Klabu ya Geita Gold iko kwenye mazungumzo ya kumuongezea mkataba mpya kipa wa timu hiyo Mrundi, Arakaza MacArthur baada tu ya msimu kuisha kutokana na kuridhishwa na kiwango chake kikosini.
Mwenyekiti wa timu hiyo, Leonard Bugomola aliliambia Mwanaspoti, mazungumzo baina yao na nyota huyo yanaendelea na kama watafikia makubaliano mazuri watamuongezea kandarasi mpya.
"Tuko kwenye michezo ya mwisho ya msimu lakini tunaendelea kufanyia tathimini ya timu kwa msimu ujao na kabla ya usajili wa nyota wapya tunaanza kwanza kuboresha mikataba ya waliopo," alisema.
Akizungumzia juu ya hatma yake ndani ya timu hiyo, Arakaza alisema kwa sasa akili zake ni kumaliza kwanza msimu huu na baada ya hapo ndipo atajua kama ataendelea kubaki au lah.
"Siwezi kusema kama nitaondoka au nitabaki kwa sababu hakuna anayejua kesho yetu ila napenda soka la Tanzania kwa Ukanda huu wa Afrika Mashariki kwani huvutiwa zaidi na ushindani uliopo."
Arakaza alijiunga na timu hiyo Julai mwaka jana akitokea Lusaka Dynamos ya nchini Zambia akiwahi pia kucheza Sports Club Villa ya Uganda, FC Dikhil ya Djibouti na Kakamega Homeboyz FC ya Kenya.
Timu nyingine alizozichezea nyota huyo ni Vital'O FC na Flambeau du Centre ambazo zote zinatoka Burundi.