Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Arsene Wenger aichambua Man Utd

Image 423.png Arsene Wenger aichambua Man Utd

Tue, 31 Oct 2023 Chanzo: Dar24

Kocha mkongwe wa soka, Mfaransa Arsene Wenger amedai kuwa, timu ya Manchester United hivi sasa imepoteza ubora wake, ari na kujiamini inapokuwa dimbani.

Wenger alitoa kauli hiyo baada ya Man United kukubali kichapo cha mabao 3-0 nyumbani dhidi ya mahasimu wao Manchester City katika mchezo wa Ligi Kuu ya England (EPL), uliopigwa juzi Jumapili (Oktoba 29).

Mchezo huo uliopigwa katika Uwanja wa Old Trafford jijini Manchester, mabao ya Man City yalifungwa na Erling Haaland aliyepachika mawili na Phil Foden.

Wenger ambaye ni kocha wa zamani wa Arsenal, amesema Man United hivi sasa imepoteza ubora, ari na uwezo wake wa kujiamini inapokuwa uwanjani.

“Naweza kusema pengo kati ya timu (hizo) mbili lilikuwa kubwa na zaidi kadri mchezo ulivyokuwa ukiendelea.

“Mwishowe, kwa klabu kubwa kama hiyo, unaionea huruma Man United kwa sababu hakuna matumaini katika timu,” Wenger amezungumza katika chombo cha habari cha belN Sports.

Kocha huyo ambaye anashikilia rekodi ya kuiongoza Arsenal kutwaa taji la EPL bila ya kupoteza mechi msimu wa 2003/04, amesema kuwa hafikirii kama Man United inaweza kuboresha kiwango msimu huu.

“Sioni mahali ambapo wanaweza kuboresha kiwango, kimsingi. Timu hii imepoteza kujiamini, ubora na hata ari katika mchezo wa juzi.

“Naweza kusema haikuwa ari nzuri ya mapambano kutoka kwa Man United,” amesema.

Amesema kocha wa Man United, Erik Ten Hag, hakuchanga vyema karata zake kwa kuendelea na mbinu za kuwataka wachezaji wake kurudisha mpira kwa kipa Andre Onana, badala ya kusogea mbele kushambulia.

“Naamini mahali ambapo Man United wanapata shinda sehemu kubwa, mwanzo wa yote ni kuhusu ubora, ubora wa mchezaji mmoja mmoja.

“Na nahisi juzi walikuwa vibaya sana katika kuanza kujenga mashambulizi kutokea nyuma.

“Walirudisha mpira mara nyingi kwa kipa pale walipokuwa na uwezekano wa kusogea mbele.

Wenger amesema kosa la pili la timu hiyo katika mchezo huo lilikuwa ni umbali kati ya Washambuliaji wao na mabeki.

Kutokana na kichapo hicho, Man United inashika nafasi ya nane katika msimamo wa ligi hiyo ikiwa na alama 15 baada ya kucheza mechi 10.

Chanzo: Dar24