Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Arsenal, Man United ni vita nikuvute

IMG 5946 United UEFA.jpeg Arsenal, Man United ni vita nikuvute

Tue, 7 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mchakamchaka wa Ligi ya Mabingwa Ulaya unarudi tena wikiendi hii, huku Manchester United na Arsenal zitatambua hatima yao ya kupenya ama kutopenya kwenye raundi inayofuata kwa mechi zao kali kesho Jumatano.

Man United itakuwa ugenini kukipiga na FC Copenhagen, wakati Arsenal itakuwa nyumbani kumaliza ubishi na Sevilla.

Man United itahitaji kushinda mechi hiyo ya ugenini ili kufikisha pointi sita kwenye Kundi A baada ya mechi nne, wakati Arsenal itakuwa Emirates kusaka ushindi kwenye Kundi B ili ifikishe pointi tisa, ambazo zitakuwa zimeiweka kwenye mazingira mazuri ya kutinga hatua ya mtoano.

Mambo yalivyo kwenye michuano hiyo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, ni timu nne pekee ambazo zimeshinda mechi zote tatu za hatua ya makundi hadi sasa, huku Bayern, Barcelona, ​​Manchester City na Real Madrid zikijivunia rekodi nzuri.

Timu hizi za hatari bila shaka ni miongoni mwa timu zinazopigiwa upatu kushinda mashindano haya, na zitapiga hatua kukaribia fainali ya itakayofanyika Wembley mwakani ikiwa itapata ushindi katika mechi ya nne na kutinga hatua ya 16 bora.

Miamba hiyo hakika inaendelea kuthibitisha kuwa wao ni bora zaidi kwenye hatua kubwa zaidi kwenye mbio za kuwania ubingwa wa Ligi Mabingwa Ulaya kama Kocha wa Barcelona Xavi alivyosema baada ya ushindi wa mechi tatu nyumbani dhidi ya Shakhtar Donetsk: “Pointi tisa kati ya tisa ni nzuri sana. Bado hatufuzu lakini ilikuwa hatua muhimu sana kwa upande wetu. Tunajisikia vizuri sana kuhusu hili.”

Kundi F halina mwenyewe

Liliangaziwa kama moja kundi lenye ushindani mkali katika miaka ya hivi karibuni wakati droo ilipofanyika. Paris Saint- Germain, Dortmund, Newcastle na AC Milan tayari zimeonyesha mechi za kuburudisha sana, na kati ya timu hizo, mbili zinaweza kufuzu kwani ponti nne ndio zimewatenganisha viongozi wa kundi kati ya Milan na PSG.

“Mechi za makundi ni ngumu,” Kocha wa Newcastle Eddie Howe alisema baada ya mechi iliyopita ambayo ilifunga bao 1-0 nyumbani dhidi ya Dortmund.

“Ilikuwa pigo kwetu, hasa nyumbani. Sasa tuna mechi mbili muhimu za ugenini. Haiwezekani kutabiri mambo yatakavyokuwa, lakini picha inaweza kuonekana zaidi baada ya mechi inayofuata,”

Højlund anarejea nyumbani Denmark

Baada ya kucheza dhidi ya timu yake ya zamani Copenhagen Uwanja wa Old Trafford, fowadi huyo wa Manchester United, atarejea nyumbani alipozaliwa. Mashetani Wekundu waliibuka na ushindi wa bao 1-0 Old Trafford ambalo limewekwa kimiani na Harry Maguire.

Sasa vijana wa Kocha Erik ten Hag watasafiri kuelekea Denmark kwa ajili ya mchezo wa marudiano na muhimu kwao Kundi A. Højlund alipitia katika kituo cha kukuza vipaji Copenhagen na kutoboa kwenye soka la ushindani.

Wakati anakipiga Copenhagen ya wakubwa alifunga mabao matano kwenye michuano ya UEFA Europa Conference League msimu wa 2021/22 kabla ya kuhamia Sturm Graz.

Højlund alinyimwa nafasi ya kucheza dhidi ya kaka yake Oscar Hojlund Old Trafford kwani alifanyiwa mabadiliko dakika tano kabla ya mchezo kumalizika dhidi ya Copenhagen.

Wanaweza kupata fursa nyingine ya kumenyana huko Denmark, lakini hakutakuwa na muda wa kuoneana huruma, huku pande zote mbili zikihitaji sana ushindi zikiwasaka viongozi wa kundi Bayern Munich na Galatasaray.

Dondoo tamu

•Fowadi wa Bayern Munich Thomas Muller anaweza kuweka rekodi ya kucheza mechi 150 za Ligi Mabingwa Ulaya endapo atapewa nafasi dhidi ya Galatasaray. Kiungo wa Real Madrid, Luka Modric na beki wa Sevilla, Sergio Ramos waliweka rekodi ya kucheza mechi nyingi za UEFA mechi zilizopita.

• Beki mkongwe wa Porto, atapata nafasi nyingine ya kurejea Barcelona watakapomenyana dhidi ya mimba hiyo ya Catalunya Novemba 28. Beki huyo wa zamani wa Real Madrid amecheza jumla ya El Clasico 11 akiwa na rekodi ya ushindi mara nne, sare mbili, na kufungwa mara tano.

• Man United itacheza mechi ya marudiano dhidi Galatasaray kwenye Uwanja wa Ali Sami Yen Spor Kompleksi Novemba 29. Kwenye mechi tatu za Ligi Mabingwa Ulaya dhidi ya Galatasaray haijapata ushindi na mara ya mwisho ilichezea kichapo cha bao 1-0 mwaka 2012.

MECHI ZENYEWE LEO JUMANNE

Dortmund vs Newcastle (saa 2:45 usiku). Shakhtar Donetsk vs Barcelona (saa 2:45 usiku). Atlético de Madrid vs Celtic (saa 5:00 usiku). Lazio vs Feyenoord (saa 5:00 usiku). Milan vs Paris (saa 5:00 usiku).Man City vs Young Boys (saa 5:00 usiku). Crvena zvezda vs Leipzig (saa 5:00 usiku).Porto vs Antwerp (saa 5:00 usiku).

KESHO, JUMATANO

Napoli vs Union Berlin (saa 2:45 usiku) Real Sociedad vs Benfica (saa 2:45 usiku). Bayern vs Galatasaray (saa 5:00 usiku). Copenhagen vs Man United (saa 5:00 usiku). Arsenal vs Sevilla (saa 5:00 usiku). PSV Eindhoven vs Lens (saa 5:00 usiku) Real Madrid vs Braga (saa 5:00 usiku) Salzburg vs Inter (saa 5:00 usiku).

Chanzo: www.tanzaniaweb.live