Mikel Arteta, Xabi Alonso, Cesc Fabregas na Robert Lewandowski ni miongoni mwa mastaa wenye majina makubwa waliovuna tuzo kwenye sherehe za Globe Soccer Awards zilizofanyika usiku wa Jumanne.
Tukio hilo lilifanyika kwenye ukumbi wa Hotel Cala di Volpe uliopo Sardinia, Italia.
Mtangazaji wa televisheni, mrembo Melissa Satta alisimamia shoo hiyo iliyoshuhudiwa tuzo kibao za maana zikitolewa.
Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta alikuwa miongoni mwa waliohudhuria, akiwa ameambatana na mkewe, Lorena Bernal.
Mrembo Lorena, 43, alifurahi wakati mumewe, Arteta, 42, alipokabidhiwa tuzo ya Kocha Bora wa Ligi Kuu England, licha ya kikosi chake kukosa ubingwa mbele ya Manchester City kwenye siku ya mwisho ya msimu.
Rafiki wa muda mrefu wa Arteta, Xabi Alonso, naye alikuwapo kwenye tuzo hizo sambamba na mkewe mrembo Nagore Aranburu. Alonso, ambaye ni kocha wa Bayer Leverkusen, alibeba tuzo ya Kocha Bora wa Mwaka.
Alonso, 42, alikuwa na msimu bora kabisa huko Bayer Leverkusen, ambako alipoteza mechi moja tu msimu mzima, ilikuwa fainali ya Europa League mbele ya Atalanta.
Arteta na Alonso waliungana na Mhispaniola mwenzao, Cesc Fabregas, ambaye alikuwapo kwenye tuzo hizo baada ya kuiongoza Como 1907 kupanda daraja na kucheza Serie A msimu ujao.
Kiungo wa zamani, Fabregas, 37, aliambatana na mkewe mrembo Daniela Semaan na kupewa tuzo ya "Globe Soccer Comeback Award" kwa niaba ya klabu hiyo ya Italia.
Straika, Robert Lewandowski, ambaye aliwahi kushinda kwenye tuzo hizo za Globe Soccer Awards, alichaguliwa kwenye Kikosi cha Msimu cha La Liga.
Lewa, 35, alipigilia suti ya tuxedo, aliambatana na mkewe, mrembo Anna kwenye sherehe hizo. Supastaa, Kylian Mbappe, aliyekuwa kwenye vazi jeusi juu chini, alinyakua tuzo ya Mchezaji Bora wa Ulaya.
Kwenye tuzo hizo, Mbappe, ambaye mkataba wake Paris Saint-Germain utafika tamati mwezi ujao alifichua klabu ya Serie A ambayo atapenda kuja kuichezea siku moja.
Mbappe aliiambia Sky Sport Italia: "Kama ningekuwa nacheza Italia, ningekuwa Milan. Nilipokuwa mdogo, nilikuwa shabiki wa AC Milan na siku zote niliiangalia Serie A na mechi zote za Milan. Familia yangu yote ni Milan."
Kipa veterani, Gianluigi Buffon, 46, alinyakua tuzo ya "Player Career Award" - baada ya kutundika daruga zake msimu uliopita. Man City ilitwaa tuzo ya Klabu Bora ya Mwaka kwa upande wa wanaume, licha ya kuchapwa na Manchester United kwenye fainali ya Kombe la FA, Jumamosi iliyopita.
Barcelona, yenyewe imenyakua tuzo kama hiyo ya Man City, na pia kwa upande wa soka la wanawake baada ya timu yao kubeba ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa soka la wanawake.
Harry Kane wa Bayern Munich alishinda tuzo ya Mfungaji Bora, wakati kinda wa Barca, Lamine Yamal alinyakua tuzo ya Mchezaji Bora Anayechipukia.
Kocha mkongwe, Fabio Capello alikuwapo kwenye tuzo hizo alipoambatana na mkewe, mrembo Laura Ghisi, 55.
Capello, 77, alikwenda kwenye tuzo hizo kama mgeni rasmi kumkabidhi tuzo ya Kocha Bora wa La Liga, ambapo ilinyakuliwa na Michel Sanchez wa Girona.