Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Arne Slot awajibu mashabiki Liverpool

Arne Slot Dsc Kocha mpya wa Liverpool, Arne Slot

Sat, 27 Jul 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Wakati mashabiki wa Liverpool wakilalamika kwamba timu yao haifanyi usajili wa kuboresha baadhi ya maeneo ambayo yalionekana kuwa na mapungufu, kocha wa timu hiyo, Arne Slot amesisitiza kwamba kipaumbele chake kwa sasa ni kutengeneza timu bora kupitia wachezaji alionao ndani ya timu na baadae kama akipata mastaa anaowahitaji itakuwa ni ziada tu.

Kocha huyu raia wa Uholanzi alianza kazi rasmi akichukua mikoba ya Jurgen Klopp, Juni Mosi akishirikiana na Mkurugenzi mpya wa michezo Richard Hughes.

Hadi sasa hakuna hata mchezaji mmoja ambaye wawili hao wamefanikisha kumsajili huku maswali yakibakia kwa mashabiki ambao wanatamani kuona mastaa wapya wakisajiliwa wakati wapinzani wao wakiwa wanasajili.

Licha ya kusema kipaumbele chake ni kuboresha na kutengeneza timu kupitia wachezaji alionao kwa sasa, Slot amekiri kwamba wanatakiwa kuboresha timu yao na ametoa sababu ya kuchelewa kusajili ni yeye kutaka kujiridhisha kutazama wale ambao yupo nao kuna nini wamekosa ili asajili mchezaji atakayeongeza kitu na hilo linakuwa jambo gumu kwa sababu mastaa wengi hawapo katika kikosi kwa sasa.

"Lengo la kwanza ni kufanya kazi na hawa wachezaji waliopo, ingawa pia kuna hasara kwa sababu wachezaji wengi hawapo katika kikosi kutokana na mapumziko waliyopewa baada ya kucheza michuano ya Euro 2024 na Copa America, lakini hii pia inanipa muda wa kutazama wachezaji vijana na kuwapa nafasi kubwa ya kucheza, "alisema Slot na kuongeza,

"Tunahitaji kusajili wachezaji bora sana kwa sababu tuna wachezaji wazuri. Ni kweli mimi na Richard tunahitaji kuboresha kikosi lakini haiwezi kuwa rahisi kutokana na wachezaji tunaowahitaji."

"Moja kati ya sababu zinazochangia usajili kutofanyika kwa haraka ni mimi kutaka kufanya mapitio kwanza kwa wachezaji waliopo lakini changamoto ni kwamba hawapo hapa, nimechukua timu hii kwa ikiwa bora sana ni ngumu kusajili tu wachezaji kirahisi ama kupata watakaokuwa na uwezo sawa na hawa ambao au zaidi ya hapo, na pia hata tukiwaona huwa ni ngumu kuwasajili."

Slot aliendelea kusema kwamba yeye na Mkurugenzi wake wa ufundi wanafanya kazi kuhakikisha wanasajili maboresho katika kikosi chao na kama kutakuwa na mabadiliko watatoa taarifa.

"Tayari tuna timu nzuri ambayo binafsi inanifurahisha nikiitazama lakini najua wote tutakuwa tumeshangazwa ikiwa dirisha litafungwa bila ya kusajili mchezaji hata mmoja, haya yanaweza kutokea lakini mwishoni kwa sasa tunasubiri wachezaji wetu muhimu warudi kikosini halafu tutaona ni eneo gani sahihi kusajili."

Liverpool ambayo kwa sasa imeweka kambi huko Marekani kwa ajili ya maandalizi ya msimu, inawakosa mastaa wake Alisson Becker, Trent Alexander-Arnold, Joe Gomez, Virgil van Dijk, Cody Gakpo, Alexis Mac Allister, Darwin Nunez na Luis Diaz ambao hawatoshiriki maandalizi hayo kutokana na mapumziko waliyopewa baada ya kuyatumikia mataifa yao katika michuano ya Cop America na Euro.

Wiki hii imewapokea Diogo Jota, Ibrahima Konate na Ryan Gravenberch waliowasili ambao wanaweza kucheza dhidi ya Arsenal huko Philadelphia Agosti 01.

Majogoo hawa wa Jiji la Liverpool wanatarajiwa kuanza kampeni za msimu ujao Agosti 10, katika mchezo dhidi ya Ipswich Town.

Chanzo: Mwanaspoti