Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Antonio Conte atua Napoli na jina la Romalu Lukaku

Contee Pic Antonio Conte atua Napoli na jina la Romalu Lukaku

Wed, 5 Jun 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Antonio Conte anayetarajiwa kutangazwa kuwa kocha mpya wa Napoli siku chache zijazo, amependekeza jina la straika wa Chelsea na timu ya taifa ya Ubelgiji, Romelu Lukaku ili asajiliwe katika dirisha hili la majira ya kiangazi ili kuboresha eneo lao la ushambuliaji.

Conte anamfahamu vizuri Lukaku kwa sababu aliwahi kuchukua naye ubingwa mwaka 2021 akiwa na Inter Milan na staa huyu alionyesha kiwango bora sana.

Lukaku ambaye msimu huu amecheza mechi 47 za michuano yote na kufunga mabao 21, mwaka huo 2020/21 alicheza mechi 44, akafunga mabao 30 na kutoa asisti 10.

Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2026, lakini Chelsea ipo tayari kumuuza ikiwa itapata ofa sahihi kwani benchi la ufundi halijaonyesha kumwitaji aendelee kuwepo.

Lukaku pia ametajwa kuwa katika orodha ya mastaa ambao matajiri wa Saudi Arabia wanataka kuwasajili katika dirisha hili.

Lukaku amekuwa mmoja wa washambuliaji bora duniani miaka ya karibuni na ameshapita kwenye timu nyingine kubwa ikiwamo Manchester United na Kocha Conte anaamini uwepo wa nyota huyo msimu ujao Napoli utaisaidia kurejesha taji lao walilolipoteza mwisho wa msimu uliomalizika.

LIVERPOOL huenda ikaanza mazungumzo na Newcastle United kwa ajili ya kuipata saini ya kiungo wa timi hiyo na timu ya taifa ya Brazil, Bruno Guimaraes katika dirisha hili majira ya kiangazi kwa sababu kocha mpya Arne Slot amependekeza kusajili kwa kiungo mwingine atakayekwenda kuchukua nafasi ya Wataru Endo ambaye hajaridhishwa na kiwango chake. Liverpool ina kazi kubwa ya kuishawishi Newcastlel.

BORUSSIA Dortmund huenda ikaangukia pua kwenye mchakato wao wa kutaka kumsainisha mkataba wa kudumu beki wa Chelsea anayecheza kwa mkopo kwenye timu yao Ian Maatsen. Uwezekano wa kufeli kwenye dili hilo unatokana na kipengele kilichopo katika mkataba wa Ian ambacho kinaeleza timu yoyote inaweza kumnunua kwa Pauni 35 milioni katika dirisha hili licha ya kuwa amecheza kwa mkopo Dortmund.

WINGA wa Manchester United, Jadon Sancho amepanga kufanya kila linalowezekana kuhakikisha anasaini mkataba wa kudumu wa kuendelea kusalia Borussia Dortmund alikotua dirisha lililopita kwa mkopo wa nusu msimu. Sancho ameendelea kushikilia msimamo wake wa kutaka kuondoka Man United ikiwa Erik ten Hag ataendelea kuwa kocha wa timu hiyo.

VIGOGO kutoka Ligi Kuu ya Marekani, San Diego, wamepanga kutuma ofa kwenda PSV Eindhoven ili kuipata saini ya winga wa timu hiyo, Hirving Lozano, 28, dirisha lijalo la majira ya kiangazi. San Diego ambayo pia inahusishwa na Olivier Giroud, inamtaka Lozano kutokana na kiwango bora alichoonyesha msimu uliomalizika na alicheza mechi 33 za michuano yote na kufunga mabao sita.

BAYERN Munich inataka kumsajili kiungo wa Paris Saint-Germain, Xavi Simons, ambaye msimu uliomalizika alicheza kwa mkopo RB Leipzig na katika mechi 43 za michuano yote alifunga mabao 10 nakutoa asisti 15. Xavi mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwaka 2027 na Bayern baada ya kukosa ubingwa inataka kurudisha makali yake chini ya Kocha Vincent Kompany.

BAADA ya kutajiwa bei yake, mabosi wa AC Milan wameachana na mpango wao wa kutaka kumsajili beki wa Tottenham, Emerson Royal dirisha hili. Awali Milan ilitaka kumsajili kwa sababu iliambiwa anauzwa Pauni 21 milioni, lakini imeshindikana baada ya Spurs kudai zaidi ya hapo. Kwa sasa Milan inaangalia uwezekano wa kumpata beki mwingine.

BAADHI ya timu za Ligi Kuu England zinatajwa kuwa kwenye mchakato wa kutaka kumsajili mshambuliaji wa AS Roma, Paolo Dybala dirisha hili. Dyabala ameonyesha nia ya kutaka kuondoka Italia na kutua England na taarifa zinadai kuna uwezekano akauzwa kwa zaidi ya Pauni 10.2 milioni kwa mujibu wa kipengele kilichopo kwenye mkataba wake.

Chanzo: Mwanaspoti