Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Arsenal hakuna wa kuwazuia, ubingwa EPL wanukia

Arsenal February 2023 1 Arsenal hakuna wa kuwazuia, ubingwa EPL wanukia

Mon, 20 Mar 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Ni miaka 19 sasa Arsenal inahaha kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England, lakini sasa ni wazi hakuna wa kuwazuia kwenye mbio hizo za kuwania taji hilo kubwa nchini humu.

Ni vichapo tu inatembeza sasa na kuukaribia ubingwa huo ambao unasubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa timu hiyo duniani kote baada ya ushindi mnono jana jioni wa mabao 4-1 dhidi ya Crystal Palace kwenye mwendelezo wa Ligi Kuu England.

Kutokana na matokeo hayo, Arsenal sasa imefikisha pointi 69, ikiwa ni tofauti ya pointi nane dhidi ya wapinzani wao wa karibu Manchester City ambao wanasaliwa na mchezo mmoja mkononi baada ya juzi kucheza mchezo wa robo fainali ya FA dhidi ya Burnley.

Katika mchezo huo wa EP, kwenye Uwanja wa Emirates, Arsenal ilijipatia mabao mawili kipindi cha kwanza na Gabriel Martinelli alianza kufunga dakika ya 28 akipokea asisti kutoka kwa Bukayo Saka, kabla ya Saka huyo huyo kufunga la pili dakika ya 43 kwa asisti ya Ben White.

Bao na asisti aliyotoa Saka ilimwezesha kuandika rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza wa Arsenal baada ya Alexis Sanchez kufunga mabao 10 na asisti 10 au zaidi kwenye msimu mmoja wa Ligi Kuu England, Sanchez alifanya hivyo msimu wa 2016-17. Arsenal ilirudi na moto ule ule wa kipindi cha kwanza na katika dakika ya 55, Granit Xhaka alifunga bao la tatu kwa asisti ya Leandro Trossard na dakika ya 74 Saka akaifungia Arsenal bao la nne na kuzidi kulizamisha jahazi la Palace.

Baada ya ushindi huo Arsenal sasa itakuwa na kibarua mbele ya Leeds United kabla ya kukutana na Liverpool ugenini Aprili 09. Arsenal itakuwa inaiombea mabaya Man City ipoteze mchezo wao dhidi ya Liverpool unaotarajiwa kupigwa Aprili 01, ili pengo la alama liendelee kubakia nane na kuwapunguzia presha tofauti na ilivyo hivi sasa.

Palace inaendeleza wimbi la matokeo mabovu tangu mwaka huu uanze na haijapata ushindi wowote katika mechi 13 ilizocheza na imetoka sare nne na kufungwa mara tisa.

Matokeo yao mabaya yalisababisha imfukuze kocha wao Patrick Vieira wiki hii na baada ya kufungwa na Arsenal imeendelea kusalia kwenye 12, ikiwa na pointi 27 baada ya kucheza mechi 28 ikiwa imeshinda sita, sare tisa na kufungwa 13.

Palace kwa sasa inapambana kuhakikisha inafikisha Pointi 40 ili kuwa na uhakika wa asilimia nyingi za kubakia kwenye ligi kwa msimu ujao kwa sababu alama zake za sasa zinaweza kufikiwa kirahisi na timu za chini ikiwa itaendelea kupoteza kwenye mechi moja au mbili zijazo.

Takwimu zinaonyesha msimu huu Saka ndio amekuwa na kiwango bora zaidi tangu ajiunge na Arsenal akiwa amefunga jumla ya mabao 13 ya michuano yote huku 12 yakiwa ni yale ya Ligi Kuu England, hakuwahi kuwa na idadi hii ya mabao katika msimu mmoja hapo nyuma.

Wakati huo huo, kwenye michuano ya FA, Sheffield United ilitinga nusu fainali baada ya kuifunga Blackburn Rovers mabao 3-2 huku Brighton yenyewe ikitembeza kichapo cha mabao 4-0 kabla ya mchezo wa usiku ambao Manchester United ilicheza na Fulham zikisaka ushindi kuungana na miamba hiyo pamoja na Man City.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: