Imefahamika kuwa Meneja wa Klabu Bingwa nchini Hispania Real Madrid Ancelotti Carlo aliwawakia wachezaji wake katika chumba cha kubadilishia, baada ya mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Girona uliopigwa mwishoni mwa juma lililopita.
Real Madrid ambayo imeuweka rehani Ubingwa wa La Liga msimu huu, ikitanguliwa na FC Barcelona kwa tofauti kubwa ya alama, ilipoteza mchezo dhidi ya Gerona kwa kuchapwa mabao 4-2.
Real Madrid ilikubali kichapo hicho juzi katika mchezo wa Ligi Kuu ya Hispania (La Liga), uliochezwa katika Uwanja wa Municipal de Montilivi nchini Hispania.
Imeelezwa kuwa Kocha Ancelotti alichukizwa na kiwango cha wachezaji wake na kufikia hatua ya kusemea maneno makali kwa madai ya kuonesha viwango duni katika mchezo huo.
Hata hivyo alipozungumza na Waandishi wa Habari baada ya mchezo huo, Meneja huyo kutoka nchini Italia alisema wachezaji walicheza chini ya kiwango, hali iliyosababisha wapoteze alama tatu.
“Levo yetu ilikuwa chini sana. Tunaomba radhi, timu haikucheza kabisa. Tulikuwa vibaya katika kujilinda na huo ndiyo ulikuwa msingi wa kupoteza,” alisema.
Ancelotti alikiri mashabiki wa timu hiyo hawatokuwa na furaha kutokana na kichapo hicho dhidi ya timu ambayo msimu uliopita haikuwa La Liga.
Baada ya kichapo hicho Real Madrid, inashika nafasi ya pili ikiwa na alama 65 katika michezo 31 wakati Girona inashika nafasi ya tisa ikiwa na alama 41.