Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Arsenal ipo siriazi Mbio za ubingwa EPL

Arsenal X Noyyingham Forest Arsenal ipo siriazi Mbio za ubingwa EPL

Wed, 14 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Ligi Kuu England (EPL) ni weka niweke. Mambo ni moto usipojipanga, unapangwa. Cheki kwenye msimamo wa ligi hiyo unavyosoma. Kuna tofauti ya pointi saba tu, baina ya timu ya kwanza na inayoshika nafasi ya pili.

Lakini, kinachovutia kuna tofauti ya pointi mbili baina ya vinara na timu inayoshika nafasi ya tatu. Liverpool ipo kileleni na pointi 54, ikifuatiwa na Manchester City yenye pointi 52, kisha Arsenal 52, halafu wanaokamilisha Top Four, Tottenham Hotspur wana pointi 47.

Hata hivyo, Man City ambao ni mabingwa watetezi wamecheza mechi moja pungufu, hivyo kama wataibuka na ushindi kwenye kiporo watakwea kileleni na kuweka pengo la pointi moja.

Wikiendi iliyopita, ilikuwa suala la kila mtu ashinde mechi zake. Man City ndiyo iliyoanza, ikiichapa Everton 2-0 na kupata hadi kileleni kwenye msimamo wa ligi, wakaishusha Liverpool.

Liverpool iligomea kitu hicho, kwa saa chache baadaye ilirejea kileleni baada ya ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Burnley. Spurs ilihitaji bao la dakika za majeruhi kushinda 2-1 dhidi ya Brighton na kutinga kwenye Top Four. Kazi ilikuwa kwa Arsenal, baada ya washindani wenzake kwenye mbio za ubingwa kushinda mechi zao, wao wangefanyaje? Na hakika walichofanya ni hatari.

Arsenal iliandikisha ushindi wa nne mfululizo tangu ilipopoteza kwa Fulham, baada ya kuiangushia kipigo kizito West Ham United cha mabao 6-0. Ushindi huo umerudisha matumaini kwa kocha Mikel Arteta katika harakati za kunyakua ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu.

Manchester United yenyewe pia iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 ugenini huko Villa Park, wakati ilipoichapa Aston Villa ya kocha Unai Emery. Ushindi huo, umeifanya Man United ya kocha Erik ten Hag kuamsha matumaini yao ya kucheza michuano ya Ulaya msimu ujao, kwani ipo nyuma kwa pointi sita tu kuifikia timu inayoshika nafasi ya nne, ambayo ndiyo yenye tiketi ya mwisho ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa upande wa Ligi Kuu England.

Lakini, gumzo la wikiendi hii lilikuwa la mbio za kufukuzia ubingwa wa Ligi Kuu England. Liverpool na Man City zilishinda mechi zao, hivyo shughuli ilikuwa kwa Arteta kama anaweza kujibu mapigo.

Na mbele yao walisimama wabishi West Ham na kwa ubishi wao huo, ulimfanya Arteta kuja na mkakati kabamba wa kuwabana wapinzani wao hao waaonolewa na David Moyes kuanzia mwanzo hadi mwisho. Mabeki wa kati, Gabriel na William Saliba walikuwamo kwenye orodha ya waliotikisa nyavu kwenye ushindi wa mabao 6-0 ugenini, huku Martin Odegaard na Declan Rice walikuwa mabosi kwenye safu ya kiungo.

Viungo hao wawili walichangia mabao matano kati ya hayo sita, wakifunga moja na kuasisti manne. Winga Bukayo Saka, naye alikuwa moto kwenye mechi hiyo, akifunga mara mbili kwa mkwaju wa penalti na baadaye kufuatia asisti ya Odegaard, huku staa huyo Mwingereza akihusika kwenye mabao sita katika mechi sita za mwisho, huku mwenyewe akisema: “Tulikuwa mbele 4-0 katika kipindi cha kwanza na tungeweza kufunga zaidi. Tulikuwa moto na tulitaka kuua kabisa.” Matokeo ya aina hiyo yanaongeza nguvu kwenye timu hasa mbio za kusaka ubingwa na kwa lililotokea wikiendi iliyopita, bila shaka Arsenal inaonekana kudhamiria kufanya jambo msimu huu.

Baada ya mechi hiyo iliyofanyika kwenye Uwanja wa London, hizi hapa takwimu za kibabe kabisa kuhusu Arsenal na mipango yao ya msimu huu katika kufukuzia ubingwa wa Ligi Kuu England.

Akiwa na umri wa miaka 22 na siku 159, Saka amekuwa mchezaji kijana kufikisha mabao 50 kwenye kikosi cha Arsenal tangu alipofanya hivyo Frank Stapleton mwaka 1978.

Hiyo ilikuwa mara ya kwanza Arsenal kufunga mabao manne hadi mapumziko kwenye mchezo wa ligi England, tangu ilipotoka sare ya 4-4 na Newcastle United miaka 13 iliyopita, Januari 2011.

Arsenal imefunga mabao mengi zaidi kwa mipira ya kona (11) na mipira ya kutenga (14) isiyohusisha penalti kwenye Ligi Kuu England msimu huu.

Kabla ya mechi hiyo ya jioni ya Jumapili, Arsenal ilikuwa na rekodi ya mechi nne tu ambazo ilifunga mabao sita au zaidi kwenye historia yao kwenye Ligi Kuu England.

Huu ni ushindi mkubwa zaidi wa Arsenal kwenye mechi zake dhidi ya West Ham tangu mwaka 1960. Katika msimu wa 1960-61, The Gunners ilipata pia ushindi wa mabao 6-0 dhidi ya mahasimu hao wa London.

Hii ni mara ya kwanza kwa Arsenal kufunga mabao sita ugenini kwenye mchezo wa ligi tangu walipomchapa pia David Moyes wakati huo alipokuwa Everton, mabao 6-1, Agosti 2009.

Odegaard alikosea pasi sita tu kati ya 113 alizopiga kwenye mchezo huo. Nahodha huyo wa Arsenal alitengeneza pia nafasi saba za mashambuliaji na kuasisti mara mbili katika mechi hiyo ya kibabe.

Huu ni ushindi mkubwa zaidi wa Arsenal kwenye Ligi Kuu England kwa mechi za ugenini. Kabla ya mechi hiyo ya juzi Jumapili, ushindi wao mwingine uliokuwa mkubwa kwa mechi za ugenini, ni ule wa mabao 6-1 dhidi ya Everton mwaka 2009 na waina hiyo dhidi ya Middlesbrough mwaka 1999.

Arsenal ilipiga mashuti 25 huku 12 yakilenga goli. Jambo hilo liliifanya Arsenal kuweka rekodi tamu ya kuwa na wastani wa kupiga mashuti 16.5 kwa kila mechi kwenye Ligi Kuu England msimu huu.

Chanzo: Mwanaspoti