Uongozi wa Simba umeweka wazi kuwa makosa makubwa ambayo yamefanya anguko kwenye timu hiyo hajaanza leo bali miaka miwili nyuma.Msimu huu Simba imepoteza matumaini ya kutwaa taji la ligi linalotetewa na Yanga iliyo nafasi ya kwanza na pointi 71.Leo ina kibarua cha kusaka ushindi dhidi ya Ruvu Shooting mchezo unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa Azam Complex.
Ni mastaa wawili ambao wametajwa kuvuruga mipango yao ambao ni Clatous Chama na Luis Miquissone baada ya kuondoka kwao ghafla.
Luis kiungo wa kazi ngumu alisepa na kuibukia Al Ahly ya Misri huku Chama yeye akiibukia RS Berkane ya Morroco kabla ya kurudi kwa mara nyingine ndani ya Simba.
Kupitia mahojiano maalumu na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba SC, Salim Abdallah ‘Try Again’ kupitia Azam TV kiongozi huyo amebainisha hayo.
Try Again amesema:”Wengi wanaangalia anguko letu kwa sasa lakini anguko letu lilianza miaka miwili nyuma baada ya kuwaruhusu kuondoka Chama na Luis halafu hakukuwa na mbadala wao.
“Watu ambao walikuja walishindwa kufanya yale yaliyofanywa nao hivyo tunajipanga kuangalia ni namna gani tutafanya maboresho kwenye kila idara ya timu ili kuwa bora,” amesema.
Tayari Chama amerejea kikosi cha Simba ametoa pasi 14 za mabao huku kukiwa na tetesi kuwa wapo kwenye mpango wa kumrudisha Luis kwa mara nyingine tena.