Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Argentina yatwaa Kombe la Dunia 2022, Messi ang'ara

Messi Argentina Wc.jpeg Argentina yatwaa Kombe la Dunia 2022, Messi ang'ara

Mon, 19 Dec 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Doha, Qatar. Jamani nyie! Hatimaye Lionel Messi kalibeba Kombe la Dunia baada ya miaka zaidi ya 15 ya kulisaka kwa jasho na damu wakati siku haikuisha vyema kwa Ufaransa na staa wao Kylian Mbappe, ambaye alifunga 'hat-trick' katika mechi ya fainali iliyoamuliwa kwa matuta baada ya dakika 120 kumalizika kwa sare ya 3-3.

Messi amemaliza michuano hiyo kishujaa nchini Qatar akiiongoza Argentina kutwaa taji lao la kwanza tangu mwaka 1986, wakati Diego Maradona alipoliwezesha taifa hilo kubeba taji lao la pili na sasa Waargentina wameshinda taji hilo mara tatu tangu michuano hiyo ilipoanzishwa mwaka 1930.

Mbappe hakutoka mikono mitupu akishinda tuzo ya mfungaji bora wa fainali hizo za 2022, baada ya kufunga mabao manane, kipa wa Argentina Emiliano Martinez alishinda tuzo ya Golden Gloves ya kipa bora, Enzo wa Fernandes alishinda tuzo ya Chipukizi Bora, huku Messi akishinda tuzo kubwa Mchezaji Bora wa fainali hizo, akipata tuzo hiyo kwa mara ya pili baada ya kuitwaa pia mwaka 2014 katika michuano ambayo walifungwa 1-0 katika fainali na Ujerumani.

Hii inakuwa ni fainali ya nne kwenye fainali tano za mwisho za Kombe la Dunia kuchezwa kwa dakika 120, fainali nyingine zilizofika hadi dakika hizo 30 za nyongeza ni zile za 2006, 2010 na 2014.

Unaweza kusema ilikuwa ni shoo ya Mbappe na Messi kwani mastaa hao ndio ambao waliweka rekodi nyingi sambamba na kuhusika kwenye mchezo mzima kuanzia dakika ya kwanza hadi ya mwisho.

Messi ndio alianza kufungua akaunti ya mabao kwa Argentina baada ya kupiga penalti hiyo katika dakika ya 23 na kuipatia Argentina uongozi wa bao la kwanza, ikawachukua dakika 13 tu Argentina kabla ya kupachika bao la pili kupitia Di Maria dakika ya 36.

Mbappe yeye alifunga mabao yote ya kusawazisha kwa upande wa Ufaransa akianzia lile la penalti dakika ya 80, kabla ya kufunga la pili kwa shuti kali dakika ya 81.

Baada ya kuongezwa kwa dakika 30 za ziada, Messi aliipatia Argentina bao la tatu katika dakika ya 108, kabla ya Mbappe kuisawazishia Ufaransa dakika ya 118 na kuweka rekodi ya kuwa staa wa pili kufunga hat-trick katika mechi ya fainali baada ya Geoff Hurst aliyefanya hivyo kwenye michuano ya mwaka 1966 kati ya England na Ujerumani, akiifungia England.

Pia Mbappe aliweka rekodi ya kuwa mchezaji aliyefunga mabao mengi zaidi katika mechi ya fainali ya Kombe la Dunia hadi sasa akitupia manne.

Lionel Messi ameweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kufunga katika hatua zote kwenye shindano moja la Kombe la Dunia akifanua hivyo mwaka huu ambapo amefunga kwenye hatua ya makundi, 16 bora, robo fainali, nusu fainali na fainali.

Mbappe ameweka rekodi ya kuwa mchezaji pekee aliyefunga mabao mawili kwenye Kombe la Dunia kwa muda mfupi sana akifanya hivyo kwa tofauti ya sekunde 97 kutoka bao la kwanza.

Messi pia ameweka rekodi ya kuwa mchezaji aliyehusika kwenye mabao mengi zaidi katika historia ya Kombe la Dunia (21) akiwa amefunga mabao 13 na kutoa asisti nane.

Mbappe pia ndio amemaliza michuano hii akiwa mfungaji bora baada ya kufunga mabao manane akifuatiwa na Messi aliyefunga mabao saba.

Hii inakuwa ni mara ya mwisho Lionel Messi kuonekana kwenye michuano ya Kombe la Dunia kwani kabla ya kuwasili nchini Qatar alishaeleza kwamba atastaafu kucheza timu ya taifa baada ya michuano hii.

Hili linakuwa ni kombe la tatu kwa Argentina, ikiwa ni kwa mara ya kwanza kuchukua taji hilo tangu mwaka 1986 ambapo ilicheza fainali dhidi ya Ujerumani ya Magharibi ambapo iliifunga mabao 3-2 kule nchini Mexico.

Ufaransa pia ilikuwa inaangalia uwezekano wa kuchukua taji hili kwa mara ya tatu na kulitetea kwa mara nyingine baada ya kulichukua mwaka 2018, ikiwa ni kwa mara ya kwanza tangu ilipolichukua mwaka 1998 kwenye michuano ambayo wao ndio walikuwa wenyeji.

Hii ilikuwa ni fainali ya sita kwa Argentina, kati ya mara hizo sita, wanakuwa wameshinda mara tatu.

Mara ya mwisho Argentina kucheza fainali ilikuwa kwenye michuano ya mwaka 2014 kule nchini Brazil ambako ilikutana na Ujerumani na kupoteza kwa bao la jioni la Mario Gotze kwenye dakika 30 za ziada.

Historia inaonyesha kuwa wababe hawa wamekutana kwa mara ya 13 kwenye michuano yote, mara nne kati ya hizo ikiwa ni kwenye Kombe la Dunia, Argentina ina rekodi ya kushinda mechi tatu na kupoteza moja.

Mara ya kwanza kukutana kwenye historia yao ilikuwa ni mwaka 1930, katika michuano ya kwanza ya Kombe la Dunia ikiwa kwenye hatua ya  makundi ambapo Argentina ilishinda bao 1-0.

Mara ya pili kukutana kwenye Kombe la Dunia ilikuwa mwaka 1978 ambapo Argentina ilishinda mabao 2-1, pia ilikuwa ni katika hatua ya makundi.

Mara ya mwisho kabla ya jana ilikuwa ni kule Urusi ambapo Argentina ilikubali kichapo cha mabao 4-3 katika hatua ya 16 bora.

Kwenye kipindi cha kwanza Ufaransa ilishindwa kabisa kupiga shuti lililoingia kwenye boksi la Argentina ama kucheza mpira ndani ya boksi la wababe hao.

ZAWADI Kwa kuchukua ubingwa Argentina imezawadiwa Dola 42 milioni ambayo ni sawa na bilioni 97 kwa pesa ya Bongo, Ufaransa yenyewe imezawadiwa Dola 30 milioni (Sh69 bilioni), Croatia ambaye ni mshindi wa tatu alipata Dola 27 milioni (Sh62 bilioni), mshindi wa nne Morocco, walipata Dola 25 milioni (Sh58 bilioni), timu zilizoishia hatua ya robo fainali zilipata Dola 17 milioni (Sh39 bilioni), hatua ya 16 bora Dola 13 milioni (Sh30 bilioni) na zile zilizokwama hatua ya makundi zilipata Dola 9 milioni(Sh20 bilioni).

Chanzo: www.tanzaniaweb.live