakaopigwa Uwanja wa Fly Emirates kuanzia saa 11:00 jioni.

Chanzo: Mwanaspoti