Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ansu Fati: Kutoka mrithi wa Messi mpaka mkopo Brighton

Brighton Na Ansu Fati Ansu Fati: Kutoka mrithi wa Messi mpaka mkopo Brighton

Sun, 3 Sep 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Nyota wa La Masia, Ansu Fati aliyerithi jezi namba 10 iliyokuwa ikivaliwa na mchezaji bora wa dunia, Lionel Messi amepoteza mvuto huko Catalunya na sasa ametua kwa mkopo Brighton ya Ligi Kuu England.

Kwa miezi 12, Ansu alionekana kuwa tayari kurithi jezi ya Messi. Alianza kucheza kwa mara ya kwanza Septemba 2019, na akakiwasha kwelikweli kwenye La Liga kwa karibu mwaka mzima.

Alivunja rekodi nyingi, alifunga kwa kiwango bora kuliko Messi alipokuwa na umri kama wake, alicheza soka la kiwango cha juu. Huyu ndiye nyota mpya wa Barcelona ambaye alikuwa akitazamwa, mtu ambaye Barca wangeweza kumtegemea kwa miaka mingi ijayo.

Au ndivyo ilionekana. Lakini kwa bahati mbaya akaandamwa na majeraha, alikubwa na majeraha ya goti, na alipata matatizo ya misuli. Miaka minne baada ya kucheza mechi yake ya kwanza, Fati sasa ameonyeshwa mlango wa kutokea kwa mkopo na Barcelona.

Lakini ni jinsi gani yote yalikwenda vibaya? Mwanaspoti linakuletea maisha ya Fati, ikiangalia jinsi mchezaji aliyewahi kutajwa kuwa mmoja wa wachezaji bora zaidi duniani sasa anatafuta pahali pengine kwa ajili ya kusimama tena mbali na Catalunya.

Julai 24, 2019: Kwenye mstari wa nukta

Fati alikuwa sehemu muhimu ya timu za vijana za Barca kwa muda mrefu wa 2018-19, na mpango ulikuwa kwamba kijana huyo acheze msimu ujao wa Barca B katika daraja la pili la Hispania, kabla ya kupandishwa kwenye kikosi cha kwanza msimu unaofuata.

Lakini ilipobainika kuwa Barca ilihitaji huduma yake mbele, basi alisainishwa kwa haraka mkataba wake wa kwanza kama mchezaji wa kulipwa. Hivyo ilianza kupanda kwa kasi.

Agosti 25, 2019: Kuvunja rekodi mara ya kwanza

Barcelona ilihitaji kuimarishwa mwanzoni mwa msimu wa 2019-20, na Fati lilikuwa jibu sahihi zaidi kati ya safu za akademia huku Luis Suarez na Messi wote wakiwa wamejeruhiwa, Barcelona ilimgeukia kinda huyo wa miaka 16  akitokea benchi.

Dhidi ya Real Betis kwenye Uwanja wa Camp Nou, Fati aliingia kwenye mchezo dakika ya 78, na kuisaidia timu hiyo kuibuka na ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na Antoine Griezmann. Akiwa na miaka 16 na siku 298, Fati alikuwa mchezaji wa pili mwenye umri mdogo zaidi kucheza La Liga katika historia ya klabu hiyo.

Agosti 31, 2019: Kwenye orodha ya wafungaji

Wiki moja baadaye dhidi ya Osasuna, Fati alipata bao kwa mara ya kwanza akipokea krosi ya Carles Perez na kutumbukiza mpira wavuni.

Umaliziaji wake mzuri haukutosha kuisaidia Barca kushinda kwani walitoka sare ya mabao 2-2, lakini ilimfanya kuwa mfungaji wa bao mdogo zaidi katika historia ya klabu hiyo.

Septemba 14, 2019: Mwanzo wa kwanza wa kukumbukwa

Kinda huyo alifanya vya kutosha katika wiki zilizofuata kuthibitisha alistahili nafasi kikosi cha kwanza na Fati alianza kucheza dhidi ya Valencia, huku Suarez akianzia benchi, alikuwa sehemu ya washambuliaji watatu wa mbele wa Barca.

Ilikuwa ni utendaji wa ndoto kutoka kwa kijana wa miaka 16 wakati huo. Ndani ya dakika saba, alikuwa amefunga na kutoa pasi na kumfanya kuwa mchezaji bora wa mchezo huo wakiibuka na ushindi wa mabao 5-2.

Asisti yake, hasa, ilikuwa ya kuvutia, winga huyo akiwapita mabeki wawili upande wa kushoto kabla ya kurudisha mpira kwa Frenkie de Jong.

Desemba 10, 2019: Mvunja rekodi wa Ligi ya Mabingwa

Barca walichukua uongozi wa mapema dhidi ya Inter katika Ligi ya Mabingwa mapema Desemba 2019. Romelu Lukaku, hata hivyo, alisawazisha kabla ya mapumziko, kumaanisha Barcelona  ilihitaji  bao lingine ili kupata ushindi muhimu wa ugenini  huko San Siro.

Fati alitokea benchi na kufanya maajabu yake, akipiga shuti la chini chini kwenye kona ya chini kutoka ukingo wa goli.

Lilikuwa bao la kukumbukwa na lililomfanya kuwa mfungaji wa bao mdogo zaidi katika historia ya Ligi ya Mabingwa, rekodi anayoishikilia hadi sasa.

Septemba 3, 2020: Heshima ya Kimataifa

Baada ya Fati kuwa kwenye kiwango bora, alipata shavu la kuitwa timu ya taifa la Hispania.

Septemba 6, 2020: Mambo yajipa Hispania

Luis Enrique alimpa kinda huyo wa miaka 17 mchezo wake wa kwanza wa kimataifa dhidi ya Ukraine na alifunga moja ya mabao bora zaidi maishani mwake hadi sasa, akitumia mguu wake wa kulia wenye nguvu na kuachia mkwaju kutoka nje ya eneo la hatari.

Oktoba 24, 2020: Historia El Clasico

Mchezo wa Clasico uliofanyika Oktoba 2020 haukuwa wa kukumbukwa kwa Barcelona. Klabu hiyo ya Catalan ilichapwa na Madrid mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Camp Nou.

Lakini Fati alionyesha ubora wake. Winga huyo alijipenyeza ndani ya eneo la goli na kumalizia krosi iliyochongwa vizuri na Jordi Alba na kusawazisha na kumfanya kuwa mfungaji wa pili mwenye umri mdogo katika historia ya mechi hiyo.

Novemba 9, 2020: Alifanyiwa upasuaji

Hapa ndipo majanga yalipoanza kumuandama. Winga huyo alikuwa amekumbwa na majeraha ya goti hivyo jopo la madaktari wa Barcelona liliamua afanyiwe upasuaji ambao ulimweka nje ya uwanja kwa zaidi ya wiki sita.

Januari 4, 2021: Awamu nyingine ya upasuaji

Miezi miwili baadaye, goti lilionyesha dalili chache za kupona, na mshono ulishindwa kusaidia majeraha yake kupona. Kwa hivyo, Fati alifanyiwa upasuaji mwingine, ulioelezewa na klabu kama “matibabu ya kibaolojia ya kuzaliwa upya”.

Machi, 2021: upasuaji wa tatu

Maumivu ya goti yaliendelea na mara tu ya mshono wa Fati uliposhindwa kupona vizuri kwa mara ya pili, akachagua kufanyiwa upasuaji wa tatu.

Hilo halikufaulu, aliendelea kupata maumivu na uvimbe katika goti lake la kushoto. Baadaye aliachana na daktari ambaye alikuwa amekamilisha upasuaji wa tatu wa kwanza, akajitenga hadi mwisho wa msimu wa 2020-21 na kutafuta njia nyingine ya matibabu yake.

Mei, 2021: Suluhisho?

Mwisho wa msimu wa 2021, Fati hatimaye alikubali ushauri wa wale walio karibu naye. Meniscus ‘kipande chenye umbo la C ambacho hufanya kama mto kati ya shinbone (tibia) na paja (femur)’ ilikuwa bado haijajiunganisha ipasavyo, na hakuwa na chaguo ila kuondoa nyuzi.

Ilikuwa ni utaratibu wa kawaida, lakini ambao ulionekana kuwa unaweza kusababisha matatizo ya muda mrefu. Fati angelazimika kutunza vyema goti lililoathiriwa na misuli inayozunguka ili kuepuka kuumia zaidi. Hata hivyo upasuaji huo ulikuwa wa nne katika miezi sita. 

Septemba 2021: Kurithi jezi ya Messi

Pamoja na hayo yote, Fati bado alikuwa akiungwa mkono na klabu na baada ya jezi namba 10 kuachwa wazi wakati Messi alipolazimika  kuondoka kwenda Paris Saint-Germain msimu wa joto wa 2021, Barca walimpa kinda huyo.

Oktoba 20, 2021: Mkataba mpya wa muda mrefu

Barca walithibitisha tena imani yao kwa mchezaji huyo kwa kumpa Fati nyongeza ya mkataba kubwa, na kumfungia hadi 2027.

Novemba 1, 2021: Maumivu zaidi ya jeraha

Kiwango cha Fati kilionekana kuanza kupungua, ingawa mshambuliaji huyo alifunga mara mbili katika mechi sita kabla ya kupata jeraha lingine. Wakati huu, lilikuwa ni tatizo kubwa la misuli katika paja lake la kushoto, aina ya suala ambalo madaktari walihofia wakati sehemu ya ‘meniscus’ yake ilitolewa miezi michache hapo awali.

Machi 28, 2023: Je! huu ni mwisho wake?

Kila kitu kilikuwa sawa kwa Fati Machi 2023 chini ya Xavi, winga huyo alikuwa akipewa nafasi lakini kadiri ambavyo muda ulikuwa ukisogea mambo yaligeuka huku kwa sasa kocha huyo akionekana kuanza kuwa na imani zaidi  na  Lamine Yamal mwenye umri wa miaka 16 na ndiye anayetezamwa kwenye kikosi hicho kama Messi ijaye kutokana na kile anachokifanya.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: