Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ancelotti: Sitaingilia maamuzi yake

Luka Modric With Carlo Ancelotti Luka Modric na Carlo Ancelotti

Tue, 27 Feb 2024 Chanzo: Dar24

Kocha Mkuu wa Real Madrid Carlo Ancelotti amekiri ni vigumu kumuacha Luka Modric kwenye benchi baada ya kiungo huyo mkongwe kufunga bao zuri katika ushindi wa 1-0 wa Real Madrid dhidi ya Sevilla mwishoni mwa juma lililopita.

Modric mwenye umri wa miaka 38 ambaye ameanza mechi 11 pekee za ligi msimu huu aliingizwa kutoka benchi katika dakika ya 75 kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu na akafunga bao kwa shuti la mbali dakika sita tu baada ya kuingia.

Mkataba wa mchezaji huyo wa Kimataifa wa Croatia unatarajiwa kumalizika msimu huu wa majira ya joto, na kukosa muda wa kucheza msimu huu kumesababisha uvumi kuwa anaweza kuchagua kuhama baada ya miaka 12 ya kukaa na Madrid.

“Modric alistahili leo (juzi),” amesema Ancelotti

“Alifunga bao zuri. Alichangia sana alipoingia, alileta hali mpya. Ni vigumu kumuacha kwenye benchi. Jinsi anavyofanya mazoezi kila siku, ni mfano kwa kikosi kizima,”

Ancelotti amesema kuwa Modric, Toni Kroos pamoja na Nacho Fernandez, ambao mikataba yao pia inakamilika msimu huu wa majira ya joto wamepata haki ya kuamua mustakabali wao wenyewe.

“Modric, Kroos, Nacho wote wako katika hali moja,” alisema Ancelotti.

“Siingilii katika hilo, Klabu ina muda wa kutatua hayo yote miezi michache ijayo.. kutokana na heshima niliyonayo kwa Modric siwezi kumpa ushauri, ana akili sana, anajua vizuri kabisa kile anachopaswa kufanya.”

Modric ameshinda mataji 24 akiwa na Madrid yakiwamo matano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini anakabiliwa na ushindani ulioongezeka katika safu ya kiungo msimu huu kutoka kwa vijana Jude Bellingham, Eduardo Camavinga, Fede Valverde na Aurelien Tchouameni, pamoja na Kroos, ambaye amekuwa katika kiwango bora.

Chanzo: Dar24