Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Arsenal starboy! Namba hazidanganyi unaambiwa

Bukayo Saka Bukayo Saka

Fri, 24 Mar 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kuba sababu kibao za kuwafanya Arsenal kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu England.

Na moja ya sababu hizo nyingi ni Bukayo Saka. Mwingereza huyo ni mmoja kati ya wanasoka mahiri kabisa Ulaya kwa sasa na takwimu zake zinathibitisha wazi kwamba Saka ni starboy wa Arsenal.

Arsenal imejiweka patamu sana kwenye Ligi Kuu England, ikiongoza kwa tofauti ya pointi nane kileleni. Saka amekuwa mchezaji muhimu katika namna ambayo Arsenal inacheza soka lake na sasa akiwa amefikisha tarakimu mbili za mabao yake ya kufunga na kuasisti kwa kila upande.

Hadi sasa msimu huu, Saka ameshazidi idadi yake ya mabao aliyofunga msimu uliopita na bado kuna mambo mengi atafanya.

Umri wake ni ndio kwanza miaka 21, hivyo yajayo yanafurahisha zaidi kutoka kwa mchezaji huyo ambaye mashabiki wa Arsenal wanamwita starboy.

Saka alifunga mara mbili dhidi ya Crystal Palace kwenye mchezo wa Ligi Kuu England uliopita na Kocha Mikel Arteta alivutiwa kwelikweli na kiwango chake bora cha ndani ya uwanja.

“Nadhani timu imecheza vizuri sana na tuna vipaji binafsi ambavyo vimekuwa vikicheza kwenye ubora tunaohitaji,” alisema Arteta.

“Ukweli, Saka alikuwa vizuri, tena vizuri sana, akihusika moja kwa moja kwenye matokeo kutokana na mchango wake hasa pale alipoingia ndani ya boksi la timu pinzani. Amenifurahisha sana.

“Kiwango chake kinakua kwa sababu amezungukwa na wachezaji sahihi wanaomfanya kuwa bora na hilo ni muhimu sana. Amekuwa na mchango mkubwa kwenye timu yetu na tunataka kulilinda hilo. Amekuwa mtulivu, anafahamu kwamba anaweza kuwa bora zaidi ya anavyofanya kwa sasa kwa sababu ndio kwanza ana umri wa miaka 21.”

Kumekuwa na sifa kedekede kuhusu Saka msimu huu, lakini je, kinachosemwa kinakwenda sambamba na huduma ya mkali huyo uwanjani? Namba hazidanganyi unaambiwa.

Saka amechangia mabao 22 kwa timu yake kwenye Ligi Kuu England msimu huu, akifunga 10 na kuasisti 12. Yeye ni mmoja kati ya wanasoka watano wa kutoka Ligi Kuu tano bora za Ulaya ambao wamefanikiwa kufunga na kuasisti kwa taratimu zinazoanzia mbili kila upande ndani ya msimu huu.

Saka wa msimu huu ameingia kwenye rekodi ya kuwa mmoja wa wachezaji wanane walifanikiwa kufunga na kuasisti kwa tarakimu zinazoanzia mbili ndani ya msimu mmoja wa ligi, huku wakali wengine wa Arsenal waliofanya hivyo ni Thierry Henry, Dennis Bergkamp na Cesc Fabregas.

Akiwa na umri wa miaka 21, Saka ndiye mchezaji kijana zaidi wa Arsenal kuwa na zaidi ya mabao 10 ya kufunga na kuasisti ndani ya msimu mmoja.

Mchezaji mwingine wa Arsenal aliyewahi kufanya hivyo akiwa mdogo ni Mhispania, Cesc Fabregas - alipokuwa na umri wa miaka 22.

Erling Haaland na Harry Kane ni wachezaji pekee waliochangia mabao mengi kwenye ligi kumzidi Saka msimu huu. Lakini, wachezaji hao wawili wote ni mastraika, wakati supastaa huyo kijana wa Arsenal, yeye ni winga.

Saka amehusika kwenye asilimia 33.3% ya mabao ya Asenal yaliyofungwa kwenye Ligi Kuu England msimu huu, hivyo bila ya mabao ya mkali huyo wa Arsenal hali ya miamba hiyo ya Emirates ingekuwa mbaya na pengine isingekuwa kinara wa ligi hiyo kwa sasa.

Saka akiwa kwenye uzi wa Arsenal amepiga mashuti 124 kwenye Ligi Kuu England msimu huu, huku kukiwa na wachezaji wengine wanne tu waliofanikiwa kufanya kama hivyo kwa maana ya kupiga mashuti yanayozidi 100 kwenye ligi msimu huu.

Saka amefanya kwa mafanikio makubwa majaribio yake ya kukokota mpira, akizidi wachezaji wengine wote kwenye Ligi Kuu England, akikokota mpira mara 46, huku akifanikiwa kwa asilimia 37% katika kukokota mpira na kuwavuka wachezaji wa timu pinzani.

Mabao manne kati ya 12 yamekuwa ya ushindi kwenye mechi.

Amefunga mabao matano pia dhidi ya timu za Big Six na kuonyesha kwamba hachagui timu za kuzifunga katika kuhakikisha Arsenal inatimiza malengo yake ya kunyakua ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu.

Arsenal imeukosa ubingwa wa England kwa miaka 19.

MECHI ZA ARSENAL

-Jumamosi, Aprili 1 vs Leeds (nyumbani)

-Jumapili, Aprili 9 vs Liverpool (ugenini)

-Jumapili, Aprili 16 vs West Ham (ugenini)

-Ijumaa, Aprili 21 vs Southampton (nyumbani)

-Jumatano, Aprili 26 vs Man City (ugenini)

-Jumamosi, Aprili 29 vs Chelsea (nyumbani)

-Jumamosi, Mei 6 vs Newcastle (ugenini)

-Jumamosi, Mei 13 vs Brighton (nyumbani)

-Jumamosi, Mei 20 vs Nottm Forest (ugenini)

-Jumapili, Mei 28 vs Wolves (nyumbani

Chanzo: Mwanaspoti