Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Arne Slot azuia kuondoka kwa Mohamed Salah

Salah Mo 120 Mohammed Salah

Mon, 15 Jul 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kocha wa Liverpool, Arne Slot amesema bado anahitaji huduma ya mshambuliaji wa timu hiyo Mohamed Salah akimtaja kama sehemu muhimu ya mipango yake kwa msimu ujao.

Salah ambaye amerejea mazoezini wiki iliyopita, amekuwa akihusishwa kuwa katika harakati za kutaka kuondoka Liverpool katika dirisha hili na kutua Al Ittihad ya Saudi Arabia ambako amewekewa ofa nono.

Hadi sasa staa huyu wa kimataifa kutoka Misri amecheza Liverpool kwa misimu saba na tetesi za kuondoka kwake zilizidi kupamba moto baada ya Jurgen Klopp kutangaza kuachana na majogoo hao.

Ilielezwa, kuondoka kwa Klopp ambaye ndiye aliyemsajili staa huyu inaweza kusababisha Salah naye akaondoka kwani moja ya vitu vilivyokuwa vinamzuia asiondoke ni heshima yake kwa Klopp.

Hata hivyo, Slot hajaonyesha nia ya kutaka kumruhusu Salah kuondoka katika dirisha hili akidai ni mmoja kati ya wachezaji anaowategemea na angependa aendelee kubakia katika timu kwani ni mfano mzuri kwa wachezaji wengine.

"Mo alirejea akiwa na nguvu, alikuwa fiti sana kama ilivyo siku zote na hiki ndicho ninachohitaji kutoka kwake na wachezaji wengine, nikimwangalia pia nahitaji awe mfano kwa wachezaji wengine katika kikosi cha kwanza na wale wanaochipukia. "

Slot anaamini uzoefu ambao Salaha ameupata katika kipindi chote alichodumu Liverpool hadi sasa utamsaidia yeye katika kuisogeza timu hiyo kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu England na michuano ya kimataifa.

Waarabu waliweka ofa ya zaidi ya Pauni 100 milioni katika dirisha la majira ya kiangazi mwaka jana ili kumsajili Salah ambaye mkataba wake unamalizika mwaka 2025.

Liverpool imekuwa katika mazungumzo na Salah kwa ajili ya kumshawishi aongeze mkataba mpya kwani akiendelea kuwepo katika kikosi chao hadi msimu ujao utakapomalizika na mkataba huu huu itaenda kumpoteza bila ya kupata chochote jambo ambalo majogoo hao hawalitaki.

Chanzo: Mwanaspoti