Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Arsenal, Liverpool FC, Man City zitakavyouana kwenye ubingwa EPL

Pep X Klopp Arsenal, Liverpool FC, Man City zitakavyouana kwenye ubingwa EPL

Tue, 12 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Pale juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu England, timu ya kwanza hadi ya tatu, zimetofautiana pointi moja tu na mechi zenyewe zimebaki 10 kumpata bingwa wa msimu huu wa 2023/2024.

Vita ya kusaka ubingwa ni kali kati ya Arsenal, Liverpool na Manchester City zikiwa zimejipanga kwa mpangilio huo kutoka nafasi ya kwanza hadi ya tatu. Mwali atakwenda wapi? Emirates, Anfield au Etihad? Mchawi ni mechi 10 ambazo zimebaki kwa kila timu.

Mwanaspoti linakuletea uhondo wa vita hiyo ulivyo kwa ratiba ya kila timu, ipi imebakiza mechi ngumu nyingi na ipi ina afadhali.

ARSENAL – POINTI 64

Arsenal ndiyo timu ambayo ipo kwenye viwango bora zaidi kwa sasa kuliko wapinzani wake hao watatu, ambapo imeshinda mechi nane mfululizo ilizocheza tangu mwaka huu 2024 ulipoanza, huku ushindi huo ukijumuisha ule wa mabao 3-1 iliyopata dhidi ya Liverpool, Januari.

Katika mechi hizo nane, kikosi hicho cha kocha Mikel Arteta kimefunga mabao 33 na hivyo kuweka uwiano mzuri kwenye tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa na hicho ndicho kitu kinachowafanya waongoze kwenye msimamo wa ligi hiyo kwa sasa.

Kwa sasa, Arsenal haitakuwa na mechi tena ya ligi hadi hapo Machi 31, itakapomenyana na Man City na katika kipindi cha miezi 12 iliyopita, kikosi hicho cha Emirates kimeonyesha mabadiliko makubwa sana.

Kikosi hicho chaArsenal kilichapwa mabao 4-1 huko Etihad msimu uliopita kwenye mechi kama hiyo na kuondoka kwenye mbio za ubingwa. Mwaka huu itakuwaje?

Lakini, mwaka huo mmoja, Arsenal imefanya mabadiliko makubwa kwenye kikosi chake kwa kuleta mastaa makini kama Declan Rice na Kai Havertz, ambao wamekuja kuleta ubora mkubwa kwenye timu. Ukiweka kando mechi ya Man City, Arsenal pia itakuwa na kibarua kigumu cha kuwakabili mahasimu wao wa London, Tottenham na bado haijacheza pia na Manchester United, Brighton na Wolves ugenini.

RATIBA YAO ILIVYO:

Machi 31: Man City (ugenini)

Aprili 3: Luton (nyumbani)

Aprili 6: Brighton (ugenini)

Aprili 13: Aston Villa (nyumbani)

Aprili 20: Wolves (ugenini)

Aprili 27: Tottenham (ugenini)

Mei 4: Bournemouth (nyumbani)

Mei 11: Man United (ugenini)

Mei 19: Everton (nyumbani)

*Chelsea (nyumbani, itapangiwa)

LIVERPOOL – POINTI 64

Vijana wa Jurgen Klopp, Liverpool walishindwa kutumia vyema kipindi cha pili wakati walipowashika vilivyo Man City kwenye mchezo wa Ligi Kuu England uliomalizika kwa sare ya bao 1-1 uwanjani Anfield, juzi Jumapili. Hata hivyo, kikosi hicho kwenye karatasi kinaonekana kuwa na ratiba nyepesi kutokana na soka lao wanalocheza na hivyo kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kutabiriwa kubeba ubingwa.

Kocha Klopp ameiweka Liverpool kwenye ubora mkubwa unaoweza kuwafanya kushinda mataji manne msimu huu licha ya kikosi chake kuandamwa na majeruhi wengi kuliko timu nyingine kinazoshindana nazo kwenye mbio za ubingwa wa ligi hiyo.

Alisson Becker, Trent Alexander-Arnold na Diogo Jota bado wapo nje ya uwanja kwa kuwa majeruhi, lakini kocha Klopp amewaweka kwenye ubora wachezaji wengine ambao wanaifanya Liverpool kuwa matata uwanjani. Mohamed Salah alitokea benchi kwenye mechi mbili zilizopita, wakati Dominik Szoboszlai na Darwin Nunez walipata nafasi ya kuanza kwenye kipute hicho cha Man City.

Kingine, Liverpool itakuwa na nguvu ya ziada kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England kutokana na kukabiliwa na mechi zisizokuwa tishio sana kwao kwenye Europa League na Kombe la FA Cup. Watasafiri kuifuata Man Unitd wikiendi ijayo kwenye robo fainali ya Kombe la FA na itakuwa mechi nyingine ya ligi kwenye uwanja huo wa Old Trafford mwezi ujao.

Ratiba nyingine yenye utata inayowakabili ni ile ya kukabiliana na mahasimu wao Everton na timu zinazofukuzia nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya, Tottenham na Aston Villa kwenye mechi zao mbili kati ya tatu za mwisho katika msimu huu.

RATIBA YAO ILIVYO:

Machi 31: Brighton (nyumbani)

Aprili 4: Sheffield United (nyumbani)

Aprili 7: Man United (ugenini)

Aprili 14: Crystal Palace (nyumbani)

Aprili 20: Fulham (ugenini)

Aprili 27: West Ham (ugenini)

Mei 4: Tottenham (nyumbani)

Mei 11: Aston Villa (ugenini)

Mei 19: Wolves (nyumbani)

* Everton (ugenini, itapangiwa)

MAN CITY – POINTI 63

Man City imelenga kuandika rekodi ya kuwa timu ya kwanza kushinda mara nne mfululizo ubingwa wa Ligi Kuu England, lakini kwa msimu huu itabidi ipambane sana kufanya hilo kutokana na wapinzani wao, Arsenal na Liverpool kuwa makini na bora uwanjani.

Pep Guardiola amekiri kwamba kikosi chake kimenusurika kwenye tsunami katika mchezo wao dhidi ya Liverpool, lakini kubwa ni pointi moja waliyoondoka nayo huko Anfield inazidi kuweka hai matumaini yao kwenye kutetea taji la ubingwa wa Ligi Kuu England, kwa sababu tofauti yao na vinara wa ligi hiyo, Arsenal ni pointi moja tu.

Kingine kinachowapa matumaini Man City ni kwamba mchezo wao ujao watakipiga na Arsenal uwanjani Etihad, wanafahamu ushindi kwenye mechi utawaweka pazuri kwenye mbio za ubingwa, kwani siku nne baadaye, watakuwa na mechi nyingine ngumu dhidi ya Aston Villa.

Kwa mwezi ujao, watakuwa na mengi nyingine ngumu ikiwamo ya kuwakabili Tottenham, ambao mara nyingi wamekuwa wakiwasumbua wanapokutana kwenye mikikimikikiki ya Ligi Kuu England.

RATIBA YAO ILIVYO:

Machi 31: Arsenal (nyumbani)

Aprili 3: Aston Villa (nyumbani)

Aprili 6: Crystal Palace (ugenini)

Aprili 13: Luton (nyumbani)

Aprili 20: Tottenham (ugenini)

Aprili 27: Nott’m Forest (ugenini)

Mei 4: Wolves (nyumbani)

Mei 11: Fulham (ugenini)

Mei 19: West Ham (nyumbani)

* Brighton (ugenini, itapangwa)

Chanzo: Mwanaspoti