Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ancelotti: Mbappe atacheza hivi real

Mbappe X Acelotti Ancelotti: Mbappe atacheza hivi real

Sat, 27 Jul 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Baada ya Kylian Mbappe kusajiliwa na Real Madrid katika dirisha la majira kiangazi linaloendelea akitokea PSG, moja kati ya maswali yaliyoibuka ilikuwa eneo gani atacheza na sasa kocha wa kikosi hicho, Carlo Ancelotti amejibu.

Kiasili Mbappe anacheza zaidi eneo la winga wa kushoto ambalo katika kikosi cha Real Madrid mwenye namba yake ni Vinicius Jr.

Akizungumza na The Obi One Podcast, Ancelotti aliulizwa wapi Mbappe atacheza, na akasema: “Naona akicheza nafasi ya mshambuliaji pale na nafikiri kitu muhimu zaidi katika eneo la ushambuliaji ni kuwa na mchezaji anayehama asiyekaa eneo moja.”

“Nikikuuliza Vinicius alicheza wapi msimu uliopita ni ngumu kusema, hakucheza kama winga wa kushoto. Wakati mwingine alicheza upande wa kushoto wakati mwingine katikati.

“Bellingham pia kuna muda alicheza upande wa kushoto wakati mwingine alicheza katikati, wakati mwingine kulia. Rodrygo alianza michezo mingi upande wa kulia lakini muda mwingine mchezo ulipokuwa unaendelea alikuwa akibadilika na kwenda upande wa kushoto, hili ndilo jambo muhimu.

“Nataka kuwapa wachezaji wangu uhuru. Tuliwahi kucheza mchezo mmoja dhidi ya Man City huku Rodrygo na Vinicius wakiwa upande wa kushoto kwa sababu tulidhani tunaweza kupata kitu kwa wao kucheza eneo hilo.”

Vilevile Ancelotti aliulizwa jinsi anavyoweza kumuingiza Mbappe na timu kwa ujumla, akajibu: “Mbappe kuingia kwenye timu haitakuwa tatizo jambo muhimu ni yeye mwenyewe kuhakikisha anaendana na timu na kuhakikisha anajitoa kwa asilimia kubwa kwa ajili ya timu.” Mbappe sio sehemu ya kikosi cha Real Madrid kilichopo Marekani kujiandaa na msimu mpya baada ya kupewa mapumziko kutokana na jeraha la pua alilopata katika Euro 2024.

Chanzo: Mwanaspoti